ANGALIA LIVE NEWS

Monday, October 15, 2012

pombe, sigara ukahaba ni marufuku zanzibar


Na Salma Said
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imepiga marufuku biashara ya ukahaba, matangazo yote ya pombe na uvutaji wa sigara katika mikusanyiko ya watu katika visiwa vya Unguja.

Hayo yamebainika kufuatia marekebisho ya kifungu cha sheria cha 112, cha mswada wa sheria ya kuhusiana na hifadhi na usimamizi wa vihatarishi vya afya ya jamii na afya ya mazingira na mambo inayohusiana na hayo iliyopitishwa ndani ya baraza la wawakilishi jana.


Waziri wa Afya Zanzibar, Juma Duni Haji aliwaambia wajumbe wa baraza la wawakilishi kwamba kutokana na michango mingi ya wajumbe kutaka suala la matangazo ya pombe, uvutaji wa sigara, na biashara ya ukahaba vipigwe marufuku, serikali imekubaliana na maoni ya wajumbe hao na hivyo kifungu hicho kinafanyiwa marekebisho kwa kufutwa matangazo ya ulevi na uvutaji wa sigara katika maeneo ya watu.

Sheria hiyo kabla ya kufanyiwa marekebisho ilikuwa haijakataza kuweka matangazo ya pombe katika matamasha na sehemu nyengine za starehe katika maeneo ya Zanzibar lakini baada ya wajumbe kutishia kuzuwia sheria hiyo, serikali ililazimika kuondosha kifungu hicho cha 112 (1) na (2) kinachohusu matangazo ya biashara.

Awali kabla ya marekebisho kifungu hicho kilikuwa kikisomeka kwamba matangazo yote ya pombe ni lazima yawe na onyo na tahadhari la kiafya na kiuslama kwa watu na madereva.

Waziri Duni, alisema kuanzia sasa kwa mujibu wa sheria hiyo itakuwa ni marufuku kutangaza au kushajiisha matangazo ya pombe kwa kutumia njia mbali mbali zikiwemo ufadhili wa au matamasha ya muziki na starehe nchini.

Maeneo mengine ambayo yalitajwa kuhusishwa na marufuku hiyo ni pamoja na kutangaza maatangazo ya pombe kwa kutumia vipeperushi, vijarida na njia yoyote ya kufikisha ujumbe kwa watu waliomo ndani ya Zanzibar vikiwemo vyombo vya habari.



Pia Waziri huyo alisema eneo jengine ambalo limebadilishwa ni pamoja kudhibiti shughuli za maudhi zinazotokana na uendeshaji biashara ya kujiuza miili ambapo sasa watu ambao watakuwa wakifanya biasharaya ukahaba watakuwa wanakumbana na mkondo wa sheria.

“Zamani dada zetu wakikamatwa wanashitakiwa kama wazururaji lakini sasa chini ya sheria hii itakuwa ni marufuku mwana dada kujiuza kwa sababu hiyo sio mila na utamaduni wetu na kwa kweli waheshimiwa wajumbe jambo hili linaumiza sana vichwa vyetu ni aibu na ni fedheha” alisema Duni.
  
Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Othman Masoud Othman alisema anakubaliana na maoni ya wajumbe wa baraza la wawakilishi kuondoa kabisa matangazo ya pombe kwa kuwa Zanzibar ina maadili yake ni vyema kufuata maamuzi hayo hasa kwa kuzingatia hayawezi kuathiri sheria za kimataifa.
Akitoa maelezo ya kisheria Mwanansheria huyo alisema anakubaliana na mawazo ya wajumbe hao kwa vile ni moja ya mambo ya msingi kufanyika hivi sasa kwani haiwezekani kuwapo kwa kifungu hicho.

Alisema matangazo ya pombe ni vyema serikali ikaliondoa kwani hivi sasa Shirika la Afya Duniani WHO, na Umoja wa Ulaya EU, na baadhi ya nchi ikiwemo  Sweeden tayari wamezuiya matangazo ya pombe na Zanzibar kufuata sheria hiyo ni jambo la busara.

Alisema ni kweli wapo wanaopenda kunywa pombe kutokana na baadhi ya sheria zilizopita kuonyesha kuruhusu pombe ikiwemo ya 1997  na 1964 iliruhusu kila mtu anaetaka kunywa anywe, ingawa  bado maadili yanakataza kufanya vitendo hivyo hadharani.

Masoud alisema kuwepo kwa sheria kutasaidia sana kwani kuwepo kwa matangazo ya sigara kunaweza kuchochea utumiaji mkubwa jambo ambalo linaweza kuleta madhara kwa wananchi wengi huku akisisitiza kinga bora kuliko tiba.


“Hakuna haja ya kuifanya Zanzibar  kuonekana washamba kwa sababu watu wanafuata sheria kwani huku kudharau na kutofuata sheria na kuwa na tabia ya kuoneana muhali katika utekeleaji wa sheria ndio kwa kiasi kikubwa kumechagia kuharibika kwa maadili katika jamii” alisema Mwanasheria huyo.

Alisema serikali kutunga sheria zake kwa ajili ya kuwakinga wananchi wake ni jambo linalokubalika hata katika mataifa makubwa yalioendelea yamekuwa yakifanya hivyo licha ya maendeleo makubwa waliyonayo lakini bado wanaweka kinga katika sheria zao ili kuepusha athari na madhara yanayoweza kutokezea kutokana na matumizi kama hayo.


Masoud aliwaambia wajumbe wa baraza hilo kwamba mfumo wa sasa wa serikali za mitaa kuonekana kuwa dhaifu ndiko kunakosababisha kuchangia kuwapo kwa mambo ambayo yanakinzana na jamii katika shughuli zao kwa kukosa kinga.

Aidha alisema hali hiyo haiwezi kuachwa na ni lazima serikali iweke sheria ambazo zitaweza kuweka mazingira sawa ya maisha ya kijamii kutokana na hivi sasa watu wengi kutopenda kufuata sheria kutokana na kujengeka tabia ya kuoneana muhali.

Licha ya wajumbe wengi kuunga mkono kuondoshwa kwa matangazo ya pombe na uvutaji wa sigara katika mikusanyiko ya watu Masoud alisema sheria na suala moja na utekelezaji wa sheria ni suala jengine hivyo aliwaomba wajumbe hao kushirikiana na serikali yao katika utekelezaji wa sheria zake na kuondokana na tabia ya kukwepa mkono wa sheria.

“Tatizo letu kubwa mtu anapokamatwa na sheria ikataka kuchukua mkondo wake basi hao hao wazee ambao ni waheshimiwa ndio wanaokwenda mahakamani wakataka kesi zifutwe au wakataka wamalize shauri hilo nje ya mahakama...sasa kwa tabia hii nadhani tutakuwa tunatunga sheria lakini utekelezaji wake utakuwa mgumu iwapo bado hatujawa tayari kwa kufuata sheria na mtu asiogope sheria lakini aache kufanya mambo yaliokatazwa na sheria” alisema Masoud.

Kabla ya sheria hiyo kupitishwa serikali ilikuwa ikikataza udhamini wa pombe hasa katika ligi kuu za michezo lakini hakukuwa na sheria maalumu inayokataza lakini matangazo ya pombe yalikuwa yalikuwa yakibandikwa katika matamsha mbali mbali ya muziki na starehe na hivyo kwa mujibu wa sheria hiyo kuweka tangazo lolote la pombe itakuwa ni kosa kisheria.


Awali wakichangia mswaada huo wajumbe wa baraza hilo waligoma kuupitisha iwapo hakitafutwa au kufanyiwa marekebisho ya kuondoshwa matangazo ya pombe, sigara na ukahaba ambao kwa sasa unaonekana kwa kiasi kikubwa kuharibu heshima na na ni kinyume na maadili wa wazanzibari.

Baada ya kufanyika kwa marekebisho hayo wajumbe hao wote kwa sauti moja waliunga mkono marekebisho yaliofanywa na baada ya ufafanuzi huo walikubali kuipitisha sheria hiyo.

No comments: