Wednesday, August 22, 2012

Tenga amkatalia Rage kujiuzulu TFF


Rais  wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amekataa barua ya kuomba kujiuzulu ya Mjumbe wa Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji, Ismail Aden Rage.

Rage aliwasilisha barua ya kuomba kujiuzulu juzi katika ofisi za TFF juzi, akidai kwamba amefikia maamuzi ya kujiondoa kwenye kamati hiyo baada ya kuona mahasimu wao, Yanga wakipendelewa katika masuala mbalimbali, hasa yanayohusiana na usjaili wa wachezaji. 



Rage ambaye pia ni Mwenyekiti wa Klabu ya Simba, alimuandikia barua hiyo Rais wa TFF, Leodgar Tenga na kusema kuwa anajiuzulu kwa vile kamati hiyo imeshindwa kwa makusudi kusimamia sheria na kanuni za uendeshaji wa mchezo wa soka Tanzania.

Afisa Habari wa TFF, Boniface Wambura, alisema jana kuwa Tenga amekataa ombi hilo kwa maelezo kuwa kama Rage amehisi kuwepo udhaifu wa kutosimamia sheria na kanuni kama inavyotakiwa, ni vyema akaendelea kuwamo kwenye kamati hiyo ili kusaidia usimamiaji wa sheria na kanuni hizo kama inavyotakiwa na si kujiuzulu.

Wambura alisema kuwa Tenga amekataa maamuzi ya Rage kujizulu kwa sababu uzoefu na uwezo ambao Mwenyekiti huyo wa Simba anao katika uongozi wa mpira wa miguu unahitajika sana na kwamba, ni vyema akautumia kuisaidia kamati kutekeleza wajibu wake kama inavyotakiwa kwa mujibu wa sheria ili kusaidia kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya soka nchini.

Wambura alisema vilevile kuwa Tenga amesisitiza ni muhimu kwa mchezo wa soka kuongozwa kwa kufuata sheria na kanuni zilizopo, rai ambayo ameitoa pia kwa kamati zote za TFF ili kuhakikisha kuwa mpira wa miguu unaongozwa bila kuonea wala kupendelea upande wowote.

Tenga aliongeza kuwa, kamati zinapaswa kuchukua hatua zinazostahili bila woga pale kanuni zinapotaka hatua kuchukuliwa. Amezitaka kamati zisisite kwa namna yoyote ile kuchukua hatua, hivyo mpira wa miguu kuongozwa kwa kuzingatia sheria na haki.

Akizungumza na NIPASHE jana kuhusiana na kukataliwa kwa ombi lake, Rage alisema kuwa hana cha kusema kwa sasa kwavile bado hajapokea majibu rasmi ya maandishi kutoka kwa TFF.

"Hivi sasa siwezi kusema lolote kwa sababu mimi nilipeleka ombi langu kwa barua rasmi na hadi sasa sijapokea majibu hayo kwa njia hiyo ya kiofisi," alisema Rage.


 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake