Tom Saintfiet katikati akisaini mkataba wa kuinoa Yemen na mabosi wake wapya (Picha zote kwa hisani ya Tom Saintfiet)
Na Mahmoud ZubeiryKOCHA Mbelgiji Tom Saintfiet aliyefukuzwa Yanga baada ya siku 80 za kuwa kazini, jana amesaini rasmi mkataba kuifundisha timu ya taifa ya Yemen katika sherehe zilizoifanyika mjini Sana’a.
Akizungumza na BIN ZUBEIRY kutoka Sana’a, Yemen jana, Tom Saintfiet alisema amefurahia mkataba huo mzuri na namna alivyopokewa kwa furaha na upendo katika ofisi mpya.
“Nimefurahi sana, kila kitu ni kizuri, mazingira ya kufanyia kazi na watu waelewa pia, sasa ni jukumu langu kuwafurahisha watu wa Yemen kwa kuwatengenezea timu nzuri itakayowapa furaha kwa matokeo mazuri,”alisema Mtakatifu Tom.
Tom alisema kwamba anatarajia kuiongoza timu hiyo ya Magharibi mwa bara Asia katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Magharibi mwa Asia (kama Kombe la Challenge la CECAFA) itakayofanyika nchini Kuwait Desemba mwaka huu.
Alisema katika michuano hiyo, amepangwa kundi moja na Saudi Arabia, Iran na Bahrain na Januari mwakani, ataiongoza timu hiyo katika Kombe la Gulf huko Bahrain.
“Kwa sasa nipo katika Jiji la Sana'a na kesho nitaanza kazi kwa kambi ya kujiandaa na mchezo wa kirafiki Beirut, Oktoba 16 dhidi ya Lebanon,”alisema Mtakatifu Tom.
Saintfiet alifukuzwa Yanga baada ya kutofautiana misimamo na uongozi wa Yanga, akiwa amefanya kazi siku 80 na kuiachia timu taji la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame.
Saintfiet amefungwa mechi mbili Yanga katika mechi 14 alizoiongoza timu hiyo tangu ajiunge nayo, Julai mwaka huu, akirithi mikoba ya Mserbia, Kostadin Bozidar Papic.
Katika mechi hizo, zimo sita za Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, ambazo aliiwezesha Yanga kutwaa taji, ikipoteza mechi moja tu dhidi ya Atletico ya Burundi.
No comments:
Post a Comment