ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, November 20, 2012

Jukwaa la Katiba ‘lamchefua’ Jaji Warioba

MWENYEKITI wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba 

MWENYEKITI wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, amesema Katiba Mpya itapatikana April mwaka 2014 kama kalenda ya tume hiyo, inavyoonyesha licha ya Jukwaa la Katiba Tanzania kukosoa hata ratiba ya mikutano ya utoaji wa maoni.

Amesema Jukwaa hilo linakosoa hata muda wa kufanya mikutano ambayo ni asubuhi na mchana na kuhoji kama jukwaa linataka kazi hiyo inafanyike usiku.
Jaji Warioba alisema hayo jana jijini Dar es Salaam, katika mkutano wake na waandishi wa habari "Hawa jamaa sasa wanakosoa kila kitu hata ratiba yetu ya kufanya mikutano asubuhi na jioni, hivi wanataka tuwe tunafanya mikutano usiku,” alihoji Warioba.
Alisema katiba hiyo itakuwa imekamilika katika kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 na kwamba  muda utakaobaki utatosha kuzifanyia marekebisho sheria zitakazohitajika baada ya mabadiliko ya Katiba Mpya.
Jukwaa la Katiba Tanzania, Jumamosi iliyopita lilitaka sheria ya mabadiliko irekebishwe, ili mchakato wa kupata Katiba Mpya uendelee baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
“Hawa jamaa wa Jukwaa la Katiba nawashangaa sana, wanataka tufuate wanayoyataka badala ya sisi kufuata sheria ya tume, tuna uzoefu wa kazi hii,” alisema Jaji Warioba.
Alisema, “ baada ya Katiba Mpya kupatikana Aprili mwaka  2014 kutakuwa na muda wa kutosha kuandaa sheria zitakazohitajika kutokana na mabadiliko hayo.”
Jaji Warioba ambaye aliwahi kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania, alisema anashangazwa na Jukwaa hilo kutaka sheria hiyo ifanyiwe marekebisho, wakati awali walikuwa wadau wakuu wa kutungwa kwake.
“Tumekuwa tukishirikiana na asasi mbalimbali na zimekuwa zikitutembelea kwenye mikutano ya utoaji wa maoni lakini nashangaa Jukwaa la Katiba, kila wakati limekuwa likikosoa kila kinachofanywa na tume,” alisema.
Kuhusu kuwafikia watu wenye ulemavu, Jaji Warioba alisema idadi kubwa ya kundi hilo limeshatoa maoni yake. “Kuna walemavu wa aina mbalimbali wameshatoa maoni yao, hata wasioona wameshatoa maoni yao kupitia maandishi ya alama za nundu,” alisema Jaji Warioba.
Akizungumzia zoezi la utoaji maoni, alisema limekuwa likiboreshwa siku hadi siku na kwamba hata watu waliokuwa wakitumwa na vyama vyao kutoa maoni ya aina fulani, sasa wameacha.
Akizungumzia awamu ya tatu ya utoaji wa maoni iliyomalizika hivi karibuni, alisema tume ilifanya mikutano 522 katika mikoa tisa.
Alisema jumla ya wananchi 392,385 walihudhuria mikutano na kwamba kati yao, 21,512 walitoa maoni yao kwa kuzungumza na wengine 84,039 walifanya hivyo kwa maandishi.
Alisema katika awamu ya nne iliyoanza jana, tume itakuwa na mikutano katika Mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Simiyu, Geita, Mara na Mjini Magharibi.
Alisema baada ya wananchi kumaliza kutoa maoni katika mikoa hiyo, Januari 7 mwaka 2013,  tume hiyo itaanza kupokea maoni kutoka katika taasisi mbalimbali.
“Tutakutana na taasisi mbalimbali vikiwemo vyama vya siasa, asasi za kiraia, asasi za kidini, vyama vya kitaaluma na wafanyakazi,” alisema Jaji Warioba.
Mwananchi

No comments: