ANGALIA LIVE NEWS

Monday, August 13, 2012

Moyo sasa abanwa Z'bar kauli yake ya Muungano


Waziri wa zamani wa
Serikali ya Muungano,
Hassan Nassor Moyo


Baraza  la Wazee wa CCM na UVCCM, wameitaka jamii kuyatahadhari matamshi yanayotolewa na Waziri wa zamani wa Serikali ya Muungano, Hassan Nassor Moyo, kuhusu mwelekeo na hatma ya Tanzania.

Wakizungumza na NIPASHE kwa nyakati tofauti, Wazee na UVCCM walimtaka Mzee Moyo kuyatafakari maoni yaliotolewa hivi karibuni na  Mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu Julius Nyerere, Profesa Issa Shivji.

Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa CCM Zanzibar (BWCZ), Makame Mzee Suleiman, alisema matamshi ya Shivji yana msingi ili kulilinda Taifa lisibomoke kinyume na mtazamo wa Moyo.



Akiyazungumzia matamshi ya Mzee Moyo alidai yanaweza kutafsiriwa na wana jamii kama yanayotaka kulisambaratisha Taifa ambalo limejengeka kwa misingi ya umoja wa kitaifa.

Mwenyekiti huyo wa Wazee Zanzibar, alisema hatakiwi kuyakebehi mawazo ya waasisi wa Muungano ila kuuheshimu uoni wa kitaalam wa Shivj kwa utulivu na historia.

“Mzee mwenzangu hapaswi kuponda mawazo ya  waasisi wetu, ana wajinu na ulazima wa kuyatafakari kwa kina maoni ya Shivji kuhusu hatma ya Muungano wa Serikali mbili,” alisema.

Akieleza kwa upole, alisema maoni yasiozingatia chimbuko, asili na sababu ya kiungwana kwetu anaweza kulizamisha Taifa lake katika dimbwi la mivutano badala ya kuliokoa Taifa alioitumikia kwa heshima na uaminifu.

Mzee Suleiman ambaye aliwahi kuwa Katibu wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar kwa miaka kadhaa, alisema kusudio la Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Amani Karume ni kupata Taifa moja lenye umoja, nguvu za kiuchumi na kisiasa.

Alisema nia ya Mzee Karume na Nyerere ilikuwa ni kujenga Taifa moja la mfano Afrika Mashariki ambalo halitakuwa  athari zilizopandikizwa na wakoloni za ubaguzi wa rangi, dini na ukabila.

“Hapa Zanzibar wakoloni walitugawa kwa matabaka,  Karume alichukia sana ubaguzi, ubwana, umwinyi na ukabila ,Moyo ajaribu kuweka akiba ya maneno yake, amaana akiba haiozi," alieleza.

Kwa upande wa UVCCM Zanzibar, Kaimu Naibu Katibu Mkuu wake, Jamal Kassim, alisema maelezo ya Mzee Moyo yameligawa kundi ya vijana katika mtazamo wa utengano.

Alisema hilo si jambo jema kwa mtu kama yeye anaeheshimika kutokana na utumishi wake katika Serikali zote mbili za SMZ na SMT kuhesabika hivyo.

Kassim alisema akumbuke anapotoa matamshi ya mkanganyiko ni sawa na kujaribu kumwaga maji ardhini akitarajia anaweza kuyazoa hapo baadaye.

“Mzee Moyo atambue maji yakimwagika hayazoleki, hasara yake itakapochomoza haitachagua jina la mtu, kundi au chama cha siasa, hasara huwa ni hasara milele, aliasa.

Aidha, Kiongozi huyo wa UVCCM Zanzibar aliwataka wanachama wa CCM kuzizungumzia kero zilizopo katika Muungano na ikibidi baadhi ya mambo ya Muungano yaondolewe bila ya kuutikisa Muungno uliopo.

“Muungano ni kama moyo wa amani na utulivu wetu, nje ya Muungano kunaweza kutokea mtikisiko mkubwa, kwanini tusizungumzie kuziondoa kero ila kutaka  Muungano wa mkataba, hapa lipo jambo gani?,” Alihoji.

Tangu kuundwa kwa Tume ya kuratibu maoni ya Muungano, kumeibuka kikundi Zanzibar kinachofanya kampeni za Zanzibar kujitenga katika Muungano wakiungwa mkono na baadhi ya viongozi wa chama na serikali Zanzibar.

CHANZO: NIPASHE

No comments: