ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, November 25, 2012

MAISHA NDIVYO YALIVYO: Mwenzio akiomba msamaha kwa kosa alilokukosea, kubali yaishe!



 Mpenzi msomaji, utakumbuka wiki iliyopita nilikuletea hapa kisa cha kijana mmoja aliyesalitiwa na mpenzi wake wakati wa uchumba. Hivi sasa ni miaka miwili tangu wameoana na wamebahatika kupata mtoto mmoja.

Bibie akakumbuka jambo alilomkosea mwenzake wakati wa uchumba akamuomba msamaha. Lakini kijana jambo hilo likamuuma na sasa anaomba ushauri. Na bado alikuwa hajakubali msamaha huo. Wapo wasomaji wengi wamempa ushauri kuwa amsamehe mwenzake.

Hata hivyo, miongoni mwa wadau hao, yupo aliyetoa ushauri kwa kijana mwenzake huyo, huku akimtahadharisha hasa ikizingatia kwamba naye yaliwahi kumkuta kama hayo lakini ilibidi waachane na mwenzake. Uamuzi huo anaujutia hadi leo. Hebu tumsikie anasemaje kupitia ujumbe mfupi wa simu na mwisho wasomaji wengine nao wana maoni yao.
Msomaji huyu wa Dodoma anaanza ujumbe wake namna hii: “Nimesoma mada yako kwenye gazeti la NIPASHE Jumapili! Ushauri wako umenigusa kwani na mimi ni mwathirika wa huo mkasa mpaka leo nateseka na hatma yangu siijui.

Namshauri huyo jamaa kwa kuwa mwanamke wake alimwambia ukweli hana budi kumkumbatia na kuilinda familia yake inavyopaswa. Karne hii ni wanawake wachache ambao wanaweza kuwatii kwa kiasi hicho cha kusema ukweli na kujutia kwa kosa lililopita. Nampongeza sana huyo mdada huyo.

Nitoe ushuhuda wangu mwenyewe…Mimi nina umri wa miaka 35. Nilikuwa na mpenzi niliyedumu naye kwa miaka mitatu. Ikatokea akanisaliti katika kipindi hicho. Baadaye akaniambia ukweli na kunitaka radhi. Iliniuma sana.

Nilikuwa nampenda na kumuamini sana. Nilimsamehe lakini moyo wangu ulikuwa mgumu kusahau nikajikuta amani na furaha vinatoweka nikawa sitimizi majukumu yangu kwake kama ilivyokuwa awali.

Naye akakosa matumaini ikabidi tuachane. Lakini mpaka sasa najuta kwa kuruhusu hali iliyotokea ya kuachana. Nilijaribu kumfuata mara kwa mara na kumtaka arudi bila mafanikio. Tangu tulipoachana nimekuwa na mahusiano ambayo mpaka sasa sijapata mwanamke ambaye ananifaa kama ilivyokuwa huyo wa awali. Kitu kinachonifanya mpaka leo nishindwe kutimiza ndoto zangu!

Huyo jamaa anatakiwa asiharibu maisha yake kwa kosa la siku moja. Asante sana (GR, Dodoma)

…Mimi naitwa Joseph Kiwia napenda kumshauri huyo jamaa amsamehe kwani kama ameweza kujishusha na kuomba msamaha ana nia nzuri ya kuongoza familia.

…..Mwingine anasema; “kwanza nampa pole huyo kijana. Pia amsamehe mkewe maadam kaamua kusema mwenyewe kwani huyo katambua kosa lake. Pia nadhani hawezi kurudia na ni furaha kuambiwa ukweli kwani wengine hawasemi wanarudia kwa siri.

Huyo msamehe, jifikirie wewe binafsi umetembea na wangapi ndio ukampata yeye? Msamehe nawe usije lipa kisasi ni dhambi.(Mama Lulu, Kitunda).

Mpenzi msomaji, bila shaka umewasikia wasomaji wenzetu hao walivyompa ushauri kijana niliyemjadili mada iliyopita. Utaona kuwa kumbe visa vya aina hii huwapata watu wengi lakini humezea na kuugulia moyoni. Kwa mfano kijana huyo wa Dodoma aliyempa mwenzake ushauri lakini pia hakusita kueleza yaliyomsibu akiyalinganisha na yaliyompata kijana mwenzie. Tena tatizo lake yeye ni baya zaidi kwani ilifikia hatua waachane na mwenza wake na anajutia uamuzi ule kwani hadi sasa hajapata mwanamke anayemfikia yule aliyemuacha.
Hakika hili ni funzo kwa vijana kwamba wakati mwingine maamuzi ya pupa huleta madhara makubwa yaziyoponyeka. 
Kama kwa Mungu kuna msamaha, kwanini usisamehe hata pale mwenzako anapokiri kosa na kuomba msamaha?  Na ni vema tukumbuke ule msemo wa wahenga kwamba kufanya kosa siyo kosa bali kurudia kosa. Kama mwenzako kafanya kosa akakwambia na kuomba msamaha na wala hajalirudia kosa hilo, kwanini usimsamehe?

Tujifunze kuwa wavumilivu na wepesi wa kuhimili mambo na ikibidi kuchunguza kabla ya kuchukua hatua stahiki. Siyo kila kosa mtu anachukua maamuzi magumu bila kufanya uchunguzi wa kina na kujiridhisha kuhusu uwezo wa kuhimili matokeo yake.

Jamaa wa Dodoma anajutia uamuzi wa kumuacha mwenzake aliyemuomba masamaha. Sasa anajutia uamuzi ule kwani kila akimbembeleza mtalaka wake anamkatalia na katu hajapata mbadala, kila ampataye ni mbabaishaji. Kuacha kuna gharama! Au siyo msomaji wangu? Kubwa likiwa ni namna ya kuanza mahusiano mapya.  Vijana yafaa wajifunze kutoka kwa vijana hao wawili. Mwenzio akiomba msamaha kwa kosa alilokukosea, kubali yaishe, vinginevyo mikosi yaweza kukuandama hadi uchanganyikiwe. 

Naam. Hayo ndiyo mambo mpenzi msomaji wangu. Kama unalo jambo lako, mkasa, unataka tuujadili kwa pamoja usisite kunibonyezea ujumbe.

Ukiwa na maoni, ushauri kuwa huru kuwasiliana nami kwa kutuma ujumbe mfupi kupitia simu ya ofisi namba 774268581(usipige), au barua pepe; fwingia@gmail.com
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

1 comment:

Anonymous said...

Jamani kweli ,haya mambo yapo.tumeyaona na yametukuta.mmmm,wanaume hawaaminiki hata kidogo,ndio maana mungu anawafundisha ,mtu anafanya kosa lakini ataki kujirekebisha.mpaka ujui umsaidie vipi.