BEKI wa kushoto Ashley Cole ameafikiana mkataba mpya na klabu yake ya Chelsea.
Wakati dili hilo bado halijasainiwa rasmi, taratibu zinatarajiwa kukamilika mwanzo ni mwa wiki hii, huku ripoti zikidai kwamba ameongezwa mwaka mmoja.
Taarifa hizo zinahitimisha utata uliotawala kuhusu hatma ya nyota huyo mwenye umri wa miaka 32. Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu.
Licha ya kuelekea ukingoni mwa maisha yake ya soka, Cole bado anachukuliwa kama mmoja wa mabeki bora wa kushoto duniani.
Beki huyo alikuwa akitarajiwa kwa kiasi kikubwa kuondoka Stamford Bridge. Muda mfupi baada ya kuchukua madaraka ya kuiongoza Chelsea, kocha Rafa Benitez aliulizwa kama anadhani kwamba Cole na Frank Lampard (34) wataondoka klabuni hapo mikataba yao itakapomalizika. "Nadhani hivyo, nadhani iko hivyo kwa sasa," alijibu.
Na klabu ya PSG, ambayo kocha wake Carlo Ancelotti, alimfundisha Cole enzi akiwa Chelsea, amekuwa akihusishwa kwa kiasi kikubwa na mchezaji huyo Muingereza.
Cole amecheza mechi 99 za timu ya taifa ya England na amekuwa katika kikosi cha kwanza cha Chelsea tangu alipotua Stamford Bridge akitokea Arsenal mwaka 2006.
Tangu uhamisho huo ulioonekana wa utata, Cole ameshinda ubingwa mmoja wa Ligi Kuu ya England, makombe manne ya FA, moja la Ligi na Mei mwaka jana alibeba kombe lake la kwanza la Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.
No comments:
Post a Comment