ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, August 16, 2012

MABONDIA KUONESHANA UBABE IDD MOSI TANGA


Bondia Bonzo (63) akitoa tambo baada ya kumpiga bondia chipukizi James Martin (22) ambae ni sawa na mwanae wa tatu. Kulia ni Ibrahim Kamwe na kushoto ni Yasin Abdallah-Ustadh. Bondia huyu atazipiga siku ya Idd Mosi.
Mohamed Bonzo anayesemekana kuwa ndiye bondia mzee kuliko wote nchini, wakati wa pambano lake na  James Martin.
Kampuni ya Mwazoa Promotions ya Tanga chini ya Mkurugenzi wake, Ally Omari inaendeleza na mkakati wake wa kunyanyua vipaji vya wanamichezo wa Jiji la Tanga hasa katika mchezo wa ngumi kwa mapambano ya ubingwa wa Afrika Mashariki yatakayopigwa Idd Mosi na Idd Pili.

Ally Omari 'Mwazoa' amemuhakikishia katibu mkuu wa ngumi za kulipwa nchini, Ibrahim Kamwe 'Bigright' kuwa maandalizi ya mapambano yote yamekamilika na mabondia wapo katika hali nzuri.
Mapambano hayo yatafanyika katika Ukumbi wa CCM, ambapo Said Mundi wa Tanga atazipiga na
Habibu Pengo wa Dar es Salaam katika kuwania ubingwa wa Taifa wa TPBC uzito wa Super Feather raundi kumi, naye Jumanne Mohammed wa Tanga atazipiga na Ally Bugingo wa Dar es Salaam katika uzito wa Light Weight raundi kumi, katika uzito wa Super Fly, Haji Juma(Tanga) na Mwaite Juma (Dsm) watacheza raundi nane na mapambano mengineyo mengi ya utangulizi wa mabondia watakaotoka katika vitongoji mbalimbali vya Jiji la Tanga.
Idd Pili katika Ukumbi wa Pweza kutakuwa na pambano kubwa la ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati, kati ya Alen Kamote wa Tanga na bondia kutoka Uganda, hili ni pambano la raundi kumi ambapo Zuberi Kitandula wa Tanga atazipiga na Sadiki Abdul Azizi wa Dar es Salaam raundi kumi, Jay Jay Ngotiko wa Tanga atapigana na bondia Juma Afande kutoka Morogoro, pia kutakuwepo na mapambano mengine ya utangulizi ya mabondia wakongwe wa Tanga na wale chipukizi takribani mabondia wote wa kulipwa wa Tanga watapata nafasi ya kupimana ubavu na wapinzani wao. Mwazoa alimalizia kwa kusema hizi ni mbio za kuyakusanya mataji yote ya Tanzania na Afrika Mashariki yafike Tanga na tayari mpaka sasa ina mabingwa sita wa Tanzania na mmoja wa Afrika mashariki.

No comments: