Uongozi wa juu wa Chama cha Demokrasia (Chadema), ukiongozwa na Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe (wa pili kushoto), Naibu Katibu Mkuu (Bara), Zitto Kabwe (wa tatu kushoto), Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Hamad Mussa Yussuf (wa kwanza kushoto) na Mkuu wa Masuala ya Sheria wa chama hicho, Tundu Lissu (kulia), ukiwasili kwenye ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam jana, tayari kwa mkutano wa kwanza wa makundi maalum na Tume ya Kukusanya Maoni kuhusu Katiba mpya.
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Chama cha Wananchi (CUF) vimewasilisha maoni kwa tume ya Mabadiliko ya Katiba vikitaka madaraka ya Rais yadhibitiwe pamoja na kutaka Muungano wa serikali tatu.
MAPENDEKEZO YA CHADEMA
Chadema jana kiliwasilisha mapendekezo kadhaa kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba; mojawapo kikitaka kuwapo kwa mfumo wa shirikisho wa serikali tatu kwenye Katiba Mpya.
Katika mfumo huo, Chadema kinataka kuwapo kwa Serikali ya Tanganyika na Zanzibar, ambazo kila moja itakuwa na mamlaka kamili ya Rais, Bunge na Mahakama, na kuwapo pia kwa Serikali Ndogo ya Muungano.
Mwenyekiti wa Sekretarieti ya Chadema iliyokutana na Tume hiyo jana, Tundu Lissu, alisema katika mapendekezo waliyoyawasilisha kwa Tume, wanataka Rais wa Serikali ya Muungano achaguliwe na wabunge wa Bunge la Tanganyika.
Pia achaguliwe na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, magavana, mameya na wenyeviti wa halmashauri za wilaya.
Lissu, ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki na Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari nje ya ukumbi wa Karimjee, jijini Dar es Salaam, muda mfupi baada ya sekretarieti yake kukutana na Tume hiyo jana.
Wajumbe wengine waliounda sekretarieti hiyo, ni Freeman Mbowe (Mwenyekiti wa Chadema na Mbunge wa Hai); Zitto Kabwe (Naibu Katibu Mkuu Chadema Tanzania Bara na Mbunge wa Kigoma Kaskazini) na John Mnyika (Mkurugenzi wa Habari na Uenezi Chadema na Mbunge wa Ubungo).
Wengine ni Said Issa Mohammed (Makamu Mwenyekiti Chadema Zanzibar); Hamad Mussa Yussuf (Naibu Katibu Mkuu Chadema Zanzibar); John Mrema (Mkurugenzi wa Halmashauri na Masuala ya Bunge Chadema) na Profesa Kulikoyela Kahigi (Mbunge wa Bukombe).
Lissu alisema katika mapendekezo yao, wanataka kuwapo kwa pande mbili za Muungano haki ya kujitoa kwenye Muungano kwa sharti kwamba, wanaotaka hivyo, wapige kura ya maoni.
Alisema pia wanataka yabaki mambo saba pekee, ikiwamo linalohusu ulinzi na usalama katika Serikali ya Muungano.
Lissu alisema wanataka Rais wa Muungano akae madarakani kwa miaka mitano ingawa anaweza kuongezewa muda, lakini kuwapo na utaratibu wa kupeana zamu za urais kati ya Tanganyika na Zanzibar.
Alisema Rais huyo pia ndiye atakayekuwa na mamlaka ya kutangaza vita, lakini ataruhusiwa kufanya hivyo baada ya kupata kibali cha Bunge na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar.
Katika mapendekezo yao mengine, alisema wanataka kinga ya mashtaka ya jinai dhidi ya Rais iondolewe, na pia kuwapo na udhibiti mkubwa wa mamlaka ya Rais.
Alisema wanataka kila atakayeteuliwa na Rais lazima aombe kazi husika kwenye tume huru za kitaalamu na athibitishwe na Bunge.
Lissu alisema pia wanataka serikali iwe na wizara zisizozidi 18 na zisizopungua 15 na pia Bunge liwe na wabunge 250 na liwapo Bunge la majimbo litakalokuwa na wabunge 50.
Pia alisema katika mapendekezo yao, wanataka kila raia aliyetimiza umri wa miaka 18 awe na haki kuchagua na kuchaguliwa, na kwamba, lile sharti la awali la kutaka anayetaka kugombea urais lazima atimize miaka 40, wanataka lisiwepo.
Alisema pia kuwapo na utaratibu wa kila raia mwenye haki ya kupiga kura apige kura awe ndani au nje ya nchi, au awe huru au amedhibitiwa na vyombo vya dola.
Lissu alisema pia wanataka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) isiteuliwe na Rais kama ilivyo sasa, badala yake wanataka iwe tume huru yenye wajumbe 25.
Alisema katika wajumbe wa tume, 15 wapendekezwe na vyama vyenye uwakilishi katika Bunge na kwamba, wajumbe wengine wa NEC watoke kwenye chama cha mawakili wa Tanganyika, taaluma, taasisi zisizokuwa za kiserikali, vyama siasa, visivyokuwa na uwakilishi bungeni.
Lissu alisema wajumbe hao wakipatikana, watatakiwa kupelekwa bungeni kuthibitishwa na Bunge na kwamba, Mwenyekiti na Makamu wake wa NEC watateuliwa na wajumbe wa tume.
Kuhusu umilikaji wa rasilimali, alisema wanataka Katiba Mpya itamke kwamba, maliasili ni mali ya wananchi na kwamba, kama wananchi hawatatoa ridhaa isichukuliwe.
Pia alisema pia wanataka malipo ya mrahaba yapelekwe kwenye maeneo yaliko madini ili wananchi wanaoishi katika maeneo hayo wapate asilimia 40 walipe kodi na asilimia 60 ibaki serikalini.
Alisema katika mfumo wa utawala, wamependekeza utaratibu wa kuwapo kwa mikoa na wilaya uliorithiwa kutoka kwa wakoloni uondolewe, kwa madai kwamba, mikoa na wilaya zimetengwa kwa misingi ya kabila.
Lissu alisema badala ya mfumo huo, kuwapo na mfumo wa majimbo yasiyopungua 10, ambayo alisema yataondoa ukabila.
Alisema katika mapendekezo yao, badala ya mkoa, wanataka kuwapo Jimbo la Nyanza Magharibi litakalohusisha mikoa ya Kagera, Geita na Shinyanga.
Jimbo lingine alisema liwe la Nyanza Mashariki, ambalo litahusisha mikoa ya Mara, Mwanza na Simiyu; Jimbo la Ziwa Tanganyika (Kigoma, Katavi na Rukwa); Jimbo la Kati (Tabora, Dodoma na Singida); Jimbo la Kaskazini (Kilimanjaro, Arusha na Manyara) na Jimbo la Pwani Kaskazini (Tanga, sehemu ya Pwani na sehemu ya Morogoro).
Jimbo lingine, alisema ni la Mji Mkuu wa Dar es Salaam; Jimbo la Pwani Kusini (Mtwara, Lindi, Mafia, Rufiji na Ulanga) na Jimbo la Nyanda za Juu Kusini (Njombe, Mbeya na Ruvuma).
“Ukigawanya nchi namna hiyo, hakuna jimbo litakuwa na rasilimali zake,” alisema Lissu.
Alisema pia wamependekeza kwenye mfumo wa utawala, kusiwapo mtu atakayeshawishi kwa Rais ili ateuliwe.
Pia wamependekeza miji iongozwe na mameya wa kuchaguliwa na kwamba, Katiba Mpya itamke kwamba, Kiswahili ni lugha ya taifa na kitumike katika shughuli zote za kiserikali, na pia miswada na sheria zote viandikwe kwa Kiswahili.
MAPENDEKEZO YA CUF
Nacho CUF kimependekeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania apunguziwe madaraka ya kuteua Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na kwamba kufanya hiyo kutaiwezesha kutekeleza majukumu yake bila kuingiliwa na mtu yoyote.
CUF kimependekeza kuwa mwenyekiti wa NEC pamoja na wajumbe wake wachaguliwe na vyama vya siasa pamoja na Asasi za Kiraia kwa niaba ya wanachi, na sio Rais kuteua mtu yoyote.
Kadhalika, chama hicho kimependekeza kuundwa kwa serikali tatu na kila moja iwe na Katiba yake ili kuondokana na malalamiko ya Muungano yaliyodumu kwa muda mrefu hapa nchini.
Pia CUF kimetaka mkataba uliounda muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar utafutwe popote ulipo ili wananchi wapate fursa ya kuujadili.
Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba muda mfupi baada ya chama chake kuwasilisha maoni yao kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Profesa Lipumba alisema chama chake jana kiliwasilisha maoni yao kama walivyofanya wananchi wengine.
“Hili jambo la Tanganyika na Zanzibara kuwa nchi moja halikubaliki kwa sababu kunapotokea kuzungumzia matatizo ya muungano uwakilishi hautoshi,” alisema Profesa Lipumba
“Mapatano ya muungano yalikuwa kwamba kila serikali itakuwa na mamlaka kamil, lakini mambo yasiyo ya muungano na yale ya muungano yaliwekwa chini ya serikali ya Tanganyika,” alisema Profesa Lipumba
Mapendekezo mengine yaliyotolewa na CUF kwa tume hiyo ni pamoja na Katiba kutambua mgombea binafsi kwa kuanzia ngazi ya Diwani, Mbunge na Rais.
Aidha, CUF kilipendekeza kwamba ushindi wa kiti cha urais uanzie asilimia 50 na kwamba mgombea akipata kura chini ya asilimia hizo uchaguzi urudiwe asitangazwe kama mshindi.
Profesa Lipumba kwa niaba ya CUF alisema, wamependekeza kwa tume kusiwepo na uchaguzi mdogo endapo kutatokea tatizo lolote kwa mgombea aliyeshika nafasi hiyo kutenguliwa au kupoteza maisha badala yake nafasi hiyo ichukuliwe na mgombea aliyeshika nafasi ya pili.
Mapendekezo mengine waliyotolewa na CUF ni pamoja na kutaka haki za binadamu kuingizwa katika Katiba pamoja na raslimali za nchi zitambuliwe na kugawanywa kwa usawa.
Alisema wamependekeza kwamba vyama vya siasa viruhusiwe kuungana na kusimamisha mgombea mmoja pamoja watendaji wa ngazi mbalimbali wasiteuliwe na Rais na kushika madaraka mpaka Bunge liwathibitishe.
CUF kilitaja baadhi ya nafasi ambazo Bunge linatakiwa kuzithibitisha kuwa ni pamoja na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama (CDF), Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na, Majaji.
Waliokiwakilisha CUF ni Profesa Lipumba; Naibu Katibu Mkuu Bara, Julius Mtatiro; Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Hamad Masoud Hamad; Mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi wa, Mbarala Maharagande; Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana wa CUF (Juvica), Katani Ahmed Katani na baadhi ya wabunge wa Viti maaalum.
CCM YAONDOA MAPENDEKEZO YA AWALI
Nacho Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambacho jana kiliwakilishwa na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, na mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombale-Mwiru, kuwasilisha maoni yake, kiliondoa waraka wake wa maoni kiliouwasilisha awali na kuwasilisha mwingine kwa Tume.
Naibu Katibu wa Tume hiyo, Casmir Kyuki, alithibitisha CCM kuchukua hatua hiyo katika mkutano kati ya Tume na wajumbe hao wa chama hicho, uliofanyika katika ukumbi wa Karimjee jana.
Hata hivyo, Kyuki alikataa kueleza maoni ya CCM yaliyokuwamo kwenye nyaraka hizo kwa maelezo kwamba, hawezi kufanya hivyo.
Chenge alipoulizwa na waandishi wa habari baada ya kukutana na Tume hiyo, alithibitisha kuwasilisha kwa Tume maoni ya CCM yenye mambo matano, lakini akakataa kuyaweka bayana.
“Tumewasilisha. Watakayoona yanafaa watayachukua na wasiyoona yanafaa watayaweka pembeni,” alisema Chenge.
Kuhusu mgombea binfasi, Chenge alisema CCM inapenda iwasikilize wananchi wanataka nini na kusisitiza kuwa suala hilo liachwe kwa Watanzania wenyewe waamue.
TUME YAZUIA WAANDISHI
Katika hatua nyingine, mikutano kati ya Tume na ujumbe wa vyama hivyo, jana vilifanyika kwa siri tofauti na utaratibu uliokuwa ukitumiwa na Tume hiyo awali wa kuendesha mikutano ya kukusanya maoni ya mwananchi mmoja mmoja kwa njia ya wazi.
Hatua hiyo, ambayo ilizua maswali na manung’uniko lukuki, ilikwenda sambamba na waandishi wa habari kuzuiwa kuingia katika kumbi, ambazo mikutano hiyo ilikofanyikia.
Waandishi kutoka vyombo mbalimbali vya habari walifika katika maeneo, ambayo mikutano hiyo ilikofanyikia, ikiwamo makao makuu ya Tume na kwenye kumbi za jengo la Karimjee, jijini Dar es Salaam mapema jana asubuhi.
Lakini kinyume cha kawaida, wakashindwa kupata moja kwa moja kilichokuwa kikiendelea katika mikutano hiyo, baada ya kukumbana na kisiki kutoka kwa maofisa wa Tume.
Maofisa hao waliwazuia waandishi wa habari kuingia ndani ya kumbi, ambazo mikutano hiyo ilikofanyikia, kwa madai kwamba, wamepewa maelekezo hayo na viongozi wao.
Kitendo hicho, ambacho kilishutumiwa na wengi, kiliwafanya waandishi wa habari kulazimika kusubiri nje ya kumbi hizo kupata kutoka kwa viongozi wa vyama vya siasa kilichojiri kwenye mikutano yao na Tume.
Lissu alihoji siri iliyokuwapo katika mikutano hiyo hata waandishi wa habari wazuiwe.
“Tume ina siri gani? Kulikuwa na siri gani ya kupindua serikali iliyokuwa inazungumzwa mle? (akionyesha ukumbi uliotumika kufanyia mkutano wao na Tume),” alihoji Lissu.
Chenge alipotakiwa kutoa maoni yake kuhusiana na kitendo hicho, alisema, huo ni utaratibu wa Tume, hivyo akashauri iulizwe.
Naye Kingunge alisema: “Ni mpango wa Tume, utauweza wapi? Tutaweza kupanga mambo ya Tume?”.
Alipoulizwa haoni kama kitendo hicho kinawanyima haki wanaCCM kujua kilichojiri katika mkutano kati yao na Tume, Kingunge alisema: “WanaCCM wanajua chama kinataka nini.”
Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Joseph Warioba, alipoulizwa jana, tofauti na Naibu Katibu wa Tume, alisema walishindwa kuwaruhusu waandishi wa habari kuhudhuria mikutano hiyo jana kutokana na kumbi za mikutano kuwa finyu.
Hata hivyo, Naibu Katibu wa Tume hiyo, Kyuka, akizungumza na waandishi wa habari katika viwanja vya Karimjee jana, alisema ni utaratibu wa Tume kwamba, wanapokutana na makundi, yakiwamo yanayohusisha vyama vya siasa, hawafanyi mikutano ya wazi.
“Na hawa waliitwa na Tume kwa ajili ya kupata ufafanuzi wa baadhi ya mambo. Utaratibu wake unatoa fursa kwa wajumbe wa Tume kuuliza maswali, kwani kuna baadhi ya mambo, ambayo wamekutana nayo wananchi waliyoyasemea,” alisema Kyuki.
Alisema awali, walipanga wasikutane na makundi hayo, kwa kuwa walitarajia kuwa wangekutana nayo katika mikutano waliyoifanya na wananchi mmoja mmoja, lakini wakaona kuwa uamuzi huo ungewafanya wakose kupata maoni muhimu, hivyo wakaamua kukutana nao.
Kyuki alisema hawaamini kama kuwazuia waandishi wa habari kuhudhuria mikutano hiyo kunwanyima haki wafuasi wa vyama hivyo kupata maoni yanayowasilishwa na vyama vyao kwa Tume kwa kuwa vyama hivyo tayari vimekwishatoa misimamo yao siku nyingi kabla ya jana.
“Lakini sasa hivi ni hatua, ambayo tulitoa mialiko. Ipo tofauti kati ya mikutano ya wananchi na makundi,” alisema Kyuki.
Alisema utaratibu wa kuendesha mikutano hiyo kwa siri, utaendelea kwa makundi yote mengine yaliyosalia, kama vile jumuiya kubwa na ndogondogo za kidini, asasi za kiraia, sekta binafsi, makundi maalum (vyama vya wafugaji na wavuvi nakadhalika).

CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment