Thursday, August 23, 2012

Okwi aipasua kichwa Simba




Mshambuliaji  Mganda Emmanuel Okwi jana alianza mazoezi na timu yake ya taifa ya Uganda 'The Cranes' kwa ajili ya maandalizi ya mechi yao ya kirafiki dhidi ya Botswana keshokutwa Jumamosi, licha ya uongozi wa klabu yake ya Simba kumkatalia jambo hilo.
Uongozi wa Simba juzi ulikataa ombi la Shirikisho la Soka la Uganda (FUFA) la kumtaka Okwi kubaki nchini humo kwa ajili ya mechi hiyo ya kirafiki ambayo haimo katika ratiba ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).

Uganda inatarajia kucheza dhidi ya Botswana baada ya mechi yao ya kalenda ya FIFA dhidi ya Malawi iliyopangwa kufanyika Jumatano iliyopita kuvunjika kufuatia wageni hao kuhofia ugonjwa wa Ebola.



Kocha wa The Cranes, Bobby Williamson, aliiambia NIPASHE jana kuwa Okwi ameungana na wenzake kwa ajili ya kujiandaa na mechi hiyo ya Jumamosi.

Bobby alisema kwamba jana asubuhi Okwi alikuwa mmoja wa wachezaji aliowaongoza kwenye mazoezi na kwamba taarifa za mshambuliaji huyo kuondoka kurejea Dar es Salaam hakupewa na viongozi wa FUFA.

Okwi hajafanya mazoezi na Simba tangu msimu wa ligi uliopita ulipomalizika ambapo pia hakuichezea timu yake hiyo kwenye mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) baada ya kuondoka kwa nia ya kwenda kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa nchini Austria.

Mganda huyo alirejea katika sherehe za Simba Day lakini hakuweza kucheza kutokana na kutokuwa fiti na aliishuhudia timu yake ikifungwa magoli 3-1 na Nairobi City Stars ya Kenya siku hiyo.

Katibu Mkuu wa Simba, Evodius Mtawala, ambaye juzi alisema kuwa walipokea barua kutoka FUFA inayomtaka Okwi abaki nchini Uganda na kwamba wamekataa ombi hilo, alisema jana kuwa bado hajapata taarifa mpya kuhusu suala la Okwi.

Wakati huo huo, Simba itacheza mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya AFC Leopards ya Kenya kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Amri Abeid jijini Arusha Jumapili.

Akizungumza na gazeti hili jana, Afisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga, alisema kuwa maandalizi ya mchezo huo yanaendelea na tayari wameshapata kibali cha kutumia uwanja huo ambao hivi karibuni ilielezwa kwamba uko kwenye matengenezo na kusababisha mechi za Ligi ya Super8 kuhamishiwa Moshi.

Kamwaga alisema kuwa AFC Leopards watawasili Arusha kesho Ijumaa tayari kwa mchezo huo wenye lengo la kukiimarisha kikosi cha Simba kinachojiandaa na mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Azam.

Alisema kwamba kabla ya ligi kusogezwa mbele kocha Milovan Cirkovic alihitaji kupata mechi moja ya kirafiki lakini baada ya ligi hiyo kusogezwa mbele huenda Simba ikacheza mechi mbili dhidi ya timu ngumu.

"Kocha amesema anataka mechi ngumu ambazo zitawapa mazoezi wachezaji wake na hachagui timu, kwake timu bora ndio chaguo la kwanza," alisema Kamwaga.

 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake