ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, November 20, 2012

KUSAFISHA RUSHWA CCM `Mangula hana ubavu`

Rais Jakaya Kikwete (katikati) akizungumza na Makamu Mwenyekiti Bara CCM, Phili Mangula (kulia) na Dk. Ali Mohamed Shein (kushoto) Picha na Ikulu.
Baadhi ya wanasiasa na wasomi wamesema Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Philip Mangula, hana ubavu wa kuwang’oa viongozi walioingia katika uongozi kwa njia za rushwa.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Paulo Luisulie, amesema Mangula hana ubavu wa kufanya hivyo kutokana na viongozi wengi katika CCM kuingia madarakani kwa njia za rushwa.
Alisema Katibu Mkuu wa Chama hicho, Abdulharaman Kinana, alikaririwa akisema wakuu wa kamati za maadili katika mikoa na wilaya ni wenyeviti wa mikoa na wilaya ambao wengi wao wanalalamikiwa kuwa wamepata vyeo hivyo kwa njia za rushwa.
“Hapa nani wa kumfunga paka kengele, hawa wengi wote wanaotakiwa kuchukua hatua, wanadaiwa kuingia madarakani kwa rushwa. Tatizo hapa ni mfumo mzima wa chama hiki ambao unatakiwa kufanyiwa kazi ili aweze kufanikiwa katika hili,” alisema na kuongeza: “Na wenyewe (CCM) ni mashuhuda katika jambo hili kwamba Jumuiya ya Wazazi, Jumuiya ya Wanawake Tanzania (UWT) na ile ya Vijana (UVCCM), pamoja na wengi wa wajumbe wa Halmashauri Kuu (Nec), wameingia kwa rushwa, Mangula anakwenda kupambana na hawa, hana ubavu huo.”
Mhadhiri huyo alisema mpango huo wa Mangula utakuwa kama dhana ya kuvuana ‘magamba’ ambayo imeshindikana kutekelezwa hadi sasa katika chama hicho.

“Namuonea huruma sana Mzee Mangula kwa jinsi atakavyoweza kutekeleza hayo kwa kuwa anaokwenda kufanya nao kazi ni wale wale walioshindwa kuitekeza dhana ya kuvuana ‘magamba’. Sifahamu ni mfumo gani ambao utamsaidia katika kufanikisha hili,” alisema.
Hata hivyo, alisema jambo la kupongeza ni kwamba Chama hicho kimegundua kuwa kina shida kubwa ambayo inakisumbua katika ya jamii ya Kitanzania.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha St. John mkoani Dodoma (SJUT), Profesa Gabriel Mwaluko, alimtakia kila la kheri Mangula kwa kusudio lake la kutaka kukitoa CCM kilipo na kukirudishia heshima kilichokuwa nayo huko nyuma.
“Tusimuuingize Mangula kwenye sera ya kuvua magamba, hakuwepo wakati huo na ndio maana Chama kilimchagua kushika nafasi hiyo.

Kwa tunaomfahamu vyema Mangula tuna imani kuwa ataturejesha katika heshima tuliyokuwa nayo, namtakia kila la kheri,” alisema Profesa Mwaluko ambaye alikuwa mmoja wa wagombea ubunge katika Jimbo la Dodoma Mjini.
Profesa Mwaluko aligombea ubunge mwaka 2010 kwa tiketi ya CCM na kubwagwa na Mbunge wa sasa, David Malole katika kura za maoni.

Mhadhiri wa Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Ruaha (RUCo) mkoani Iringa, Rwezaura Kaijage, alisema kwa uzoefu uliopo mara nyingi kauli kama ya Mangula zimekuwa zikitolewa na viongozi wapya wanaoingia madarakani, lakini ajenda zao baadaye hukosa matokeo chanya ya kile walichokiahidi.

“Ili mzee Mangula atekeleze azma yake aliyokuja nayo inabidi apate sapoti ya watu wengine kwa sababu kufanikiwa au kushindwa kwake baadaye kutategemea sana safu aliyonayo. Hii inatokana na uzoefu tulionao kwamba ajenda hiyo si ngeni katika siasa za Tanzania ,” alisema Rwezaura.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana, alisema kauli ya Mangula ni ya kisiasa na siyo ya kisayansi kwani kinachotakiwa kwa CCM ni kufanya uchunguzi kwanini watu wanatoa rushwa ili wapate uongozi.

“Suala la rushwa ndani ya CCM na jamii kwa ujumla linahitaji utafiti wa hali ya juu, inatakiwa CCM washirikiane na taasisi nyingine kubaini sababu za kukithiri kwa rushwa kwenye chaguzi na wanaotoa ni akina nani ili waweze kuchukuliwa hatua,” alisema Dk. Bana.

Dk. Bana, ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Siasa na Utawala wa chuo hicho, alisema Mangula lazima atambue kuwa rushwa haiwezi kushughulikiwa kwenye majukwaa ya kisiasa hivyo Kamati ya Maadili ijipange kuwabaini watoa rushwa na hizo pesa wanazitoa wapi na kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria.

Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo hicho, Dk. Xvery Lwaitama, alisema utekelezaji wa kauli ya Mangula ni mgumu kwa sababu inamaanisha kuwa haya yeye mwenyewe (Mangula) alipigiwa kura na wala rushwa.
“Kwanza hakuna orodha yaw ala rushwa iliyopelekwa kwenye Mkutano Mkuu wa CCM, kama kuna wala rushwa ndani ya CCM ina maana waliomchagua itawezekana vipi akawaondoa,” alisema Dk. Lwaitama.

Alisema hatua ya viongozi wa CCM akiwamo Mangula kunyosheana vidole kuhusu rushwa itakibomoa Chama ambacho kwa wakati huu kilitakiwa kiwe kinajipanga kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Tanzania Bara, Julius Mtatiro, alisema Mangula hana uwezo wa kupambana na rushwa ndani ya CCM kwa sababu amekuwepo ndani ya chama hicho kwa muda mrefu, lakini hakuweza kufanya kazi hiyo.

“Mangula amekuwa kiongozi ndani ya CCM miaka nenda rudi, sasa leo ameshuka toka mbinguni hadi aweze kumudu kupambana na rushwa, huo ni uongo na ni danganya toto tu,” alisema Mtatiro.

Alisema CCM kimekuwa chama cha kusema uongo huku akitolea mfano kuwa walipochukua nchi, walisema kuwa kitakuwa chama cha wakulima na wafanyakazi, lakini leo hii kimekuwa cha wafanyabiashara.

Naye Mkurugenzi wa Mafunzo na Oganaizesheni wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Benson Kigaila, alisema Mangula hawezi kuwa na jipya ndani ya CCM kwa sababu amekuwa kiongozi na ufisadi wote ulifanyika akiwepo.

Kigaila alisema anawashangaa watu wanaosema Sekretatieti ya CCM ni mpya na itaweza kuleta mabadiliko ndani ya chama hicho wakati viongozi wote waliochaguliwa wamekuwepo na bado hakikufanya mabadiliko yeyote.
Chama cha APPT Maendeleo kimesema Mangula, ana uwezo wa kupambana na rushwa na ufisadi ndani ya chama chake kwa sababu hana kashfa kama ilivyo kwa baadhi ya wanachama na viongozi wa chama hicho.
Mwenyekiti wa Chama hicho, Peter Kuga Mziray, alisema Mangula ana uwezo wa kupambana na rushwa ndani ya CCM kwa sababu ni kiongozi pekee ambaye hana kashfa na hapendi rushwa jambo ambalo litaleta matumaini ndani ya Chama hicho.

“Mangula ni tofauti na wana CCM wengine, ana sifa kubwa ya kutopenda rushwa na ufisadi pia hana tamaa,” alisema Mziray.
Alisema ili aweze kufanikiwa katika vita ya rushwa ndani ya chama hicho, sekretarieti mpya iliyochaguliwa inatakiwa kuwa kitu kimoja kwa kuhakikisha haiyumbi katika maamuzi yake kama ilivyojitokeza kwa viongozi waliopita.
Mziray alitoa mfano suala la kujivua gamba ambalo lilishikiwa kidedea na viongozi wa CCM, lakini hadi sasa suala hilo halijatekelezwa na kuacha maswali mengi yasiyokuwa na majibu kwa Watanzania.

Alisema pamoja na sekretarieti ya CCM kuonekana kujipanga vizuri kukirejesha chama kwenye mstari, lakini kutokana na baadhi yao kuwa na umri mkubwa wanaweza wakashindwa kuhimili kasi ya siasa ya kipindi hiki.
Mangula akizungumza juzi katika viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam, wakati wa sherehe zilizoandaliwa na viongozi wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam kuwapongeza viongozi wapya, alisema walioshinda katika chaguzi za chama hicho kwa rushwa wajiandae kung’olewa ndani ya miezi sita.
Imeandikwa na Thobias Mwanakatwe, Dar, Godfrey Mushi, Iringa na Sharon Sauwa, Dodoma.  
CHANZO: NIPASHE

No comments: