Wizara ya Afya Zanzibar imesema muongozo wa Shirika la Afya Duniani (WHO) katika kutibu ugonjwa wa malaria ni kutumika kwa dawa za mchanganyiko ambazo zina uwezo mkubwa wa kutibu maradhi hayo.
Naibu Waziri wa Afya Dk Sira Ubwa Mamboya aliwaambia wajumbe wa baraza la wawakilishi wakati akijibu maswali ya ngongeza aliyoulizwa ndani ya kikao cha baraza hilo kinachoendelea Chukwani Mjini Zanzibar.
Dk Sira alisema dawa za mchanganyiko ndiyo zenye uwezo zaidi wa kutibu ugonjwa malaria kwa sasa kwa mujibu wa maelekezo na utafiti uliofanywa na shirika la afya la duniani na hivyo Zanzibar haina sababu haa moja ya kubadilisha dawa hizo au kuacha kuzitumia kwa kuwa hakuna kigezo cha kuziwacha.
“Waheshimiwa Wajumbe wa baraza la wawakilishi nataka kusema kwamba kwa mujibu wa muongozo wa shirika la afya la dunia WHO dawa za mchanganyiko ndiyo sahihi kwa ajili ya kutibu ugonjwa malaria” alisema.
Alisema dawa iliyokuwa ikitumika kutibu malaria kwa sasa Chloroquine imepitwa na wakati na haitakiwi tena kutumika kutibu ugonjwa wa malaria katika mzunguko wa dawa za kutibu maradhi hayo.
Naibu waziri huyo alisema kwa sasa dawa zinazokubalika kwa ajili ya kutibu ugonjwa wa malaria ni dawa za mchanganyiko ambazo alizitaja dawa ya Amodiaquine na Antisine ambazo zimeonekana uwezo wake wa kutibu malaria unatosheleza na unawasaidia wagonjwa wengi wanaotumia dawa hizo.
“ Long acting drugs ni dawa inayokaa muda mrefu mwilini bila ya kupoteza nguvu zake kwa mfano dawa ya Amodiaquine ambayo inatumika kwenye kutibu malaria” alisema na kuongeza.
Alisema kwa lugha ya kitaalamu “Short acting drugs dawa inayokaa mwilini muda mfupi ambayo haidizi masaa sita na kuhitaji kuongezwa mwilini ili ifanye kazi vizuri, mfano dawa ya homa ya mapafu Preumonia” alisema.
Alisema dozi ni kipimo cha dawa ambacho kinakadiriwa kutokana na umri na uzito wa mgonjwa kwa hivyo dawa za malaria zinazotolewa zinafuata utaratibu huo.
Hata hivyo alisema ili nchi iweze kubadilisha dawa inayotumika kutibu maradhi kama vile malaria kuna vigezo maalumu vimewekwa na shirika la afya ulimwenguni ambapo vigezo vyake ni kuwa madhara makubwa katika jamii, kutokuwa na uwezo wa kutibu 'resistance', zile na gharama kubwa kuliko uwezo wa nchi.
“Kwa vigezo hivi dawa za malaria zinazotumika hapa nchini kwetu hazijafikia kigezo hata kimoja kati ya hivyo, kwa hiyo hatuna sababu ya msingi ya kuibadilisha dawa inayotumika” alisema Naibu waziri huyo.
Alisema dawa mmoja hutumika kwa ajili ya kusafisha wadudu wa malaria waliopo kwenye damu, na dawa nyengine hutumika kwa ajili ya kutibu wadudu wa malaria wanaokwenda kushambulia ini.
“Hizo ndiyo faida za dawa mchanganyiko za kutibu ugonjwa wa malaria ambazo zinatibu mambo mengi kwa wakati mmoja tofauti na dawa ya awali ya Chloroquine iliyokuwa ikitibu ugonjwa huo”alisema.
Aliwaeleza wajumbe wa baraza hilo kwamba tangu kutumika kwa dawa mchanganyiko ya kutibu ugonjwa wa malaria ni miaka miwili sasa ambapo yameonekana mafanikio makubwa huku vijidudu vya ugonjwa huo vikipoteza maisha kwa dawa hizo kwa urahisi.
Dk Sira aliwata wajumbe wa baraza la wawakilishi kutoa elimu zaidi kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kutumia dawa mchanganyiko ya kutibu ugonjwa wa malaria ambayo ndiyo sahihi kwa sasa zikiwa na uwezo mkubwa.
Katika suali lake la msingi Mwakilishi wa Jimbo la Wawi (CUF) Saleh Nassor Juma aliipongeza serikali ya Zanzibar na wahisani wa maendeleo kwa juhudi zao za kufanikiwa kuutokomeza ugonjwa wa malaria nchini ikiwa pamoja na kugawa neti kwa wananchi mbali mbali lakini alitaka kujua ni kwa nini serikali inashindwa kuwaletea wananchi dawa zenye dozi ndogo za malaria.
No comments:
Post a Comment