Thursday, August 23, 2012

Ndugai aasa itungwe sheria kuwabana wabunge watoro




Tatizo  la utoro kwa baadhi ya wabunge kwenye vikao vya Bunge limemfanya Naibu Spika wa Bunge, Job Ndungai, awaombe wananchi kutoa maoni kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ili suala hilo liwe sheria.

Ndugai amesema suala hilo likitungiwa sheria litawezesha wabunge wasiohudhuria vikoa vya Bunge wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria hiyo.

Alitoa ushauri huo wakati akihojiwa jana na Radio One katika kipindi kilichokuwa kinataka wananchi watoe maoni hatua gani zichukuliwe kukomesha tatizo la utoro wa wabunge bungeni.



Alisema ili kukomesha tatizo hilo ambalo limekuwa sugu kwa baadhi ya wabunge pamoja na kuwepo kwa kanuni za bungeni, linatakiwa liwepo ndani ya Katiba ili iwe sheria.

Ndugai alisema ili kufanikisha hilo, wananchi watoe mapendekezo yao kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ili liingizwe kwenye Katiba ijayo.

"Kimsingi, suala la utoro wa wabunge bungeni limekuwa sugu kwa baadhi ya wabunge lakini kinachotakiwa ni wananchi watusaidie kwa kutoa maoni kwenye Tume ya Jaji Warioba, ipo kanuni tu inayosema mbunge asipohudhuria mikutano mitatu ya Bunge anapoteza ubunge, lakini suala la mbunge anayetoroka vikao halijazungumzwa," alisema.

Kuhusu madai ya baadhi ya wabunge kutaka vikao vya Bunge visiwe vinaonyeshwa kwenye runinga, Ndungai alisema ofisi ya Bunge haitalifanyia kazi suala hilo kwa sababu wabunge wanaopendekeza hicho ni wachache.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (Tucta), Nicholaus Mgaya,  alisema njia pekee ya kukomesha tatizo hilo ni kutungwa kwa sheria rasmi itakayowalazimisha wabunge kuhudhuria vikao vya Bunge pamoja na kuwakata posho wasiohudhuria vikao hivyo.

“Wapo wabunge wakati wa vikao badala ya kwenda bungeni wanakwenda kunywa pombe, sasa ifike wakati itungwe sheria rasmi ya kuwalazimisha waende bungeni,” alisema.

Mgaya alisema tatizo hilo la utoro wa wabunge pengine ndilo hata lililochangia kupitisha kwa sheria ya mifuko ya hifadhi kwa mafao ya wafanyakazi ambayo ni kandamizi.

Naye Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR Mageuzi), David Kafulila, alisema suala la mbunge kuhudhuria vikao ni wajibu wake lakini inakuwa ni aibu kwa mbunge asiyekuwa na dharura yeyote kuamua kukacha vikao kwa makusudi.

Mapema Julai 15, mwaka huu, Spika wa Bunge, Anne Makinda, aliwashukia wabunge wanaokimbia vikao vya Bunge na kusema kama tabia hiyo itaendelea, ipo siku serikali itashindwa kupitisha bajeti yake.

“Wakati wa kupitia vifungu kwenye Kamati ya Matumizi ya Wizara, ni muhumu wabunge wote tuwepo, ipo siku tutashindwa kupitisha bajeti,” alisema.

Tangu kuanza kwa vikao vya Bunge la Bajeti kilichomalizika hivi karibuni, mahudhurio ya wabunge hayakuwa ya kuridhisha na hivyo kusababisha wabunge wengi washindwe kuchangia.

Mathalani, kutokana na tatizo hilo, bajeti ya Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika ishindwa kupitishwa kutokana na idadi ndogo ya wabunge.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake