Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema) kimekataa mwaliko wa Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa,
kushiriki katika semina aliyoiandaa kuhusu amani na usalama wa nchiChama hicho kimesema hakitashiriki katika semina hiyo wakati huu kwa
kuwa kinasubiria hatua za Rais kuhusu mauaji ya kisiasa yaliyotokea
katika mikoa mbalimbali nchini.
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi Chadema, John Mnyika, katika taarifa yake
kwa vyombo vya habari alisema chama hicho kimechukua hatua hiyo
kikitambua umuhimu wa amani na usalama wa nchi na wajibu wa Jeshi la
Polisi pamoja na Vyama vya Siasa katika kukuza demokrasia ya vyama
vingi.
Mnyika alisema hatua hiyo imefikiwa kufuatia utendaji dhaifu na wa
kipropaganda unaoonyeshwa na Tendwa uliosababisha Kamati Kuu ya Chadema
kumtangaza kuwa ni adui wa demokrasia na hafai kuwa katika nafasi aliyo
nayo.
“Kamati Kuu iliazimia kuwa pamoja na kuendelea kuheshimu sheria ya vyama
vya siasa, Chadema haitashiriki shughuli zozote zitakazosimamiwa na
John Tendwa hadi hapo atakapoondolewa katika nafasi yake na kuteuliwa
msajili mwingine,” alisema.
Alisema Kamati Kuu ya Chadema ilifanya kikao maalumu Septemba 9 mwaka
huu kilichojadili hali ya siasa nchini kufuatia mfululizo wa mauaji
yanayofanywa na Jeshi la Polisi katika shughuli za kisiasa za Chadema na
mipango ya baadhi ya viongozi wa Serikali ya kudhibiti Vuguvugu la
Mabadiliko (M4C) kwa mbinu haramu.
“Katika majadiliano ya kina kabla ya kufikia maamuzi Kamati Kuu pamoja
na mambo mengine ilieleza kusikitishwa na kauli za kisiasa ambazo
zimekuwa zikitolewa na Tendwa, zenye mwelekeo wa kukibeba Chama Cha
Mapinduzi ( CCM) na serikali,” alisema.
Nipashe
No comments:
Post a Comment