Bw. Miraji Mrisho Kikwete.
Shirikisho la Ngumi la Kimataifa Africa (IBF/Africa) limemteua bwana Miraji Mrisho Kikwete kuwa Makamu wa Rais anayeshughulikia maendeleo ya vijana katika bara la Afrika, Ghuba ya Uajemi na Mashariki ya Kati. Uteuzi wa Miraji unaanza January mwaka mpya 2013.
Katika kumteua Miraji, Rais wa IBF katika bara la Afrika, Ghuba ya Uajemi na Mashariki ya Kati bwana Onesmo Ngowi alisema kuwa Miraji ana uwezo wa kuwahamasisha na kuwaunganisha vijana katika shughuli za maendeleo.
Aliendelea kusema kuwa Miraji atakuwa anawahamashisha vijana, kuwaunganisha, kuwajengea uwezo wa kimaendeleo yatakayoratibiwa na IBF.
Aidha, Rais huyo alisema kuwa Miraji atakuwa anabuni njia mbalimbali za kuwaunganisha vijana wa Afrika, Ghuba ya Uajemi na Mashariki ya Kati ili waweze kufaidika na miradi ya IBF ambayo inalenga kwenye elimu, kujenga vipaji pamoja na kuwaunganisha kwenye biashara ya utalii wa michezo.
Katika mkutano wake wa mwaka uliofanyika katika jiji la Honolulu, jimbo la Hawaii, nchini Marekani hivi karibuni IBF iliupokea mradi wa “Utalii wa Michezo” uliobuniwa na kuwakilisshwa na Rais wa IBF katika bara la Afrika, Ghuba ya Uajemi na Mashariki ya Kati Mtazania Onesmo Ngowi.
Lengo kuu la mradi huu ni kulifanya bara la Afrika hususan Tanzania kuwa kitovu kikuu cha “Utalii Michezo” hivyo kujenga uchumi imara. Nchi za Tanzania na Ghana ziliteuliwa kuwa nchi za mfano kwenye mradi huu.
Katika mradi huu, IBF itatumia mtandao walionao katika nchi zaidi ya 203 duniani kuhamasisha wanachama wake na famlia zao, wapenzi pamoja na marafiki zao kuja Afrika/Tanzania kutalii pamoja na kuwekeza katika miradi mbalimbali.
Uteuzi wa Miraji utasaidia kuwaunganisha vijana ili waweze kuchangia na kufaidika na biashara ya utalii kwenye mradi huu umefanywa wakati muafaka.
Miraji ambaye ni Mjasiliamali amejipambanua katika maendeleo ya jamii na ana mchango mkubwa sana katika kuendeleza vijana nchini Tanzania.
Rais Ngowi alimwelezea Miraji kama tegemeo ambalo vijana wanalihitaji kwani wanahitaji uhamasishaji wa hali ya juu na Miraji ana uwezo wa kufanya kazi hiyo kwa ufanisi mkubwa kwani alishawahi kuifanya kwa kipindi kitefu.
Miraji Mrisho Kikwete ni msomi wa chuo kikuu cha nchini Oman ambako amesomea elimu ya utawala wa biashara ambayo ndiyo lengo kuu la uteuzi wake. Ana haiba ya kupendwa na vijana pamoja na uwezo wa kujichanganya nao.
No comments:
Post a Comment