ANGALIA LIVE NEWS

Monday, January 7, 2013

Polisi wawili wanaswa na meno ya tembo

Askari wawili wa Jeshi la Polisi mkoani  Kagera, wametiwa mbaroni kwa tuhuma za kukutwa wakiwa na meno ya tembo katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti mkoani Mara.

Mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Taifa (Tanapa), Allan Kijazi, aliliambi NIPASHE jana kuwa askari hao walikamatwa juzi jioni na askari wa Hifadhi ya Serengeti kwa kushirikiana na Polisi wa Kituo cha Mugumu.


Alisema askari hao walifanikiwa kuwakamata askari wenzao wakati wakipeleleza kuhusu matukio ya wizi wa nyara za serikali na hivyo wakuwakuta wakiwa na vipande vya meno ya tembo ambavyo vikiunganishwa yanafikia meno mazima sita.

Alisema watuhumiwa hao walikuwa wakisafirisha meno hayo ya tembo kutoka kijiji cha Bunchugu wilayani Serengeti kwenda mjini Mugumu kwa kutumia pikipiki mbili.

Hata hivyo, Kijazi alisema polisi na askari wa wanyamapori wamemkamata mmoja wa watu waliokuwa wakiendesha pikipiki na mwingine aliyekuwa amebeba mzigo huo lakini mwingine akimbia.

Alisema watuhumiwa hao baada ya kukamatwa waliwapeleka askari kwa matajiri waliokuwa wakipelekea mzigo huo katika hoteli moja ya mjini Mugumu.

Kijazi alisema matajiri hao pia wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa mahojiano zaidi pamoja na gari lao dogo.

Alisema baada ya kuhojiwa, wamegundulika kuwa ni askari polisi mmoja mwenye cheo cha Koplo na mwingine Konsitebo kutoka Biharamulo mkoani Kagera.


Alisema waliwasiliana na Mkuu wa Polisi katika eneo walikotoka na kuthibitisha kuwa ni askari wake lakini alishtushwa kukutwa kwa askari hao Serengeti mkoani Mara.

Alisema katika simu zao, zilionyesha walikuwa wakiwasiliana na watu walioko kwenye mtandao  mkubwa wa ujangili wa meno ya tembo.

“Huu mtandao ni mkubwa sana sana na wazi sasa imebainika hata yule faru aliyepokelewa na Rais Kikwete, ndiyo waliohusiku kumuuaa kwa ajili ya kuchukua nyara zake…hii ni hatari kwa wenzetu polisi kushiriki  kufanya hujuma kwa taifa lao,” alisema Kijazi.

Alisema baada ya mahojiano yanayofanyika Kituo Kikuu cha Mugumu wilayani Serengeti, taarifa kamili ya watuhumiwa hao zitatolewa.

“Tunaomba ushirikiano na wananchi ili kuhakikisha kuwa tunalinda rasilimali zetu…kwani bila ushirikiano kamwe hatuwezi kufanikiwa,” alisema Kijazi.

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Said Mwema, alithibitisha kukamatwa kwa askari hao.

IGP Mwema alisema hatua hiyo imetokana na ushirikiano mzuri kati ya askari polisi na watumishi wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (Senapa).

Akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu jana, IGP Mwema alisema ingawa kitendo hicho kimelifedhehesha Jeshi la Polisi, lakini kamwe jeshi hilo halitakata tamaa kwa kuwaondoa kazini askari wake wanaokwenda kinyume cha maadili.

“Jeshi la Polisi tumekuwa na ushirikiano mzuri na wenzetu wa Tanapa hata kukamatwa kwa askari hawa wawili, kumetokana na ushirikiano uliopo kati ya Polisi Mugumu na watumishi wa Hifadhi ya Serengeti,” alisema IGP Mwema.

Alisema Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Tanapa limekuwa likiendesha mazoezi mbalimbali ya kupambana na ujangili katika maeneo mbalimbali nchini hivyo kamwe haliwezi kurudi nyuma kwa utovu wa nidhamu ambao umeonyeshwa na askari hao.

“Ndani ya Jeshi, tuna progaram ya kutoa zawadi kwa kila askari wanaofanya vizuri katika kupambana na uhalifu pia kwa wale wanaokwenda kinyume, tumekuwa tukiwachukulia hatua ikiwa ni pamoja na kuwafukuza kazi,” alisema.

Aliongeza: “Mpango wa kutii sheria bila shuruti, pia unawalenga askari, hivyo nakuhakikishia kuwa lazima tutalisafisha Jeshi letu la Polisi kama kuna askari anajijua hawezi kwenda na kasi hii ya sasa, ni vema akajiondoa mwenyewe.”

Hata havyo,  ameomba wananchi kutoa ushirikiano wa kutosha katika kupambana na vitendo vya uhalifu katika maeneo yao na ujangili kwenye hifadhi za taifa.

Kuhusu mauaji ya kikatili yanayoendelea mkoani Mara, IGP Mwema alisema tayari Jeshi la Polisi limetuma timu maalum ya kuendesha operesheni maalum ambayo itahakikisha inakomesha unyama huo.

“Tulituma timu ya kwanza ya kukusanya taarifa sasa tumetuma timu kubwa ya kufanya operesheni kubwa na ya aina yake ili kuhakikisha kila aliyehusika anakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria... lakini pia ni vyema wananchi wakatoa ushirikiano wakati wa kazi hiyo kubwa na vikundi vya ulinzi pia vifanye kazi yake,” alisema.

TRAFIKI WABANWA WAREJESHE FEDHA

ZAIDI ya abiria 30 waliokuwa wakisafiri na basi Eicher kutoka Masasi kwenda Tandahimba mkoani Mtwara, walilazimika kuvunja ukimya na kuteremka kutoka ndani ya gari hilo na kuwataka askari wa Usalama Barabarani wilaya ya Newala warejeshe fedha walizozichukuwa kutoka kwa kondakta wa basi hilo.

Tukio hilo ambalo lilishuhudiwa na mwandishi wa habari hizi, lilitokea eneo la nyumba ya kulala wageni ya Country Lorge iliyopo mjini Newala Januari Mosi, mwaka huu, saa 8:45 mchana.

Basi hilo lenye namba za usajili T 641 BJX likiendeshwa na dereva aliyefahamika kwa jina moja la Remmy kutoka Masasi kwenda Tandahimba, lilisimamishwa na askari hao akiwamo mmoja wa kike (Namba na jina la askari huyo kwa sasa limehifadhiwa).

Aidha, baada ya askari huyo kulisimamisha, alipanda ndani ya basi hilo na kuteremka kisha akaenda kando ya barabara alikokuwa amesimama askari mwenzake wa kiume.

Akia hapo, askari huyo alichukua kitabu chake na kumuandikia kondakta faini (notification) ya Sh. 30,000 kwa kosa  la kutokuwa kwa kisanduku cha huduma ya kwanza katika basi hilo.

Waandishi waliokuwa wakisafiri na basi hilo kutoka wilayani Masasi kwenda Tandahimba, waliiona `notification' hiyo aliyoandikiwa kondakta wa basi hilo yenye namba A: 0344140 ya Januari 01, mwaka huu, iliyosainiwa na askari huyo wa kike.

Baada ya askari huyo kumuandikia faini hiyo, kondakta wa basi hilo aliyefahamika kwa jina la moja la Mnandi, alitoa fedha hizo na  kumkabidhi askari huyo ambaye naye alichana `notification' kutoka kwenye kitabu hicho na kumkabidhi kondakta.

Lakini kondakta alirejea kwenye basi bila ya kupewa risiti kutokana na fedha alizozitoa.

Kitendo cha kondakta huyo kurejea bila ya kupewa risiti ya malipo aliyotoa kilishuhudiwa na abiria na kumtaka arejee kwa askari hao ili wampatie risiti yake.

“Hebu tujulishe mbona unarudi bila ya risiti wakati fedha za faini umeshalipa? Rudi wakakupatie risiti na kama hawana wakurudishie fedha ukalipie ofisini kwao vinginevyo hatuondiki hapa,” alisikika mmoja wa abiria hao akisema kwa jazba.

Kondakta aliporejea kwa askari wale, alipewa lugha ya vitisho kwa kuambiwa iwapo anahitaji risiti au kurejeshewa kwa fedha hizo watahakikisha wanakula naye sahani moja.

“We konda unawasikiliza hao abiria, wewe hii ni njia yako unafikiri watakusaidia mpaka lini hao?,” alisikika askari huyo wa kike akisema.

Kauli ya askari huyo iliwafanya abiria hao kupandwa na hasira na kuteremka kutoka kwenye basi na kuwafuata mahali walipokuwa wamesimama kutaka wafahamu sababu zinazowafanya wasitoe risiti huku fedha wamezichukuwa kutoka kwa kondakta.

Hata hivyo, askari hao walijitetea kwamba kitabu cha risiti kimekwisha.

“Kwa vile mnasema kitabu cha risiti kimekwisha na huyu mmeshamuandikia notification, fedha mlizozichukua hakuna sababu ya kuendelea kubaki mikononi mwenu. Zirudisheni aende akalipe ofisini kwenu,” alisema abiria mwingine.

Wakati askari hao wakiendelea kutafakari nini cha kufanya, baadhi ya abiria waliwaeleza wasipotoa risiti au kurejesha fedha hizo, hawatakuwa tayari kuendelea na safari yao huku wakisisitiza wapo tayari kumpigia simu Mkuu wa Polisi nchini (IGP), Saidi Mwema, kumuelezea matatizo yanayofanywa na askari hao.

Hata hivyo, matamshi ya abiria hao pamoja na askari kusuasua kutekeleza yale waliyotakiwa, ndipo dereva Remmy, alipochukua uwamuzi wa kuwaomba abiria hao waendelee na safari yao.

Lakini ombi la dereva huyo lilidumu kwa takriban dakika tano na kupokewa na abiria wake kwa shingo upande.

 
CHANZO: NIPASHE

No comments: