ANGALIA LIVE NEWS

Friday, November 2, 2012

Ulinzi mkali Kisutu

 
*Watu wakaguliwa kwa mitambo maalum
  *Kundi kubwa la askari lazingira mahakama
  *Amri ya kumfutia dhamana yaendelea

Ulinzi mkali jana uliimarishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam kabla ya kesi inayomkabili Sheikh Ponda Issa Ponda na wenzake 49 kutajwa.

 Ponda na wenzake hao wanakabiliwa na mashtaka matano ikiwamo kula njama, kuingia, kujimilikisha ardhi kwa jinai, wizi wa mali ya Sh. milioni 59.6. Sheikh huyo pia anakabiliwa na shtaka la kufanya uchochezi wa kuhamasisha wafuasi wake kutenda makosa.



WATU WAKAGULIWA KWA MITAMBO

NIPASHE lilishuhudia watu waliokuwa wakipita kwenye lango la kuingilia mahakamani hapo kila mmoja akifanyiwa upekuzi kwa kutumia mitambo maalum ya CCTV.

Vile vile, lilishuhudia makachero waliovaa kiraia ambao haikujulikana kama wanatoka kwenye majeshi ya ulinzi na usalama wa raia au la, wakiwa wametanda katika maeneo mbalimbali ya Mahakama hiyo ili kuhakikisha yanakuwa na amani na utulivu kabla na baada ya washtakiwa hao kufikishwa mahakamani hapo.

Kadhalika, kulikuwa na  ulinzi wa askari polisi na magereza waliovaa vifaa maalum, vikosi vya mbwa na farasi.



Ilipofika majira ya saa 2:00 asubuhi,  askari ambao idadi yao haikujulikana waliovaa sare za polisi na magereza, walisambaa katika viunga vya mahakama hiyo.

Mitambo hiyo ikiwa imefungwa karibu na geti la kuingia mahakamani hapo, ilitumika kuchunguza kila mtu aliyekuwa akiingia na magari.

Makachero hao walizuia watu wote waliofika eneo la lango kuu la kuingilia mahakamani hapo na kuwaruhusu wafanyakazi wa mahakama hiyo, watu waliokuwa na kesi na waandishi wa habari.

DHAMANA YA PONDA BADO IMEFUNGWA


Baadaye saa 2:30 asubuhi, Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Victoria Nonga, aliwasomea washtakiwa 49 masharti ya dhamana isipokuwa Sheikh Ponda ambaye ni mshtakiwa namba moja kwa kuwa  Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) hajaondoa pingamizi la dhamana dhidi yake.

Washtakiwa hao walitakiwa kuwa na mdhamini mmoja kila mmoja atakayesaini hati ya dhamana ya Sh. milioni moja.

Hakimu Nongwa alisema mshtakiwa atakayetimiza masharti ataachiwa kwa dhamana.
Hadi NIPASHE linaondokana mahakamani hapo, washtakiwa hao walishindwa kutimiza masharti ya dhamana na kurudishwa mahabusu hadi Novemba 15, mwaka huu, kesi hiyo itakapotajwa tena.

Kabla ya kuahirisha kesi hiyo, Wakili Mwandamizi wa Serikali, Tumaini Kweka, alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na kuiomba Mahakama hiyo kupanga tarehe ya kuwasomea washtakiwa hao maelezo ya awali.

Hakimu Nongwa alikubaliana na ombi hilo na kuahirisha kesi hiyo hadi Novemba 15, mwaka huu.

Oktoba 18, mwaka huu washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza na kusomewa mashtaka, lakini DPP, aliwasilisha hati ya kiapo cha kupinga dhamana ya Sheikh Ponda kwa usalama wake na maslahi ya Taifa.

Washtakiwa wengine ni Kuluthumu Mohamed,  Zaldah Yusuph, Juma Mpanga,  Farida Lukoko,  Adamu Makilika, Athum Salim, Seleman Wajumbe, Salum Juma, Salum Mkwasu na Ramha Hamza.

Wengine ni Halima Abas, Maua Mdumila,  Fatihiya Habibu, Hussein Ally, Shaban Ramadhani, Hamis Mohamed, Rashid Ramadhani, Yusuph Penza, Alawi Alawi, Ramadhani Mlali,  Omary Ismaili, Salma Abduratifu,  Khalidi Abdallah,  Said Rashid,  Feswali Bakari,  Issa Wahabu, Ally Mohamed,  Mohamed Ramadhani, Abdallah Senza, Juma Hassani na Mwanaomary Makuka.

 Wengine ni Omary Bakari,  Rashid Ndimbu,  Hamza Ramadhani, Ayubu Juma, Maulid Namdeka,  Farahan Jamal,  Smalehes Mdulidi, Jumanne Mussa, Salum Mohamed, Hamis Halidi, Dite Bilali, Amiri Said, Juma Yassin, Athuman Rashid, Rukia Yusuph, Abubakari Juma na Ally Salehe.

Upande wa mashtaka ulidai kuwa katika shtaka la kwanza, Oktoba 12, mwaka huu huko Temeke jijini Dar es Salaam, washtakiwa wote 50 walikula njama ya kutenda makosa.

Katika shtaka la pili, ilidaiwa kuwa siku ya tukio la kwanza, eneo la Chang’ombe Markas, Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam, washtakiwa hao kwa jinai walivamia kwa nia ya kutaka kujimilikisha kiwanja mali ya Agritanza Ltd.

Ilidaiwa kuwa katika shtaka la tatu kuwa, kati ya Oktoba 12 na 16, mwaka huu katika eneo la Chang’ombe Markas pasipo uhalali na hali ya uvunjifu wa amani, washtakiwa hao walijimilikisha ardhi hiyo.

Katika shtaka la nne, ilidaiwa kuwa kati ya Oktoba 12 na 16, mwaka huu karika eneo hilo, washtakiwa hao waliiba vifaa mbalimbali vya ujenzi yakiwamo matofali 1,500, tani 36 za kokoto na nondo vyenye thamani ya Sh. 59,650,000.

Upande wa Jamhuri ulidai katika shtaka la tano kati ya Oktoba 12 na 16, mwaka huu huko Chang’ombe Markas, Sheikh Ponda akiwa Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislam Tanzania, aliwashawishi wafuasi wake kutenda makosa ya jinai. Washtakiwa hao walikana mashtaka dhidi yao.
CHANZO: NIPASHE

No comments: