ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, November 20, 2012

Stars yahofia Ebola Uganda

Baadhi ya wachezaji wa timu ya Taifa (Taifa Stars), wakifanya mazoezi kujiandaa na mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Kenya wiki iliyopita. Stars inatarajia kushiriki michuano ya Chalenji, Uganda baadaye mwezi huu. Picha na Maktaba.

BARAZA la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), limeziondoa hofu ya tishio la ugonjwa wa Ebola timu za taifa zitakazoshiriki michuano ya Chalenji, Kampala, Uganda
Timu ya Taifa ya Tanzania (Kilimanjaro Stars) ni miongoni mwa timu zitakazoshiriki michuano hiyo ya mwaka huu itakayoanza Novemba 24 mpaka Desemba 8.
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema jana kuwa wamepokea barua kutoka Cecafa ikiwahakikishia usalama wa afya za wachezaji wote.
"Juzi tulipokea barua kutoka Cecafa ikituhakikishia usalama wa wachezaji wetu (Kilimanjaro Stars)," alisema Wambura.
Wambura alisema barua hiyo ya Cecafa ni jibu la barua yao waliyoituma wakiuliza juu ya usalama wa afya kufuatia kuwapo taarifa za ugonjwa wa Ebola.
"Cecafa iliwasiliana na Wizara ya Afya ya Uganda ambayo iliwahakikishia hakuna tishio la Ebola Kampala,".
Shirikisho la Soka Kenya (FKF), nalo limeomba kuhakikishiwa usalama wa wachezaji wake kama walivyofanya wenzao TFF.
"Tumeomba mwongozo juu ya suala hili kutoka mamlaka zinazohusika, Shirika la Afya Duniani (WHO) na Wizara ya Afya kabla ya kupeleka timu," alisema Katibu Mkuu wa FKF, Joseph Agola.
Wakati huohuo, nahodha wa Kilimanjaro Stars, Juma Kaseja amesema pamoja na kikosi chao kushindwa kufanya vizuri kwenye michuano hiyo ugenini, hali hiyo kamwe haiwezi kuwakatisha tamaa mwaka huu.
Stars haijawahi kutwaa ubingwa wa Chalenji nje ya Tanzania tangu ilipofanya hivyo mara ya mwisho mwaka 1965 nchini Uganda.Kaseja alisema dhamira yao kufanya vizuri haijapotea, na kwamba wasingependa historia ya kuboronga kwenye mashindano hayo ijirudie tena.
Alisema tofauti na miaka ya nyuma, kikosi cha mwaka huu kina wachezaji wazuri, huku wengi wao wakiwa vijana.Stars inatarajiwa kurejea Dar es Salaam kutoka Mwanza Novemba 23 kwa ajili ya mapumziko mafupi kabla ya kwenda Uganda.
Mwananchi

No comments: