Tuesday, August 21, 2012

Watoto wanne kuiwakilisha Tanzania EAC


Watoto wanne nchini wamechaguliwa na wenzao kuiwakilisha Tanzania kwenye mkutano utakaowakutanisha watoto toka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) unaotarajiwa kufanyika katika jiji la Burundi nchini Burundi kuanzia Septemba Mosi mwaka huu.

Mkutano huo wa watoto unaoratibiwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto kwa kushirikiana na Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Tanzania, unafanyika kwa lengo la kuona ni kwa namna gani nchi za EAC zitashiriki kutengeneza sera ya maendeleo ya watoto wa Afrika Mashariki.

Akizungumza kwenye ufunguzi wa mkutano wa watoto toka sehemu mbalimbali waliokutana jijini Dar es Salaam pamoja na mambo mengine, kwa lengo la kuchagua wawakilishi wa Tanzania kwenye mkutano huo, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Watoto wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Tukae Njiku, alisema kwamba wanakutana Bujumbura kujadili changamoto mbalimbali zinazowakabili watoto wa Jumuiya hii.

“Nyingi ya changamoto za watoto katika nchi zetu zinafanana, lakini katika mkutano wa Burundi tutajikita katika changamoto tatu ambazo ni zile zinazowakabili watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani, wenye ulemavu na namna mila na desturi za Kiafrika zinavyoathiri maendeleo ya watoto na baadaye tutakuja na sera ya maendeleo ya mtoto wa Afrika Mashariki,” alisema.



Watoto waliochaguliwa kuiwakilisha Tanzania ni pamoja na Wastara Athumani aliyechaguliwa kuiwakilisha kanda ya Kati na Pwani, Faraja Maulidi anayeiwakilisha kanda ya Kusini, Selemani Kibakaya anayeiwakilisha kanda ya Kaskazini na Hudhaima Mbaraka anayeiwakilisha kanda ya Zanzibar.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake