ANGALIA LIVE NEWS
Monday, September 24, 2012
Yanga kufikishwa mahakamani
Na Zahoro Mlanzi
UONGOZI wa Hoteli ya Peter Safari, umeijia juu Klabu ya Yanga kwa kuitaka iiombe radhi hoteli hiyo na ikishindwa italishughulia suala hilo kisheria kutokana na kudai aliyekuwa kocha wao, Tom Saintfeit kuwadhalilisha kwa kusema huduma zao za hali ya chini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na hoteli hiyo Jijini Mbeya jana na Mkurugenzi Mtendaji wa hoteli hiyo, na gazeti hili kupata nakala yake ilieleza kwamba hoteli hiyo na Chama cha Wamiliki wa Hoteli Mbeya, kinachukulia suala hilo kama kampeni maalumu ya kudhalilisha na kukatisha tamaa wateja kuiona Mbeya haina hoteli za hadhi za kuishi timu na watu wenye hadhi katika jamii, kitu ambacho si kweli.
Alisema visingizio hivyo vimetokana na kushindwa kwake kuwezesha timu kufikia matarajio ya mashabiki na wapenzi wa timu hiyo huku viongozi wa wake waliomba kuwalaza wachezaji wawili katika kitanda kimoja tofauti na taratibu za hoteli na hiyo ilitokana na mipangilio yao hasa kwenye suala la uwezo wa kulipia kila mchezaji chumba chake.
"Uongozi wa hoteli ulijitahidi kwa kadri ya uwezo wake kuhakikisha kuwa wachezaji wanapata huduma walizohitaji na hata wakati mwingine kutoa usafiri kwa ajili ya kununua mahitaji ya familia zao kitu ambacho hakifanyiki maeneo mengine kwa gharama za hoteli," ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Alisema kwakuwa maneno ya kocha huyo yametamkwa na kutangazwa kwenye vyombo vya habari pasipo kukanushwa na viongozi wake, suala hilo ni kama sehemu ya kashfa iliyojengwa kwa nia ya kuiharibia hoteli biashara na kuipotezea hadhi mbele ya wageni na watumiaji wa huduma zao.
Alisema kutokana na hali iliyojitokeza, wanautaka uongozi wa Yanga kuiomba radhi hoteli hiyo kutokana na lugha ya kashfa na isiyoendana na utamaduni wa Mtanzania kwa kuzingatia kuwa wachezaji wakiulizwa namna walivyohudumiwa wasingeweza kuzungumza hayo ambayo mwalimu wao ameyazungumza kwa utashi wake.
Aliongeza endapo kama Yanga itashindwa kufanya hivyo, watakusudia kuchua hatua za kisheria kwa kuzingatia kuwa hoteli inaendeshwa kwa mujibu wa taratibu na sheria zinazotawala huduma za hoteli na zile za mipango miji.
Alipotafutwa Makamu Mwenyekiti wa timu hiyo, Clement Sanga kupitia simu yake ya kiganjani kuzungumzia suala hilo, iliita bila kupokelewa.
Kocha huyo wiki mbili zilizopita alikaririwa na vyombo mbalimbali vya habari akidai alipata wakati mgumu pamoja na wachezaji wake kutokana na hali waliyoikuta katika hoteli hiyo ambapo maji, chakula na malazi ilikuwa ni vya shida.
Majira
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment