KIPINDI fulani mwaka jana, gazeti hili lilichapisha mfululizo wa makala kuhusiana na masuala ya masoko ya hisa na dhamana za mitaji.
Katika kipindi chote na hata sasa, baadhi ya watu wamekuwa wakiwasiliana na gazeti hili wakitaka kujua zaidi kuhusu masuala mbalimbali ya aina hiyo ya uwekezaji.
Kwa mfano, wengi wanahoji kuhusiana na hisa ambazo wamenunua katika kampuni tofauti, wanataka kujua hatma ya fedha zao kwa kuwa tangu wawekeze, hawajapata mrejesho kutoka kwa watendaji wa kampuni husika kuhusu kinachoendelea.
Pia kuna wanaotaka kujua watafanyaje ili waweze kuuza hisa zao, baada ya kuvuna faida kwa muda fulani katika kampuni zinazozalisha faida. Wengine wako njia panda kwani, hawajui hata zilipo dhamana zao.
Kwa mfano, wakati wanahisa wa kampuni ya Nicol hawajui watawapata wapi viongozi wa kampuni hiyo, kupata ufafanuzi na kujua zilipo fedha zao, wenzao wa kampuni ya Gesi (Tol), wanalia kuwa hawajaona gawio kitambo sasa, licha ya ukweli kuwa gesi inauzwa mitaani na matumizi yake yanazidi kuongezeka.
Hisa na mitaji
Hisa na mitaji
Bado asilimia 84 ya Watanzania wote nchi nzima hawana elimu ya kutosha kuhusiana na masoko ya hisa na uwekezaji.
Hali hiyo inatokana na ukweli kuwa nchini hakujawa na mafunzo, elimu na utambuzi mwingine wa masoko ya hisa, hivyo kuwafanya watu ambao wanataka kuwekeza katika eneo hilo kukosa pa kuanzia na wengine kujikuta wakifuata matangazo au vipeperushi bila kujua misingi inayohitajika kabla ya ununuzi.
Kulingana na takwimu za Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE), hadi hivi karibuni kulikuwa na kampuni 16 ambazo zilisajiliwa sokoni hapo, Nicol ikiwa sio mojawapo.
Kampuni hizo zimeuza hisa zake kwa asilimia 0.39 ya Watanzania wote nchi nzima, ambao wamewekeza katika eneo hilo kulingana na takwimu za vyanzo mbalimbali.
Kulingana na tafsiri za kibiashara, dhamana za mitaji ni wigo mpana ambao unajumuisha pia hisa, vipande, hatifungani na amana za Serikali.
Kibiashara hisa zinaelezwa kuwa ni kitega uchumi, biashara, dhamana za mkopo na ni mtaji au akiba ambayo ipo kwa ajili ya kumuwezesha mwekezaji kuvuna faida kulingana na kile kinachopatikana kutoka kampuni husika.
Pia wawekezaji wanaweza kuvuna faida kutokana na ongezeko la thamani za hisa, lakini uwekezaji katika eneo hilo unahitaji elimu ya utambuzi wa hisa ili kujua ununue wapi hisa kwa misingi ya kupata faida, ikiwa ni pamoja na kuwa na hesabu za kampuni husika na mwenendo wa fedha kiuchumi.
Elimu inahitajika kutokana na ukweli kuwa soko la hisa kama zilivyo biashara zingine, linakabiliwa na vikwazo kadhaa ambavyo wawekezaji katika eneo hilo wanapaswa kuvifahamu.
Vikwazo hivyo ni pamoja na kushuka kwa bei za hisa sokoni, kukosa gawio na mfumuko wa bei, viwango vya riba, kukosekana wanunuzi wa hisa katika kampuni husika na punguzo la kodi ya zuio kwenye gawio, mambo ambayo kama yasipofahamika vema kwa wanajamii yanaweza kushusha ari ya uwekezaji katika hisa.
Kutokana na hali hiyo ni wazi kuwa elimu inahitajika sasa kuliko wakati mwingine, kutokana na ukweli kuwa kampuni nyingi zaidi zimejitokeza kuuza hisa zake DSE. Hii ni ishara kuwa Watanzania wengi wana shauku ya kuwawekeza katika eneo hilo.
Takwimu kuwa asilimia 84 ya Watanzania wote, hawana elimu kuhusiana na aina hii ya uwekezaji, ni wazi kuwa kuna walakini ambao unahitajika kufanyiwa kazi ikiwa ni pamoja na kushirikisha taasisi binafsi.
Serikali haipaswi kukaa kimya kuhusiana na upungufu huo ambao unafifisha mzunguko wa fedha katika eneo hilo.
Aidha, kuwepo na utaratibu wa wazi wa upatikanaji wa taarifa za mwenendo wa fedha wa kampuni ambazo zimesajili hisa zao DSE.
Uwazi na kuwepo kwa sehemu ya kueleweka ya kupata habari kuhusiana na masuala ya hisa na dhamana nje na ndani ya Dar es Salaam, kutasaidia kuwafanya wananchi kutambua kwa undani makampuni ambayo hisa zao zipo sokoni na mwenendo wao kifedha.
Pia hali hiyo itawawezesha kuwa na chaguo, badala ya ilivyo sasa ambapo walio wengi wanaongozwa na matangazo ambayo hayaonyeshi mwenendo wa kampuni kifedha.
Kinyume cha hivyo ni wazi kuwa wananchi wataendelea kubahatisha kwa kuwekeza katika makampuni ambayo kumbukumbu zake kifedha hazieleweki, hivyo kuwafanya wajikute wanaingia katika utata ambao unawakwamisha kiuchumi.
Kwa wananchi ambao wamewekeza Nicol, ingawa inaelezwa na watendaji wakuu wa kampuni hiyo kuwa fedha zao zipo salama, bado wapo gizani kwani hawajui kitu gani kinaendelea na lini watapata fedha zao.
Serikali nayo inapaswa kuondoa mkanganyiko uliopo kwa kuyaweka wazi makampuni yanayoyumba, huku ikiendelea kutoa elimu ya kutosha kwa minajili ya kulinda fedha za wananchi na kujenga imani kuwa aina hiyo ya uwekezaji inawezekana.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment