Afisa Habari wa TFF, Boniface Wambura
Hatimaye kambi ya timu ya taifa (Taifa Stars) imeanza kunoga baada ya kuripoti kwa washambuliaji Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu waliokuwa wakihangaikia ruhusa kutoka kwa klabu yao ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.Samatta na Ulimwengu waliwasili katika kambi ya Stars jijini Dar es Salaam juzi usiku na kuungana na wenzao kujiandaa na mechi ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya Ethiopia inayotarajiwa kuchezwa mwishoni mwa wiki.
Awali, Samatta na Ulimwengu walikuwa shakani kujiunga na Stars kutokana na taarifa kwamba walikuwa hawajaruhusiwa na timu yao kutokana na ukweli kuwa mechi za kirafiki zinazoikabili Stars hazimo katika kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
Hata hivyo, jitihada za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) katika kuishawishi Mazembe kupitia ujumbe uliopelekwa Kongo na Mkurugebnzi wa Ufundi wa shirikisho hilo, Sunday Kayuni, ulizaa matunda na sasa nyota hao wako katika kambi ya Stars, chini ya kocha Kim Poulsen.
Akizungumza na NIPASHE jana, Afisa Habari wa TFF, Boniface Wambura, alisema wamefurahi kuona kuwa sasa wachezaji hao wameungana na wenzao katika kambi ya Stars ili kulitumikia taifa lao.
"Suala la Ulimwengu na Samatta limekwisha na sasa wameripoti kambini na kuungana na wenzao," alisema Wambura.
Akieleza zaidi, Wambura alisema vilevile kuwa wachezaji wengine kutoka katika klabu za Simba na Azam zinazoshiriki mashindano ya Kombe la Mapinduzi mjini Zanzibar pia wanatarajia kuripoti wakati wowote kuanzia leo baada ya kuruhusiwa na timu zao.
Baadhi ya wachezaji wa Simba na wengine nane wa Azam wanaoshiriki Kombe la Mapinduzi, Zanzibar ni Juma Kaseja, Shomari Kapombe, Mwinyi Kazimoto, Mrisho Ngassa, Masoud Nassoro ‘Chollo’, John Bocco ‘Adebayor’, Salum Aboubakar ‘Sure boy’, Mwadini Ali, Erasto Nyoni na Aggrey Morris.
Mechi dhidi ya Ethiopia na nyingine za kirafiki watakazocheza Stars ni sehemu ya maandalizi yao kabla ya kuivaa Morocco mwezi Machi katika mechi yao ya hatua ya makundi ya kuwania kufuzu kwa fainali zijazo za Kombe la Dunia zitakazofanyika Brazil.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment