ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, November 1, 2012

JK awalipua wabunge kwa kumsumbua CAG juu ya ripoti zake

Nikishamteua huyu amekaa amefika… Kuna wakati wabunge wakamkasirikia kweli wakasema lazima adhibitiwe, lakini nyie hamna mamlaka ya kumdhibiti CAG,” alisisitiza Rais Kikwete.

Moshi
RAIS Jakaya Kikwete, amesema wabunge hawana mamlaka ya kuhoji uhalali wa ripoti za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) wala kuunda kamati kuchunguza kile alichokitolea ripoti.

Badala yake Rais Kikwete alisema kama wabunge ambao ni mhimili mmojawapo wa dola hauridhiki na ripoti aliyoitoa CAG, wanapaswa kufungua malalamiko Mahakama Kuu ya Tanzania.

Kauli hiyo imekuja baada ya Bunge kuunda kamati teule hivi karibuni kuchunguza upya sakata la Katibu Mkuu wa Nishati na Madini, David Jairo baada ya kutokuridhika na taarifa ya CAG iliyomsafisha.
Mwaka jana Jairo alichangisha fedha kutoka taasisi zilizo chini ya wizara yake ili kusaidia kupitisha bajeti ya wizara hiyo, kitendo kilichotafsiriwa kuwa zilitumika kuwahonga baadhi ya wabunge. Hata hivyo, kwa mara ya kwanza, Rais Kikwete alivunja ukimya wa sakata hilo lililotingisha Bunge na kusema wabunge hawana mamlaka ya kuhoji kazi ya CAG wala kumwita kuhoji uhalali wa kazi yake.

Rais Kikwete alitoa kauli hiyo jana mjini Moshi wakati akifungua Jengo la Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi Mkoa wa Kilimanjaro lililojengwa kwa gharama ya zaidi ya Sh2.5 bilioni zilizotolewa na Serikali.  “Nikishamteua huyu amekaa amefika… Kuna wakati wabunge wakamkasirikia kweli wakasema lazima adhibitiwe, lakini nyie hamna mamlaka ya kumdhibiti CAG,” alisisitiza.  Rais Kikwete alisema hakuna wa kumdhibiti CAG na mfumo huo umetengenezwa kwa makusudi kwa sababu ndiye anayekagua Serikali na mihimili mingine ya dola ambayo ni Bunge na Mahakama.

“Atasema wabunge wamelipana posho isivyostahili watakasirika na ukiwapa mamlaka ya kumdhibiti eti kwa sababu tu kosa lake ni kusema ukweli kwamba wabunge wamechukua posho si sahihi,” alisema.

Rais alisisitiza ”Kazi yake ile ina mamlaka ya kumsema yeyote hata wale wenye mamlaka.” Aka sema pia hata wabunge wakiamua kuchunguza wenyewe bado hawana mamlaka ya kikatiba ya jambo hilo.  Rais aliongeza kusema, “Atasema sisi tumekagua huu ndiyo ukweli na kwa mujibu wa katiba ya nchi hii ukweli wenu nyinyi (wabunge) hauwezi kushindana na ukweli wa CAG”.

Wakati akitoa kauli hiyo mara kwa mara alikuwa akimtazama Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (LAAC), Augustino Mrema na Makamu mwenyekiti wa PAC, Zainabu Vullu.  Wenyeviti hao walikuwa wameketi jukwaa pembeni ya Rais wakiwa pamoja na Makamu Mwenyekiti wa LAAC, Idd Azzan na Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini ambaye ni mjumbe wa LAAC.

“Hata hivyo, mtasema hivi hapa kafanyaje? mbona huyu kamwachia? hicho ndicho alichoona hana makosa basi nyie mnasema ngoja tufanye wenyewe mnasema huyu ana hatia, huyu ana hatia,” alisema Kikwete.

Rais Kikwete alisema CAG ndiye mwenye mamlaka ya mwisho ya ukaguzi na kwamba hawezi kukagua halafu wabunge nao watake kukagua alichokagua na kuhoji ‘ni kwa mamlaka gani’?  “Mnataka kukagua alichokagua nikauliza kwa mamlaka yapi …Kwa katiba ipi hamuwezi kukagua alichokagua huyu haitwi kwenye kamati akija kwenye kamati anakuja tu kwa ridhaa yake,” alisema.

Akimtazama Mrema na Vullu, Rais alisema “Mkimwita kwenye kamati na akaja anawaheshimu tu nyie wazee, lakini hamuwezi kwenda kwenye kamati na kuhoji kazi yake haiwezekani.”
Chanzo: Mwananchi

3 comments:

Anonymous said...

Mmmh! Loading. Jairo in a safety net (no one is allowed to touch him huh!

Anonymous said...

mme ona mambo haya akishamteaua amekaa ametua na ufisadi uendelea kuvuta pumzi na kunyonya kwa kidizain ya kuteuliwa na kukaa na kutuwa.

heko hongera mkuuu wetu. kula kumi, akishateuliwa amekaa ametua habanduki na fanyeni mfanyalooo walala hoiiii ha ha ha kazi kweli ipo laki yote salaam na kheri tupu


Anonymous said...

ndo maana wanaunda katiba kwa ajili ya kupitisha ufisadi wao kuuhalalisha.

mafisadi daima wanateteyana wenyewe kwa wenyewe