ANGALIA LIVE NEWS

Friday, August 17, 2012

PINDA ATAKA MWANAHALISI LIKATE RUFAA

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, amemtaka mtu yoyote asiyeridhika na uamuzi wa kulifungia gazeti la MwanaHalisi kukata rufaa katika vyombo vinavyohusika.

Alitoa wito huo jana wakati alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe (Chadema), katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo bungeni jana.



Mbowe alisema Julai 30, mwaka huu, serikali ililifungia gazeti la MwanaHalisi kwa muda usiojulikana kwa kutumia sheria ya magazeti ya mwaka 1976. Alihoji maadam katika siku za hivi karibuni serikali imetambua umuhimu wa Mahakama ni kwanini imelifungia gazeti hilo badala ya kulipeleka mahakamani na wahusika wapate nafasi ya kujitetea kabla ya hukumiwa?

Akijibu swali hilo, Pinda alisema ni kweli Serikali imechukua hatua hiyo, lakini imechukua hatua hiyo kwa kuzingatia sheria na taratibu za nchi.

Alisema mtu yoyote kwa msingi wa sheria hiyo anayeona hajatendelewa haki ni juu yake kukata rufaa kwa kuzingatia taratibu zilizopo. “Mimi nadhani ushauri mzuri ungekuwa ni huo,” alisema Pinda.

Katika swali lake la nyongeza,  Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, alisema sheria iliyotumika imekuwa ikilalamikiwa na wadau wengi na vyombo vya habari kwa muda mrefu ambayo inaipa mamlaka ya ziada serikali kuyadhibiti bila ya kuyasikiliza magazeti.

Alihoji iwapo Pinda haamini kwa kutumia sheria hiyo ni kunyima haki na ni msisitizo wa utawala usio bora?

Akijibu Pinda alisema: “ Mimi siamini hivyo kwa sababu sheria hiyo imetungwa na Bunge na kwa kuwa bado inatumia ni sheria halali, sisi tutaendelea kuitumia mpaka hapo itakapokuwa imerekebishwa.”

No comments: