ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, August 15, 2012

Wachimba kokoto watishia kususia Sensa

Nora Damian 
ZAIDI ya wakazi 3,000 kutoka mitaa ya Maweni na Mjimwema Kigamboni wametishia kususia zoezi la sensa linalotarajiwa kuanza Agosti 26, mwaka huu kwa madai ya kuzuiwa kuchimba kokoto katika eneo hilo. 

Wakizungumza Dar es Salaam jana, wakazi hao walisema kwa zaidi ya miaka 20 wamekuwa wakichimba kokoto katika eneo hilo na kwamba baadhi yao walikuwa na leseni na wengine hawana.
 

Mmoja wa wakazi hao, Maria Masimba alisema kwa muda mrefu wamekuwa wakifanya shughuli zao katika machimbo hayo na kwamba maisha yao yote wanategemea machimbo hayo. 

“Kula kwetu, kusomesha watoto na maisha yetu yote tunategemea machimbo haya hivyo wasitutoe kama wakimbizi,” alisema Masimba na kuongeza kuwa: 

 “Siwezi kujiandikisha wakati watoto wangu wanakufa ndani kwasababu ndiyo ajira yangu ninayoitegemea,” alisema.

 Mkazi mwingine, Cosmas Mateo alisema hivi sasa wamezuiwa kuingia katika eneo hilo na kwamba hata wakisafirisha mizigo yao inakamatwa. 

Alisema baadhi yao walikuwa na leseni zilizotolewa na Wizara ya Nishati na Madini ambazo walikuwa wakizipata kila mwaka lakini baadaye zilifutwa. “Serikali iseme ukweli kama imetuchoka, tumepewa stop order (amri) hatufanyi chochote halafu leo hii wanakuja kutuambia tuondoke kwenye machimbo haya,”alisema Mateo. 

Wakazi hao pia walilalamikia kitendo cha wawekezaji saba wanaoendelea na shughuli ya kuchimba kokoto katika eneo hilo kwa kile walichodai kuwa hata hao hawana leseni. 

“Kama wameamua kutufukuza basi na wale wawekezaji watoke kwasababu hakuna mwenye leseni,” alisema. 
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Maweni, Sylvester Roche, alisema hajapata taarifa zozote kutoka ngazi za juu kuhusu kusitishwa kwa shughuli za uchimbaji kokoto katika eneo hilo na kwamba hali hiyo imewachanganya wananchi. 

“Tulifuatilia madini wakasema leseni zote zimefutwa lakini iweje makampuni yanaendelea kuchimba?” alihoji Roche. 

Alisema wananchi hao hawajui kinachoendelea na kwamba kuna mkanganyiko kwani baadhi ya wawekezaji wamekuwa wakiendelea na shughuli zao wakati wananchi ambao ni wachimbaji wadogo wadogo wanazuiliwa. 

Mwananchi

No comments: