WAKAZI wa Kigamboni, Kata ya Vijibweni, Wilaya ya Temeke, Dar es Salaam, wamesema wapo tayari kuzuia msafara wa Rais Jakaya Kikwete ambaye kesho anatarajia kupita eneo hilo hadi watakapoelezwa hatima ya fidia zao.
Rais Kikwete atakwenda Vijibweni kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa daraja la Kurasini ambapo wananchi hao wametakiwa kuondoka
eneo hilo haraka.
Wakazi hao waliyasema hayo jana walipozungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti ambapo Katibu wa Umoja wa Kivuko, Bw. Said Tijinga, alisema watahakikisha wanatumia kila njia kumtaka Rais Kikwete azungumze nao ili kujua hatima yao.
“Tuna mengi ambayo tunataka Rais Kikwete ayajue, viongozi wetu wanadanganywa na ripoti za uongo za mezani, leo hii huduma ya kivuko imesitiswa, juzi Mkuu wa Wilaya hii, Bi. Sophia Mjema, alikuja na kutoa kauli chafu.
“Alidiriki kutuambia hatupo kisheria katika maeneo yetu tuondoke, ukweli Serikali yetu haijui inachofanya, inapaswa kutambua kuwa inawasha moto kwa wakazi wa Vijibweni.
“Kivuko hiki kipo kisheria, kinalipa kodi Mamlaka ya Mapato (TRA), pia kina leseni ya uendeshaji kutoka Mamlaka ya Udhibiti, Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA),” alisema.
Aliongeza kuwa, kivuko hicho kilianza mwaka 1965 hivyo kauli ya Bi. Mjema katika ziara yake ya kushtukiza na kuwataka wasitishe huduma imewachanganya hivyo wanataka Rais Kikwete awape msimamo wa Serikali kabla ya kuendelea na ujenzi wa daraja hilo.
Mkazi wa eneo hilo Bw. Faidha Hassan, alisema hakuna mwelekeo wowote wa kupewa fidia na kuhoji sababu ya viongozi wa Serikali kuogopa kuonana nao ili wajibu maswali yao.
Mama lishe waliopo eneo hilo walionekana kujawa na simanzi na wengine kutokwa na machozi kutokana na askari wa jiji kuvunja vibanda vyao na wengine kupoteza mali na fedha.
Majira
No comments:
Post a Comment