ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, August 11, 2012

OPERESHENI SANGARA YAANZA KWA KISHINDO MOROGORO


Dr. Slaa
Na Ashton Balaigwa
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeitikisa wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro baada ya kufanya mkutano mkubwa wa wa kampeni ya  vuguvugu la mabadiliko (M4C) huku ikiitaka Serikali  kutowafumba midomo wabunge kuzungumzia maslahi ya walimu pamoja madaktari.

Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika katika mji wa Ifakara, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, alisema wabunge ni sauti ya wananchi hivyo hawapaswi kuzibwa midomo katika kuzunguzia matatizo yanayowakabili Watanzania kwa kuwa ndiyo waliowachagua.

Alitolea mfano mgomo wa walimu uliotikisa nchi nzima na baadaye kusitishwa kwa amri ya mahakama na mgomo wa madaktari kuwa ni baadhi ya matokeo ya kupuuzwa kwa haki na maslahi ya wananchi.

Dk. Slaa alisema Chadema itaendelea kupiga kelele katika mikutano yake yote juu ya kero za wananchi huku ikiwataka wananchi kuunga mkono katika kampeni yake ya M4C yenye lengo la kuleta mabadiliko ya mfumo wa kisiasa nchini kwa lengo la kuboresha maisha ya Watanzania.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alisema kuwa chama hicho kimeamua kufanya uzinduzi wa kampeni za M4C wilayani Kilombero ikiwa ni ishara ya kumuenzi aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum, marehemu Regia Mtema, aliyefariki dunia kwa ajali ya gari miezi mitano iliyopita.

Alisema kampeni hiyo itakayopita katika vijiji 575, kata 180 na majimbo 10 ya Mkoa wa Morogoro, inalenga kuelimisha wananchi umuhimu wa kufanya mabadiliko katika mfumo wa kisiasa ili kuondokana na umasikini.

Mbowe alisema Watanzania wameumia vya kutosha kutokana na kero mbalimbali za kimaisha ikiwa ni pamoja na matatizo ya uhaba wa maji, umeme, elimu duni na gharama za kimaisha na kwamba kwa pamoja wanaweza kuzikataa kero hizo kwa kuunganisha nguvu zao ili kupinga unyanyasaji huo pasipo kumwaga damu.

Alisema zoezi hilo halihitaji Watanzania kuwa na fedha nyingi, isipokuwa ni moyo wa dhati wa kila mmoja kuchukua hatua pasipo woga ili kuleta mabadiliko katika nchi ya asali na maziwa.

"Sauti ya wengi ni sauti ya Mungu na kwamba jukumu hilo la kufikia mafanikio hayo si la Mbowe peke yake, Dk. Slaa wala Nassari, bali ni la Watanzania wote," alisema.

Naye Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, aliwataka wananchi kushiriki kikamilifu mchakato wa kuchangia maoni ya Katiba mpya huku akiwatadharisha wananchi kuona namna ya kupendekeza kupunguzwa kwa madaraka ya Rais.

Lissu alisema Katiba iliyopo sasa inampa madaraka makubwa Rais na kumfanya kuwa kama mfalme na kwamba katika Katiba ijayo kuwepo na fursa kwa Rais kushtakiwa anapofanya kosa.

Lissu alisema wananchi wanayo fursa ya kupendekeza kuchagua serikali inayowajibika kwa wananchi na kutokuwepo kwa nafasi za wakuu wa wilaya na mkoa kwani wanaingozea serikali gharama.

Kwa upande wake, Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari, alisisitiza juu ya azma ya chama chake kufanya mabadiliko yenye lengo la kuwaondolea umaskini Watanzania kupitia rasilimali zilizopo nchini.

Uzinduzi huo ulienda sambamba na maandamano yaliyopambwa na watembea kwa miguu, baiskeli, pikipiki na magari na kwamba utaendelea katika wilaya nyingine za Mkoa wa Morogoro.
Chanzo: Nipashe

2 comments:

Anonymous said...

That's what's up chadomo for life wapigieni mdomo hao wapate kuelewa ipasavyo. 2015 ushindi wa kishindo chadema my life.

Anonymous said...

Thanks sana makamanda wa chadema pipo now siku zinaelewa.kama kwawaida dr Slaa na makamanda wote piten kijijinkwa kijiji mtaa kwa mtaa 2015 CCM wataisoma namba