Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza na wanasoka wa Jimbo la Kiembesamaki alipokuna nao katika viwanja vya Mbweni Stars, Mbweni Zanzibar.
Wanasoka wa Jimbo la Kiembesamaki wakimsikiliza Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad alipokuna nao katika viwanja vya Mbweni Stars, Mbweni Zanzibar.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akisalimiana na wanasoka wa Jimbo la Kiembesamaki alipokuna nao katika viwanja vya Mbweni Stars, Mbweni Zanzibar.
ZANZIBAR 17/01/2013.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amezipiga tafu timu nne za jimbo la Kiembesamaki Wilaya ya Magharibi Unguja kwa kuzipatia fedha taslimu shilingi 750,000 pamoja na kuahidi vifaa vya michezo kwa timu hizo.
Akizungumza na wachezaji wa timu hizo katika uwanja wa Mbweni Stars inayoongoza ligi daraja la pili Wilaya ya Magharibi Unguja, Maalim Seif amesema atashirikiana na wananchi na wanamichezo wa Mbweni ili kuimarisha ujirani mwema.
Amesema fedha hizo zitatumika kwa ajili ya taratibu za uhamisho na usajili wa wachezaji watano watakaojiunga na timu ya Mbweni Stars ili kuongeza nguvu ya timu hiyo katika msimu ujao.
Timu nyengine zitakanufaika na vifaa vikiwemo jezi na mipira ni pamoja na timu ya Mbweni Kids, Mbweni Academy na Herbron zote za jimbo la Kiembesamaki.
“Nikiwa mkaazi wa Mbweni nitashirikiana na wananchi wote wakiwemo wanamichezo wa Mbweni ili kuhakikisha kuwa tunapiga hatua katika eneo letu”, alieleza Maalim Seif.
Amefahamisha kuwa azma ya serikali ni kuendeleza michezo nchini, na kwamba itaendelea kushirikiana na wanamichezo ili kutimiza azma hiyo.
Aidha ameitaka timu ya Mbweni Stars kuandaa utaratibu wa kuwasiliana na Baraza la mji ili kupata idhini ya kujenga uzio katika uwanja huo sambamba na kutoa agizo la kufanywa tathmini ya ujenzi huo ili aweze kuingiza mchango wake.
Mapema Katibu wa Timu ya Mbweni Stars Amir Makame alisema timu yao inakabiliwa na matatizo kadhaa yakiwemo upungufu wa wachezaji, motisha kwa wachezaji, vifaa vya michezo pamoja na ubovu wa uwanja unaotokana na kuwepo njia za kupita magari.
Ameitaja changamoto nyengine kuwa ni kutokuwepo kwa kocha wa kuinoa timu hiyo licha ya kushikilia nafasi ya kwanza ya ligi daraja la pili katika Wilaya ya Magharibi.
Nae Mwenyekiti wa timu hiyo Suleiman Haroub amempongeza Maalim Seif kwa kuonyesha mwelekeo mwema wa kushirikiana nao katika kuendeleza soka na vipaji vya vijana wa jimbo hilo.
Amesema iwapo vijana watashirikishwa kikamilifu katika michezo wataweza kujiepusha na vitendo viovu vikiwemo wizi na utumiaji wa dawa za kulevya.
No comments:
Post a Comment