ANGALIA LIVE NEWS

Monday, January 7, 2013

Baraza la Madiwani Arusha lasalimu amri kwa Serikali

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi) Hawa Ghasia 

BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, hatimaye  jana limeidhinisha kuliachia eneo la Lakilaki  lililopangwa kujengwa mji wa mfano wa Arusha (Arusha Safari Town)  na kukabidhi hati miliki ya ardhi hiyo, kwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya Taasisi za  Umoja ya Mataifa na Jumuiya ya Afrika ya Mashariki.
Uamuzi huo ulifikiwa jana katika kikao cha dharura cha baraza la madiwani wa halmashauri hiyo, ambacho kilihudhuriwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi) Hawa Ghasia,  baada ya Serikali kukubali kulipa  mkopo  uliokopwa na halmashauri hiyo  Benki ya Biashara ya Afrika (CBA), kiasi cha Sh8.6 bilioni sambamba na kurejesha gharama za mradi huo kiasi cha Sh788.2 milioni na faida ambayo halmashauri hiyo ingepata kiasi cha Sh5.6 bilioni.
Akizungumza mara baada ya madiwani hao kupitisha maombi ya kuchukuliwa eneo hilo, Waziri Ghasia  aliwapongeza madiwani hao kwa kukubali kuliachia eneo hilo na kueleza  Serikali itarejesha  gharama zote za halmashauri hiyo.
“Lengo la serikali kutolewa eneo hili kwa Wizara ya Mambo ya Nje ni kuwapa Umoja wa Mataifa na taasisi zake, ikiwepo pia Jumuiya ya Afrika ya Mashariki ili waweze kujenga majengo yao kwa manufaa ya taifa zima,” alisema Waziri Ghasia.
Hata hivyo baadhi ya madiwani walieleza kutilia shaka uamuzi wa Serikali kuchukuwa ardhi hiyo na kutoa ahadi kwa mdomo ya kulipa gharama zote, hatua ambayo ilimlazimu waziri huyo, kutoa ufafanuzi wa malipo ya halmashauri hiyo.
“Ndugu zangu kabla ya leo kuja hapa, tulikuwa katika kikao cha kutafuta muafaka wa jambo hilo, ambacho kiliongozwa na Katibu Mkuu Kiongozi na Watendaji toka ofisi ya Mwanasheria mkuu wa Serikali, Wizara ya Ardhi, Maendeleo ya Makazi na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na suala la malipo tumekubali serikali italipa”alisema Waziri Ghasia.
Waziri huyo pia  alisema, Rais Jakaya Kikwete alikuwa akifuatilia kupatikana kwa ardhi hiyo na ameiondoa hofu halmashauri hiyo kupoteza fedha ambazo tayari wametumia na ambazo wangepata kama wangetekeleza mradi huo.
“Jamani mimi ni mtu mzima siwezi kuja hapa kusema ahadi ambazo hazipo, ninawahakikishia mtalipwa na mimi tayari niliandika barua kuelezea jambo hili naomba muiamini Serikali yenu ahadi hii siyo yangu ni ya Serikali” alisema Waziri Ghasia.
Awali Mkurugenzi wa Halmashauri ya Arusha,  Halfani Hida alisema mradi wa awali kama ungetekelezwa tayari walikuwa wamepima jumla ya viwanja  348 ambavyo vingegawanywa kwa wananchi na kuipatia  halmashauri hiyo mapato ya Sh13.3 bilioni, pia viwanja vya biashara vingeingiza mapato ya Sh1.7 bilioni huku maeneo ya huduma yalitarajiwa kuingiza Sh332.6 milioni.
Mwananchi


No comments: