ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, September 19, 2012

Siri za wapenzi kutochokana!-2

JISIKIE mwenye bahati kukutana na mimi kwenye ukurasa huu. Kama ni mara ya kwanza, karibu ndugu yangu lakini habari njema kwako ni kwamba, huna cha kupoteza. Utavuna vitu vikubwa sana ambavyo  vitakupa dira maishani mwako.
Nazungumzia juu ya wapenzi kutochokana. Hili ni tatizo kubwa sana kwenye uhusiano (hasa ndoa), maana ni chanzo cha kichocheo cha usaliti. Wiki iliyopita nilianza kuelezea maana yake kwa upana, nikamalizia na mifano kutoka kwa wasomaji ambao walikuwa na matatizo mbalimbali kwenye uhusiano wao.

Kila mmoja alikuwa na lake, lakini yenye mlengo mmoja. Hebu twende tukaone kitu kupitia kwao, halafu tuendelee na somo letu. Kipo kitu cha kujifunza rafiki zangu, kipo! Karibu darasani..
TATIZO LAO NI MOJA!
Nilipata nafasi ya kuwashauri moja kwa moja (kwa nyakati tofauti), hasa baada ya kuwauliza maswali ili kujua kinachosababisha yote hayo. Wote watatu wana tatizo moja. Kuchokana.
Kulikuwa na wengine waliokuwa na kesi zinazofanana na hizo lakini baada ya kuwadadisi nikagundua kwamba kuna matatizo mengine zaidi, kubwa likiwa ni maandalizi hafifu kabla ya tendo lenyewe.
Msingi wa yote hayo ni kuchokana rafiki zangu. Ni kweli kutoandaana vya kutosha (hasa kwa wanawake) husababisha tatizo la kutokufurahia mapenzi, lakini asilimia kubwa huanza tatizo la kuchokana ambalo husababisha kupunguza mahaba na mwisho kupoteza msisimko.
Likishatokea tatizo la kupoteza msisimko, maana yake ni kwamba, hata atakapokuwa faragha hatakuwa mwenye utayari. Anataka kufanya mambo yake haraka haraka. Hana msisimko. Maandalizi yatatoka wapi? Ndiyo hapo sasa tatizo lililowapata ndugu zetu hapo juu hujitokeza.
UNAWEZA KUDHIBITI KUCHOKANA?
Ndiyo! Inawezekana kabisa. Ni kweli wapo wengi ambao hujikuta tu wamewachoka wapenzi wao. Pengine hawataki hali hiyo na wanajitahidi kushindana nayo sana, lakini wanashindwa.
Si kwa kutaka ni kwa vile hawajui kitu cha kufanya. Hapa kwenye All About Love nitakusaidia cha kufanya. Twende sasa...
KUOGA PAMOJA
Wanandoa kuoga pamoja ni tendo linaloleta msisimko wa aina yake. Mara nyingi, ndoa inapokuwa changa kabisa, wengi huwa na mazoea haya, lakini wakishazoeana na ratiba kubadilika hili husahaulika.
Utakuta baba anarudi usiku sana, ameutwika vya kutosha, mke amejichokea, kaamua kuoga mwenyewe na baadaye amekula. Anamsubiri mume. Akifika anaingia bafuni peke yake, anarudi chumbani wanalala, asubuhi mchaka mchaka wa kwenda kazini, zoezi hilo haliwezi kufanyika tena.
Ikumbukwe kwamba, kwa kuoga pamoja huzidisha msisimko wa mapenzi na si ajabu hisia za mapenzi zikaamka kwa kasi ya ajabu na baadaye mambo yakaendelea vizuri chumbani. Kwa kuacha kuoga pamoja hupunguza msisimko na ndiyo mwanzo wa kuzoeana na kuchokana.
Ni vigumu sana kuanzisha suala la mapenzi chumbani kwa ghafla tu...huanzia mbali, ikiwemo wakati wa kuoga pamoja. Bila shaka nimeeleweka marafiki zangu. Angalia kipengele kinachofuata...
KULA PAMOJA
Silaha kubwa ya kutochokana ni kufanya mambo mengi kwa pamoja. Inaeleweka kwamba, majukumu ya kila siku husababisha watu kuwa mbalimbali kwa muda mrefu hasa nyakati za mchana, lakini angalau mkipata muda wa kula pamoja, mtakuwa karibu.
Mtasogezana karibu kihisia. Hata kama mnafanya kazi ofisi tofauti, mnaweza kupanga ratiba angalau mara moja kwa wiki, mkatoka mchana na kupata chakula pamoja. Muhimu zaidi ni usiku, wakati wa chakula cha jioni ni vyema wanandoa wakapata muda wa kula pamoja.
Kukaa meza moja huongeza msisimko, utani kidogo tu mtakaofanyiana au kulishana, unaweza kujenga kitu kikubwa na kila mmoja akabaki akimuona mwenzake mpya kila siku.
BUSU
Mwaaa! Tendo dogo sana lakini lenye msisimko wa kipekee. Jenga mazingira ya kumbusu mpenzi wako kila mara. Usikubali kumuacha hivi hivi, hasa kabla ya kulala, kuamka na kuagana naye.
Mbusu shavuni, halafu mwambie: “Nakupenda sana.” Wengi (hasa wanawake) husisimka sana wanapobusiwa shavuni au shingoni. Jizoeshe mtindo huu na kamwe hutajikuta ukimchoka mpenzi wako.
Busu ni alama kubwa ambayo unaweza kumuacha nayo akiikumbuka siku nzima. Atakuchokaje?
KUKUMBATIANA
Tendo hili huambatana na busu. Unaweza kuona ni mambo ya Kizungu sana, lakini hata mnapokuwa peke yenu sehemu ambayo hamuonekani unaweza kumkumbatia mwenzako na kumuongezea msisimko wa kuwa na wewe.
Siku za mwanzo za ndoa, wengi hulala wakiwa wamekumbatiana lakini baadaye tabia hii hupotea ghafla. Hili ni tatizo. Mkumbatie mpenzi wako usiku. Wanawake wengi hulala usingizi mzuri zaidi wanapolala juu ya vifua vya wanaume zao. Kwanini usiwe wewe?
Msogeze karibu yako, mbembeleze ajilaze juu ya kifua chako akideka. Kiukweli utafurahia mapenzi na utajikuta unaendelea kumpa mpenzi wako nafasi ya kwanza kila siku. Umeona eeeh? Naamini kuna kitu kipya umejifunza na bila shaka utabadilika.
Nikuambie kitu? Nakupenda sana msomaji wangu mpenzi. Hii ni kwa sababu najua kichwani mwako kuna kitu kipya kimeingia leo. Ili nikupende zaidi, nenda kakifanyie kazi. Bye friend, next week!
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia Magazeti ya Global Publishers, ameandika vitabu vya True Love, Let’s Talk About Love na All About Love vilivyopo mitaani.

No comments: