ANGALIA LIVE NEWS
Tuesday, November 20, 2012
JINSI VYAKULA TULAVYO VINAVYOTUMALIZA - 7
WIKI ninaendelea kuelezea namna vyakula tunavyokula kila uchwao vinavyotumaliza kwa kujua au pasipo kujua. Tuwe pamoja.
Katika milo yote hiyo, mtu huyu hajala tunda la aina yoyote wala hajala mboga yoyote ya majani. Mbaya zaidi, siku nzima inaweza kuisha bila kunywa maji hata glasi moja. Kwa sababu kila amalizapo kula au asikiapo kiu, hunywa soda, bia, mvinyo au juisi iliyotengenezwa kwa kuchanganya rangi za ladha mbalimbali.
Ingawa chai, chapati, ugali mweupe, nyama, soda na juisi zilizotajwa hapo juu siyo sumu, lakini vyakula hivyo havina virutubisho vyovyote mwilini, ukiacha chai tu. Vyakula hivyo havina faida mwilini kwa sababu virutubisho vyake vilishaondolewa wakati wa matayarisho yake, kama vile unga wa sembe nyeupe, mkate mweupe na chapati zilizopikwa kutokana na ngano iliyokobolewa.
Halikadhalika soda na juisi za kutengeneza hazina virutubisho kwa sababu ni mchanganyiko tu wa kemikali, sukari na maji ambavyo havijengi mwili. Vyakula hivi vinapoliwa kwa muda mrefu bila kula vyakula vingine huufanya mwili kukosa virutubisho, vitamini na madini, hivyo kuufanya mwili kuwa dhaifu na usio na kinga.
Kwa baadhi ya watu, ulaji wa namna hii ni wa kila siku na wa maisha yote tangu mtu azaliwe. Ulaji wa matunda, mboga za majani na ulaji wa vyakula vingine vyenye virutubisho huonekana ni anasa, ingawa vipo katika mazingira wanayoishi. Katika staili ya maisha kama hii, mwili hauwezi kuwa na kinga ya kupambana na maradhi.
Kama wewe ni miongoni mwa watu wenye staili ya ulaji wa vyakula kila siku kama nilivyo elezea hapo juu, usishangae kwa nini unaugua mara kwa mara au kwa nini unakabiliwa maradhi hatari. Yakupasa kuelewa kwamba mwili wako hauna kinga kwa sababu huwa huli vyakula vyenye kuupa mwili kinga inayotakiwa.
Kwa kawaida mwili wa binadamu unapopewa virutubisho vinavyotakiwa, hujitengenezea wenyewe kinga ya kujilinda dhidi ya maradhi mbalimbali na kinga ya mwili hujengwa kwa kula zaidi matunda ya aina mbali mbali na mboga za majani. Aidha, kinga ya mwili huimarishwa kwa kula vyakula asilia au vyakula vitokanavyo na nafaka zisizokobolewa.
Ili kujenga mwili imara na kujiepusha na maradhi na hali ya kuugua mara kwa mara, ni lazima uchukue hatua ya kubadili staili ya maisha yako kwa kuangalia upya aina ya vyakula unavyokula kila siku, kuanzia asubuhi hadi jioni. Bila kukubaliana na ukweli huu, kuumwa mara kwa mara na kusumbuliwa na maradhi hatari, huwezi kukuepuka na wala usidhani umerogwa.
Katika makala nyingi zilizopita, nimeelezea kwa kirefu aina mbalimbali za vyakula, faida zake na madhara yake. Lakini katika makala haya tutaelezea kwa kifupi kanuni sahihi za ulaji vyakula na mpangilio wake.
MUONGOZO WA VYAKULA
Katika mpangilio wa vyakula, (food Pyramid), imeoneshwa ni vyakula gani tunatakiwa kula kwa wingi na vipi tumetakiwa kula kwa uchache sana.
Itaendelea wiki ijayo. (GPL)
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment