ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, August 23, 2012

Makarani wagoma kula kiapo, wengine wakosa majina yao

Katika hali ya kushangaza, makarani watakaofanyakazi ya sensa katika Kata ya Kibamba jijini Dar es Salaam jana waliibua taharuki kubwa baada ya kugoma kula kiapo wakidai kulipwa posho ya kazi hiyo.

Makarani hao ni wale waliokuwa wakishiriki mafunzo ya sensa.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, mmoja wa makarani hao, Aneth Johh, alisema wamefikia maamuzi ya kufanya mgomo wa kula kiapo kutokana na kwamba hawajalipwa posho na kwamba waliohofia kutekeleza jambo hilo kwa nia ya kushinikiza malipo.


Baada ya mgomo huo, majira ya mchana mhasibu alifika na kuanza kuwalipa jambo lililomaliza mgomo na hivyo makarani walikula kiapo.

Karani huyo alisema wamekuwa kwenye mafunzo kwa siku saba na walilipwa Sh. 140,000 hivyo walikuwa wakidai Sh. 105,000.

Katika maeneo mengine jijini, malipo ya posho hizo yalifanyika kuanzia mapema jana huku zoezi hilo likikubwa na mizengwe na kasoro kadhaa ikiwemo majina ya baadhi ya makarani kutoonekana katika orodha ya malipo.

Malipo hayo ambayo yameanza kufanyika  katika kituo cha Shule ya Sekondari Kambangwa katika Manispaa ya Kinondoni, yaingia dosari kufuatia majina ya makarani wa Kata ya Tandale kukosekana kwenye orodha ya malipo hayo na hivyo kuzua malalamiko.

Juzi makarani hao waligoma kupokea kiasi cha Sh.140,000 wakishinikiza kulipwa posho yao yote ya siku saba ambayo ni Sh. 245,000.

Mmoja wa makarani hao aliyefanikiwa kulipwa Edward John kutoka kituo cha Makumbusho alisema wamelipwa Sh. 140,000, ambazo waligoma kuzipokea juzi ambapo wameambiwa kiasi cha Sh.105,000 kilichobakia watalipwa baadae.

Aidha Makarani wanne waliosadikika kuwa viongozi wa kugomea posho hizo juzi walienguliwa kwenye orodha ya malipo na kukilalamikia kitendo hicho kuwa sio cha kiungwana kwani, wao walishiriki kwenye semina mwanzo mpaka mwisho hivyo walistahili malipo hayo.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Fortnatus Fweme, alisema bado hajapata taarifa za kuenguliwa kwa makarani hao kwenye orodha ya malipo, pamoja na kutokuwepo kwa majina ya makarani wa Kata ya Tandale.

Kwa upande wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, malipo kwa makarani hao yameendelea kama kawaida.

Katika kituo cha shule ya msingi Miti Mirefu Banana, Mwenyekiti wa Kamati ya mafunzo, Mohamed Mcheni, alisema kuwa japo  wahasibu walifika kwa kuchelewa lakini wanaendelea kufanya malipo kwa makarani waliobaki ambapo wanalipwa Sh. 140,000.

Mcheni alisema juzi walianza kuwalipa  makarani wenye dodoso ndefu yaani wenye maswali 67 ambao walichukua mafunzo yao kwa muda wa siku 10, wenye dodoso fupi ambao ni zaidi ya 1,000 wanaendelea kulipwa kituoni hapo.

Mara baada ya kukamilisha kulipa posho hizo hatua itakayofuata,  watapatiwa vifaa kwa ajili ya zoezi la uandikishaji ambalo litadumu kwa siku saba.

Ofisa Uhamasishaji wa Sensa nchini Said Ameir alisema kuwa zoezi hilo ni muhimu kwa taifa,hivyo kila mmoja anahusika  katika kuhakisha lengo linafikia.

Imeandikwa na Beatrice Shayo, Samson Fridolin na Leonce Zimbandu.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: