Lakini licha ya kwamba usaliti si kitu kizuri, watu wamekuwa wakisalitiana, tena sana tu. Inafika wakati unashindwa kuamini kama yupo mtu ambaye hajawahi kumsaliti mpenzi wake.
Niseme tu kwamba wapo wachache waliotulia ila asilimia kubwa ya walio kwenye uhusiano ni wasaliti, hata tafiti zimethibitisha hilo.
Kwa kuwa kusalitiana imekuwa ni kama sehemu ya maisha yetu ya kila siku, kuna kila sababu ya kukaa na kujiuliza kwa nini mpenzi wako afikie hatua ya kufanya hivyo?
Tukubaliane kuwa, hakuna jambo linalofanyika bila sababu. Ni vigumu sana mumeo/mkeo kuchukua tu hatua ya kutoa penzi kwa mtu mwingine bila kuwepo na sababu.
Ukijaribu kufuatilia, wapo wanaume ambao walifikia hatua ya kuwaua wake zao baada ya kuwafumania. Hii inaonesha kusalitiwa kunauma na hata pale mmoja wetu anapofanya hivyo, anajua fika mpenzi wake akijua ataumia sana.
Jiulize haya
Kama kweli wewe ukisikia mumeo au mkeo ana uhusiano na mtu mwingine, kwa nini wewe usaliti? Unajisikiaje pale unapomvulia nguo mtu ambaye unajua wazi ni wa kupita tu kwako? Hivi huoni kwamba unajishusha na kukosa ile thamani ya kuwa mke/mume wa mtu?
Mbaya zaidi wapo ambao wako ndani ya ndoa lakini wanatoa penzi kwa vijana wadogo au kwa wanaume wasio na mbele wala nyuma, heshima itabaki kweli? Hata kama utakuwa umepewa penzi ambalo hujawahi kulipata lakini baada ya hapo huoni utakuwa umejitia doa?
Kijana mmoja ambaye naishi naye mtaani anasifika sana kwa kutembea na wake za watu. Ukimuangalia na wanawake ambao wanatajwa kumpa penzi, huwezi kuamini. Kibaya zaidi ni kwamba kila kijana huyo anapotembea na mke wa mtu, huenda kuwasimulia washikaji zake kijiweni.
Matokeo yake sasa wanawake hao wakipita, wanaangaliwa kutoka kichwani hadi miguuni huku vijana wengine wakishindwa kuamini kama kwa jinsi walivyo wameweza kuwasaliti waume zao.
Kwa kweli usaliti huu ‘usio na macho’ haufai kabisa. Sioni sababu ya wewe kushobokea penzi la mtu mwingine wakati mambo ya msingi sana unayapata kutoka kwa huyo uliyenaye.
Hata kama ana upungufu wa hapa na pale lakini suluhisho si kumsaliti. Tambua hata wewe una upungufu wako ambao yeye anakuvumilia, huenda angekuwa ameshakusaliti.
Lakini sasa unapobaini mwenza wako amekusaliti au anaendelea kukusaliti, unatakiwa kujiuliza sababu za yeye kufanya hivyo. Ni sawa atakuwa amekukosea sana lakini si vibaya ukajua chanzo.
Sisemi kwamba kuna uhalali wa watu kusalitiana lakini ninachotaka kukiweka wazi hapa ni kwamba, wapo baadhi wanawalazimisha wenza wao kuwasaliti hata kama hawakuwa na mawazo hayo.
Wewe mwanaume usitarajie kuwa mkeo hatakusaliti kama unaonesha wazi ni mtu wa ‘totoz’, ukirudi nyumbani humpi mkeo haki yake ya ndoa, mgovi na usiye na heshima kwake. Katika mazingira hayo ni lazima atashawishika kwa wanaume wasumbufu wenye uchu na vya watu.
Lakini pia wewe mwanamke kama utakuwa ni mtu wa kumbania penzi mumeo, una gubu kiasi kwamba kila akirejea nyumbani amani inatoweka, usitarajie kuvumiliwa eti kwa kuwa haifai kusalitiana. Anza wewe kuona aibu kumsaliti mwenzako kisha ukisalitiwa, jiangalie mwenendo wako kabla ya kulaumu au kuchukua hatua.
Ni hayo tu kwa leo, hadi wiki ijayo tena.
www.globalpublishers.info
No comments:
Post a Comment