ANGALIA LIVE NEWS
Tuesday, November 20, 2012
Kesi ya Uamsho
Sheikh Mussa Juma Issa, Sheikh Msellem Ali Msellem na Sheikh Farid Hadi Ahmed wakirejeshwa rumande baada ya kesi yao kupigwa tena tarehe na kibali cha dhamana kushindwa kufunguliwa
Na Salma Said, Zanzibar
SHEIKH Farid Hadi Ahmed na wenzake 7 wataendelea kusota rumande baada ya pingamizi yao ya dhamana kushindwa kufunguliwa na Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar (DPP), huku Sheikh Farid akitoa kibwagizo cha kukataa muungano.
‘Mnautaka’ …..aliuliza Sheikh Farid huku watu waliokuwepo nje ya mahakama kuitikia na kujibu ‘hatuutaki’ na kufuatiwa na takbir za hapo kwa hapo wakimaanisha Mwenyeenzi Mungu Mkubwa.
Mrajis wa Mahakama Kuu Zanzibar George Joseph Kazi alitoa uamuzi wake huo baada ya kusikiliza hoja zilizotolewa na pande zote mbili wiki iliyopita na kuutaka upande wa utetezi kuwasilisha malalamiko yao Mahakama Kuu juu ya madai ya ukiukwaji Katiba na sheria yanayodaiwa kufanyiwa watuhumiwa hao huko rumande.
Mrajis alisema kuwa, Mahakama Kuu ndicho chombo pekee chenye kutoa tafsiri na ufafanuzi wowote wa Katiba, na kwa mujibu wa sheria mahakama yake haina uwezo kisheria kusikiliza madai hayo yaliowasilishwa.
Uamuzi huo wa Mrajis umekuja kufuatia malalamiko ya ukiukwaji wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 na ukiukwaji wa haki za binaadamu wanaofanyiwa viongozi hao wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (JUMIKI) baada ya kuwasilishwa mahakamani hapo na mawakili wao watatu wakiongozwa na Salim Tawfik, Abdallah Juma na Suleiman Salum wiki iliyopita.
Mawakilishi hao waliiambiwa mahakama kuwa wateja wao huko katika magereza ya Kilimani wananyimwa haki zao za msingi za kuonana na ndugu na jamaa zao, wanafungiwa ndani saa 24 bila ya kuonana na mtu yeyote wakati watuhumiwa wengine waapewa fursa hiyo, wananyimwa haki ya kufanya ibada hasa sala ya Ijumaa, kunyimwa fursa ya kubadilisha nguo na kusababisha kuvaa nguo hizo hizo zaidi ya wiki tatu sasa, na pia kutengenishwa kila mtu chumba chake na kukataliwa kukutana na wenzao wakati wao bado ni watuhumiwa na hawajatiwa hatiani.
Madai mengine yaliowasilisha na mawakili hao ni kule kunyimwa fursa ya kuletewa vyakula kutoka nyumbani wakati watuhumiwa wenzao wanaletewa na kukatazwa kwenda kusali msikitini wakati katika magereza kuna msikiti na wenzao wote wanapata fursa hiyo ya kujumuika na wenzao kusali na pia kunyolewa ndevu wakati maafisa wa magareza wanafahamu kuwanyoa ndevu ni kuwadhalilisha wakati wakijua kufuga ndevu kwa muislamu ni sehemu ya ibada.
Awali Mahakamani hapo upande wa Mashitaka ulioongozwa na Mwanasheria kutoka ofisi ya Mkurgenzi wa Mashtaka Zanzibar (DPP), Ramadhan Nassib, alitetea hoja hizo na kuiambia mahakama hiyo kuwa suala hilo sio pahala pake na kuutaka upande wa utetezi kuwasilisha madai hayo Mahakama kuu ambayo ndiyo yenye uwezo wa kutoa tafsri na maelekezo ya ukiukwaji wa Katiba.
Wanasheria wengine wa upande wa waendesha mashtaka waliosikiza kesi hiyo kwa upande wa Mkurugenzi wa Mashtaka ni Rashid Fadhil na Raya Issa Mselem ambaye aliiomba mahakama hiyo kutupilia mbali hoja ya ukiukwaji wa haki za binaadamu kwa kuwa hapo sio mahali pale na kama wanataka wafungue madai katika mahakama husika.
Raya uliiomba mahakama hiyo kuiahirisha kesi hiyo na kuipangia tarehe nyengine kwa ajili ya kutajwa, kutokana na upelelezi kutokamilika.
Katika uamuzi wake, George Kazi ambaye pia ni hakimu wa mahakama ya mkoa Vuga, alisema mahakama yake haiwezi kutoa tamko la ukiukwaji katiba, na kufahamisha kuwa Mahakama Kuu ndiyo pekee yenye Mamlaka ya kusikiliza na kutoa maamuzi yanayohusiana na ukiukwaji wa Katiba.
Mrajis huyo wa Mahakama Kuu ameutaka upande huo wa utetezi kufungua madai yao hayo Mahakama Kuu, kwani ndicho chombo pekee chenye Mamlaka ya kusikiliza masuala ya Katiba na sio katika mahakama hiyo ambayo inasikiliza kesiinayowakabili watuhumiwa hao wanane.
Mrajis wa Mahakama Kuu alikubaliana na ombi lililowasilishwa kutoka upande wa waendesha mashataka kuiahirisha kesi hiyo hadi Novemba 29 mwaka huu kwa kutajwa.
Washitakiwa katika kesi hiyo ni Farid Hadi Ahmed (41) mkaazi wa Mbuyuni, Mselem Ali Mselem (52) wa Kwamtipura, Mussa Juma Issa (37) mkaazi Makadara na Azzan Khalid Hamdan (48) mkaazi wa Mfenesini.
Wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ni Suleiman Juma Suleiman (66) mkaazi wa Makadara, Khamis Ali Suleiman (59) mkaazi wa Mwanakwerekwe, Hassan Bakari Suleiman (39) wa Tomondo pamoja na Ghalib Ahmada Omar (39) mkaazi wa Mwanakwerekwe wote ni wakaazi wa Zanzibar.
Wote hao kwa pamoja wanakabiliwa na mashitaka ya uvunjifu wa amani, ushawishi wa kuchochea na kurubuni watu, kula njama pamoja na shitaka la kufanya kitendo kinachoweza kuleta uvunjifu wa amani, ambalo linamkabili Azzan Khalid Hamdan pekee yake.
Katika shitaka la uvunjifu wa amani chini ya kifungu cha 3 (d) cha sheria za Usalama wa Taifa sura ya 47 sheria ya mwaka 2002, washitakiwa wote hao walishitakiwa kwa kuhusishwa na matukio yaliyotokea Oktoba 17 na 18 mwaka huu kuanzia saa 12:00 za asubuhi hadi usiku wa manane.
Katika shitaka hilo, kupitia barabara tofauti zilizomo ndani ya mkoa wa Mjini Magharibi Unguja walidaiwa kuharibu barabara, majengo, vyombo vya moto na piki piki, na walifanya hivyo bila ya kuwepo sababu za msingi za kuharibu na kuteketeza kinyume cha maslahi ya umma na kusababisha hasara ya zaidi ya shilingi 5,000,000.
Shitaka la pili linalowakabili ni la ushawishi na uchochezi, ambapo ilidaiwa mahakamani hapo kuwa baina ya Mei 26 hadi Oktoba 19, 2010 watuhumiwa hao walifanya mikutano katika maeneo tofauti yakiwemo Lumumba, Msumbiji, Fuoni meli sita na Mbuyuni, ambayo kwa nyakati tofauti walishawishi na kuchochea watu kutenda makosa.
Makosa waliyodaiwa kufanywa ni kuweka vizuizi barabarani kwa kutumia mawe,, makontena ya kuhifadhia taka, matawi ya miti, mapipa ya mafuta, kuchoma maringi ya magari, kuharibu majengo tofauti, magari na kusababisha huduma muhimu za jamii za serikali kuweza kuharibwa na kusababisha hasara kuwa kwa watu binafsi na serikali.
Shitaka la mwisho kwa washitakiwa wote hao ni la kula njama, ambapo sehemu tofauti zisizojulikana pamoja na muda wake ndani ya wilaya ya Mjini Unguja, kwa pamoja walidaiwa kula njama ya kusababisha Farid Hadi Ahmed kujificha katika sehemu ambazo hazijulikani na kupelekea uvunjifu wa amani katika jamii na kuzusha taharuki maeneo mbali mbali ya Zanzibar.
Katika shitaka la nne la kufanya kitendo kinachoweza kuleta uvunjifu wa amani, linamuhusu kiongozi mmoja yaw a Uamsho ni Azzan Khalid Hamdan, ambalo katika shitaka hilo alidaiwa kumtolea maneno ya kashfa na matusi Kamishna wa Polisi wa Zanzibar Mussa Ali Mussa.
Mbali na kudaiwa kumshambulia kwa matusi Kamishna huyo lakini pia kiongozi huyo alidaiwa kumwambia Kamishna huyo kuwa mjinga, jambo ambalo mahakama ilidaiwa kuwa lingeliweza kusababisha uvunjifu wa amani katika jamii.
Washitakiwa hao pia wanatarajiwa kupandishwa tena katika mahakama ya wilaya Mwanakwerekwe, mbele ya hakimu Ame Msaraka Pinja, kwa ajili ya kuendelea na kesi ya uchochezi wa kufanya fujo inayowakabili ambapo wiki iliyopita walipewa sharti gumu la dhamana ya kila mmoja kutakiwa kuwasilisha shilingi million moja taslimi na wadhamini watatu na kila mmoja aje na kiwango hicho cha fedha na awe na barua ya sheha na awe na kitambulisho vya mzanzibari mkaazi na lazima wadhamini hao wawe ni wafanyakazi wa serikali ya mapnduzi Zanzibar.
Wakati huo huo Sheikh Farid aliwafurahisha wananchi waliokuja kusikiliza kesi hiyo nje ya Mahakama Kuu baada ya kuwauliza ‘Mnautaka Muungano? Na watu hao kujibu ‘Hatutaki’ hii ni mara ya pili kwa Sheikh Farid kusema maneno wakati akipanda gari kurejesha rumande wiki iliyopita alisema ‘Haki haifichwi lazima itakuja juu siku moja’ wakati Sheikh Azzan akisema ‘Zanzibar Kwanza’.
Kesi hiyo imekuwa ikisikiliza katika mahakama kimya kimya bila ya kuruhusiwa kuingia ndugu na jamaa za watuhumiwa hao lakini wamekuwa wakisubiri nje na ndipo leo wakashangiriwa walipowaona wakitolewa ndani na kuanza kuwapigia takbir wakimaanisha Mungu Mkubwa mahakamani hapo.
Naye kwa upande wake Sheikh Mussa Juma Issa leo amewataka waandishi wa habari kwenda gerezani kuchukua taarifa na wasitosheke kuchukua taarifa za mahakamani kwa kuwa katika magereza ya Zanzibar kuna ukiukwaji wa haki za binaadamu wanaofanyiwa mahabusu.
“Msiichie na kuridhika kuandika habari za mahakamani, waandishi njooni na gerezani mje kuona unyanyasaji tunaofanyiwa sisi kule” alisema Sheikh Mussa.
Kesi hiyo imekuwa ikisikilizwa ndani na wenye kuruhusiwa kuingia ndani ni maafisa wa polisi wa usalama, jeshi la polisi na baadhi ya waandishi wa habari wachache hata hivyo ulinzi katika maeneo yote uliimairishwa huku badhi ya maafisa usalama wakiwa wametanda katika kila kona ya mahakama hiyo iliyopo Mji Mkongwe wa Unguja.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment