ANGALIA LIVE NEWS

Friday, September 21, 2012

Mufti Simba amtolea uvivu Sheikh Ponda


Mufti wa Tanzania, Sheikh Issa Bin Shaaban Simba (mwenye magongo) akitoka katika chumba cha mkutano baada ya kutoa tamko la Baraza Kuu la Waislam Tanzania (Bakwata) likilaani harakati za kikundi kinachojiita Jumuiya ya Taasisi za Kiislamu Tanzania. Kushoto ni Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhaji Mussa Salumu. Picha na Venance Nestory
MUFTI wa Tanzania, Sheikh Issa bin Shaaban Simba amesema kuwa Katibu wa Kamati ya Kutetea Haki za Waislamu, Sheikh Ponda Issa Ponda anatumia Waislamu kwa manufaa yake na siyo kiongozi wa dini.

Akitoa tamko la Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) jana, Sheikh Simba alisema harakati zinazoendeshwa na kikundi kinachojiita Jumuiya ya Taasisi za Kiislamu Tanzania, kinachoongozwa na Sheikh Ponda, kinatumika kwa ajili ya masilahi binafsi.


“Nawatahadharisha Waislamu wote nchini kwamba Ponda Issa Ponda si mwanazuoni, si Sheikh, hakusoma elimu ya msingi ya kidunia wala ya kidini, hata Qur’an hajui kusoma.  Anajaribu kuwatumia Waislamu kwa manufaa yake binafsi,” alisema Sheikh Simba na kuongeza:
“Hatujawahi kushuhudia kutoka Jumuiya ya Taasisi za Kiislamu Tanzania jambo lolote la maendeleo zaidi ya ghasia za maandamano, kupora misikiti na kudandia matukio na kuwachangisha Waislamu fedha, mwishoni mwa maandamano hayo huishia kuwatapeli waumini fedha zao ambazo huishia mifukoni mwa Ponda na wenzake.”  
Hata hivyo, Sheikh Ponda alipoulizwa maoni yake kuhusu kauli ya Mufti Simba, alisema kwamba anamshangaa kiongozi huyo mkubwa wa dini ya Kiisilamu kutoa kauli za matusi dhidi yake na kwamba harakati za kumwondoa ziko palepale na zinapamba moto.
Tamko la Sheikh Simba linatokana na vuguvugu linaloendelea nchini la kutaka kuung’oa uongozi wa Bakwata kwa kile kinachodaiwa baraza hilo limeshindwa kutetea masilahi ya Waislamu nchini.
“Ni kigenge cha watu wachache wenye kufuata madhehebu ya Mawahabi ambao kwa mujibu wa itikadi yao wanaamini kwamba Muislamu yeyote asiyefuata itikadi yao basi huyo siyo Muislamu na hafai kuwa kiongozi kwa ngazi yoyote ile,” alisema Sheikh Simba.
Alisema kikundi hiki ambacho kimejivika vazi la kuendesha wanachokiita harakati za Kiislamu  kinaongozwa na watu wachache ambao hawataki kufuata utaratibu wala kutii mamlaka ya dola, badala yake wanataka matakwa yao watu wote wayafuate.
“Vurugu, chokochoko na ghasia za uvamizi hazikuanzia Bakwata, wamekuwa wakifanya hivyo sehemu mbalimbali mikoani kwa kuvamia na kuteka misikiti na kuwaondoa viongozi waliochaguliwa kihalali kwa nguvu na udhalilishaji mkubwa na hatimaye kupora na kuhodhi rasilimali za misikiti hiyo,” alisema Sheikh Simba na kuongeza:

Mafunzo ya karate
“Wamekuwa wakiendesha mafunzo ya karate kwenye misikiti hiyo waliyoiteka na kuikalia kimabavu ili waweze kuendeleza dhuluma yao ya uporaji wa Misikiti na vituo vingine vya Kiislamu.”
Alisema aliwataka Waislamu wote nchini kutambua ya kwamba vitendo vya vurugu na uvunjaji wa sheria vinavyofanywa na Sheikh Ponda na kikundi chake kamwe havina uhusiano wowote na dini ya Kiislamu.
“Ni vitendo vinavyokiuka maadili ya Uislamu. Kwa sababu hiyo nawaonya na kuwatahadharisha Waislamu wa madhehebu yote kuepuka vitendo vya uvunjaji wa sheria unaofanywa na kikundi hiki cha watu wachache,” alisema.
Sheikh Simba alipongeza vyombo vya dola kwa jinsi vilivyoshughulikia maandamano ya Waislamu yaliyoongozwa na Sheikh Ponda ambayo yalifanyika Septemba 7 mwaka huu na kuishia katika Ofisi za Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
 Alisema kitendo kile kilikuwa ni kuvunja sheria za nchi kwani Uislamu unasisitiza kuheshimu mamlaka iliyoko madarakani,” alisema Sheikh Simba.
“Natoa wito kwa vyombo vya dola kwamba viangalie utaratibu wa kuwashughulikia watu wanaoleta vurugu kwa kujifanya viongozi wa kidini na kutoa matamko ya kutishia kuwaondoa viongozi halali wa taasisi zilizosajiliwa ambazo zinaendesha shughuli zake kwa mujibu wa sheria za nchi.”
Ponda ajibu mapigo
Akijibu tuhuma hizo, Sheikh Ponda alisema Sheikh Simba ameonyesha kukosa busara kwa sababu kama kiongozi mkuu hakutakiwa kutoa matusi kama hayo na kwamba alitakiwa kuzungumza mambo ambayo yana masilahi kwa Waislamu.

“Mambo aliyosema Mufti Simba hayana maana kwa maendeleo ya Waislamu, kwani yeye (Simba) ni kiongozi mkubwa ambaye anatakiwa kuzungumza vitu vitakavyowaletea faida Waislamu. Azma yetu ya kumng’oa iko palepale na hivi sasa nguvu ipo kubwa,” alisema Sheikh Ponda.

Alisema Waisalmu hawana mgogoro na Bakwata bali uongozi wa baraza hilo makao makuu ndiyo tatizo lao kubwa.

“Ifahamike kwamba Waislamu nchini hawana mgogoro na Bakwata, lakini wana mgogoro na uongozi wa Bakwata hasa makao makuu, kwani wamekuwa wakiuza mali za Waislamu bila hata kufuata taratibu, jambo ambalo haliwezi kukubalika,” alisema Sheikh Ponda na kuongeza:

“Sisi tutaendelea na msimamo wetu kwamba uongozi wa Bakwata haufai na kwamba, wamekuwa wakiuza mali za Waislamu tofauti na taratibu za baraza hilo zinavyoagiza jambo ambalo ndilo tunalipinga.”

Mbali ya kutaka kumng’oa Sheikh Simba, kikundi hicho cha Waislamu kinataka pia kumng’oa madarakani Katibu Mkuu wa Baraza la Mitihani (Necta), Dk Joyce Ndalichako kwa madai ya kusababisha wanafunzi kufeli somo la Maarifa ya Kiislamu kwa wanafunzi wa kidato cha sita mwaka huu.
Septemba 13 mwaka huu, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu, Suleiman Kova aliwaonya baadhi ya waumini wa Kiislamu ambao wanataka kuvamia Ofisi za Bakwata na kumtoa kwa nguvu madarakani Sheikh Mkuu Simba.
Mbali na Kova, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kikanda wa Kinondoni RPC, Charles Kenyela naye aliwatahadharisha Waislamu wanaotaka kwenda kumng’oa Mufti Simba kufuata sheria na taratibu ili kuepuka usumbufu ambao unaweza kujitokeza.
Kenyela alisema hakuna haja ya kufanya vurugu, kwani kuna taratibu zilitumika kumpata Mufti hivyo ili kuepuka adha ambayo inaweza kutokea zifuatwe sheria hizohizo.
Hata hivyo, hivi karibuni Serikali kupitia  Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo ilitangaza  kumsimamisha kazi Mkuu wa Idara ya Utafiti, Tathmini na Kompyuta wa Baraza la Mitihani  (Necta), Joseph Mbowe baada ya kubainika kufanya uzembe uliosababisha matokeo ya somo la Maarifa ya Kiislamu kwa wanafunzi wa kidato cha sita mwaka huu kukosewa.
Mara baada ya uzembe huo, Serikali ilirekebisha kasoro hiyo na wanafunzi wakarekebishiwa matokeo yao

Mwananchi

No comments: