Sunday, August 12, 2012

Wahanga wapelekwa Nairobi usiku


  Ni kufuatia agizo la Rais Mwai Kibaki
  Mmoja asahaulika wodini Muhimbili
Jitihada zilizofanywa na Serikali ya Kenya kutuma helkopta ya jeshi kuwasafirisha majeruhi na maiti wa ajali iliyoua Wakenya 12 na kujeruhi wengine 72, zimepongezwa ingawa majeruhi Mary Mungai, alisahaulika wodini katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na NIPASHE Jumapili jana, Ofisa Habari wa Muhimbili Aminiel Aligaesha, alisema majeruhi hao walianza kuchukuliwa Ijumaa kati ya saa 2:00 na saa 4:00 usiku na kwamba safari ya mwisho iliyofanyika saa 4:00 waokoaji hao waliamini kuwa walikuwa wamemaliza kazi ya kuwapakia na kuwarudisha nyumbani Nairobi.
Walisafirishwa kwa magari ya wagonjwa kutoka Muhimbili hadi uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Dar es salaam.
Alisema katika heka heka hizo za kuwachukua wagonjwa, Mungai aliyekuwa amelazwa wodi namba nane Kibasila alisahaulika na kwamba alirejeshwa nyumbani jana kwa ndege majira ya mchana baada ya mawasiliano kufanyika.
Alisema hawezi kuelewa sababu za kusahulika kwa mgonjwa huyo na kuongeza kuwa pengine ni kuchanganyikiwa kulitokana na ajali hiyo.
Wasafiri 84 wakiwa wanakwaya wa Kanisa la Presbyterian kutoka Thika nchini Kenya, wakiwa katika safari ya kuelekea Zanzibar na Dar es Salaam walipata ajali iliyosababisha vifo vya watu 12 na kujeruhi wengine 72.
Ajali hiyo iliyohusisha magari manne ilitokea juzi saa 11 alfajiri katika kijiji cha Makole karibu na daraja la mto Wami, mkoani Pwani na kuua watu 12 na kujeruhi wengine 72.
Kufuatia tukio hilo, Rais wa Kenya Mwai Kibaki, aliagiza helikopta ya jeshi la nchi hiyo kutua Dar es Salaam na kuwarudisha nyumbani majeruhi na miili ya wahanga wa ajali hiyo.
Ofisa Habari alisema Muhimbili ilipokea watu 72, kati yao 14 walikuwa na majeruhi makubwa wakati 58 walikuwa na majeraha madogo madogo ukiwemo mshtuko na kwamba maiti zilikuwa 12.
Kwa upande wake Msemaji wa Taasisi ya Mifupa (MOI) , Jumaa Almas, alisema majeruhi Jane Wangui, anaendelea kupatiwa matibabu hospitalini hapo kutokana na maumivu ya mgongo, ambayo yalizuia kusafirishwa juzi pamoja na wenzake.
Alieleza kuwa MOI ilipokea wagonjwa 18 ambao waliondoka na kubakiwa na Wangui aliyeumia vibaya sehemu za mgongoni na kwamba anaendelea vizuri.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani ilipotokea ajali hiyo, Ernest Mangu, alisema katika ajali hiyo iliyohusisha matukio mawili, mkasa wa kwanza ulikuwa wa gari namba KBQ 203P iliyokuwa imewabeba waumini hao kuacha njia na kutumbukia shimoni.
Aliliambia gazeti hili kuwa chanzo cha kuingia shimoni hakijajulikana hadi sasa na kuendelea kusema kuwa ajali ya pili iliyotokea muda mfupi, ilisababishwa na uzembe wa dereva wa lori lenye namba T 229 AFP lililokuwa na trela namba T 785 AFX lililokuwa likitokea Tanga kuelekea Dar es Salaam kuligonga ubavuni gari la waumini hao lenye namba KBL 044M lililokuwa limesimama kuwasaidia wenzao waliokuwa wameangukia korongoni.
Alisema dereva huyo ambaye hata hivyo hakumtaja jina, anashilikia na polisi akisubiri kufunguliwa mashtaka na pia uchunguzi wa tukio hilo unaendelea.
Vyombo vya habari nchini Kenya viliikariri polisi kuwa zaidi ya waumini 80 waliokuwa kwenye mabasi mawili madogo walikuwa wakielekea Dar es Salaam na Zanzibar kwa ajili ya shuguli zao za kidini.
Wakati huo huo, kutoka Nairobi nchini Kenya , Wakenya wamejitokeza kwenye mitandao kutoa maoni ya kumpongeza Rais Mwai Kibaki kwa hatua ya kuagiza helkopta ya Jeshi la Kenya kuwafuata na kuwarudisha nyumbani mara moja majeruhi na miili ya marehemu waliojeruhiwa na kupoteza maisha katika ajali hiyo.
Walimpongeza Rais wao kwa kufanya maamuzi ya kutuma helkopta ili kuwapeleka Nairobi kwa matibabu na mazishi kwa kutumia mtandao wa gazeti la kila siku la the Daily Nation na hizi ni baadhi ya taarifa za ujumbe mfupi walizomtumia;
“Hivi ndivyo Mkuu wa nchi anayejali anavyowafanyia raia wake” “ Huyu ni Rais mwenye utu ameonyesha majukumu yake kwa Wakenya walioko hata nje ya mipaka . Haya ndiyo yanayoufanya uongozi ulioheshimika. Rais wa kwanza anayejali Wakenya na mambo mengine yanayowakuta hata wakiwa nje ya mipaka yao.”
“Maagizo mazuri mheshimiwa Rais amefanya,” “Hii inaonyesha jinsi anavyowajali wananchi wake Mungu azidi kuwa naye”
“Namheshimu Rais kwa kuchukua maamuzi magumu na hatua za kuwasaidia majeruhi na kusaidia familia zao na za wafiwa hiki ndicho serikali ya watu inachotakiwa kukifanya . Maisha ya Mkenya aliyeko mbali yanatakiwa kulindwa kama ya Wakenya milioni 40. Hii ndiyo serikali ya kidemokrasia na inayowajibika kwa watu wake . Haijalishi chochote lakini lifanyike lolote ili kuokoa maisha ya raia wake.”
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments: