ANGALIA LIVE NEWS

Friday, August 24, 2012

MUHONGO ASEMA TUTAENDELEA KUSAFIRISHA MCHANGA WA DHAHABU NJE YA NCHI


 Profesa Sospeter Muhongo
WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, amesema Serikali itaendelea kusafirisha mchanga ya madini nje ya nchi ili ukafanyiwe uchunguzi kutokana na ukosefu wa maabara zenye uwezo wa kubaini aina mbalimbali za madini nchini.


Alisema kusafirishwa kwa mchanga huo, si wizi bali hali hiyo inachangiwa na ukosefu wa vifaa vya kisasa vyenye uwezo wa kuchambua aina tofauti za madini.


Prof. Muhongo aliyasema hayo juzi wakati akihitimisha ziara yake katika Wilaya ya Bunda, mkoani Mara waakati akijibu swali la mkazi wa Kijiji cha Mwibara, Bw. Qudra Maalim.

Bw. Maalim alitaka kujua sababu ya mchanga ya dhahabu kutoka migodi mbalimbali kusafirishwa kwa ndege kwenda nchi za nje ambapo Prof. Muhongo alisisitiza kuwa, si Tanzania pekee inayofanywa bali nchi nyingi zinasafirisha mchanga huo.

“Serikali itaendelea kusafirisha mchanga huu wakati ikiendelea kutafuta njia mbadala, katika migodi mingi ya dhahabu yapo madini mengine kama shaba, fedha na kopa.

“Madini haya unaweza kuyakuta katika michanga ya dhahabu na suluhisho pekee la kutopeleka michanga nje ni kujengwa maabara za kisasa zenye uwezo wa kufanya uchambuzi,” alisema.

Aliongeza kuwa, maabara zilizopo zina uwezo wa kubainisha dhahabu katika miamba ya madini kwa asilimilia 40 hivyo ili kufiki asilimia 100 ya uchambuzi huo, asilimia 60 ya michanga itokanayo na miamba hupelekwa nje kuchambuliwa kwenye maabara za kisasa.

Alizitaja baadhi ya nchi zenye maabara za kisasa kuwa ni Ujerumani na Marekani ambapo pamoja na kufanya kazi ya madini nchini, hajawahi kutumia maabara kuchunguza miamba ya madini kwa sababu uwezo wake ni mdogo.

“Niseme ukweli kwamba, mimi nilisoma katika nchi zenye maabara ya hali za juu kama Ujerumani, pamoja na kufanya shughuli za nishati na madini, sijawahi kutumia vipimo vya mahabara zilizopo nchini kwetu, huu ndio ukweli,” alisema Prof. Muhongo.

No comments: