Ni takribani miezi miwili sasa imepita tangu timu ya pili ya mabingwa wa Tanzania bara Simba Sports Club kuandika historia ya kuwa mabingwa wa kwanza katika historia ya ya michuano ya BancABC Super8 kwa kuwafunga timu ya wakubwa ya Mtibwa Sugar ya Morogoro kwa mabao 4-3.
Baada ya kutwaa ubingwa huo vijana wa Simba B chini ya kocha Selemani Matola walikuwa wanasubiriwa kutimiziwa ahadi yao waliyopewa na uongozi wa tangu mwanzo wa michuano kwamba ikiwa watafanikiwa kuchukua ubingwa wa mashindano hayo wenye zawadi ya fedha taslimu shilingi millioni 40, basi kila mchezaji angepewa mgao wa kiasi kisichopungua millioni 1pamoja na kupata mgawo mwingine wa mapato ya mlangoni.
Vijana kazi wakaitimiza na wakaiandikia historia klabu kwa kuchukua ubingwa wa Super8, na kilichobakia ilikuwa ni kupata walichoahadiwa. Fedha zikatoka na mapato ya mlangoni yakapatikana, lakini kwa taarifa za uhakika nilizozipata kutoka kwa wachezaji wa Simba B ni kwamba mpaka sasa uongozi wa klabu hiyo hawajatimiza ahadi hata moja waliyowapa.
"Hatujapewa fedha zetu tulizoahadiwa na uongozi yaani kila siku tumekuwa tukipigwa kalenda tu. Tumekuwa tukisikia kwamba zile fedha zetu tulizoshinda katika Super8 zimetumika kuipeleka timu ya wakubwa kwenye kambi Arusha. Ni jambo zuri lakini vipi kuhusu sisi ambayo tulizipigania zile fedha na tukahadiwa kupewa mgawo ule. Wengine hatupati chochote kuitumikia klabu hii na tulikuwa na tuna mipango na ile fedha, hivyo jambo hili linatukatisha tamaa na kuendelea kufanya vizuri zaidi."
Kutokana na kutokutimiziwa ahadi yao vijana hao wa Simba B wamefikia maamuzi ya kugoma kufanya mazoezi ili kushinikiza kulipwa fedha walizoahadiwa.
No comments:
Post a Comment