ANGALIA LIVE NEWS

Monday, January 7, 2013

SAJUKI, WASTARA KATIKA MAANA HALISI YA MAPENZI, TUJIFUNZE

KUNA msemo wa kweli wenye maana kubwa kwamba kipindi cha matatizo ndipo unapoweza kumjua rafiki wa kweli. Hata hivyo, ipo mifano ya marafiki waliowafaa wenzao wakiwa na matatizo lakini baadaye wakawasaliti.
Anakufaa kwa dhiki lakini baadaye anakutenda, ingawa picha iliyozoeleka ni kwamba anayesaidiwa ndiyo baadaye hugeuka mnyama. Ni mambo ya ulimwengu kwa walimwengu. Mtu mwema hapimwi kwa kipimo kimoja.
Penzi la kweli ni zaidi ya mifano ya rafiki akufaaye wakati wa dhiki. Kadhalika halipimwi kwa kuangalia utulivu wa wahusika. Ukasema fulani na fulani wanapendana kwa dhati, kutokana na namna ambavyo wanaishi bila migogoro.
Mapenzi ya kweli yana tafsiri ya ndani zaidi. Maneno kwa shida na raha yana maana zaidi ya namna yanavyochukuliwa. Yupo aliyemhifadhi mume wakati aliposimamishwa kazi lakini akawa anatoka nje ya ndoa. Kipimo cha mapenzi hakirandani na matukio ya tamthiliya.
Usiseme wewe na mpenzi wako mnapendana kwa dhati kisa huwa anakupeleka ufukweni, klabu na maeneo mengine ya kustarehe. Ukayapima kwa kigezo kuwa hajifichi kuwa nawe ndiyo maana anaongozana nawe sehemu mbalimbali. Ukiyachukulia hivyo utafeli.
Asije akatokea mtu akajidanganya kwamba yeye na mwenzi wake wanapendana kwa dhati kisa huwa hawawekeani uzio katika simu zao za mkononi. Kwamba kila mmoja yupo huru kushika ya mwenzake, kupokea na kusoma SMS, vilevile kuangalia historia ya simu na SMS zilizoingia na kutoka.
Penzi la kweli lipo ndani ya moyo. Linaweza kudhihirika kwa nje pale wahusika wanapopatwa na mitihani mikubwa. Namna wanavyozikabili changamoto na kuzivuka pamoja ndipo ukweli au unafiki wao katika mapenzi hudhihirika. Huwezi kuigiza au kujilazimisha kupenda, ipo siku utaumbuka.
Kuna walioshikamana sana wakati wa raha, wakiugua wanauguzana lakini pale mirija ya fedha ilipokata, yule aliyekuwa anajifanya anapenda, aliyekesha hospitali akimuuguza mwenzi wake mpaka akasifiwa na kupewa pongezi za kila aina, alibadilika, akawa mnyama ndani ya nyumba.
Inawezekana kwa mwanamke kumuuguza mume wake mwenye uwezo mkubwa kifedha, akimnyenyekea na kumpa huduma bora zaidi. Kumbe hafanyi hayo kwa mapenzi, bali anajionesha kwa ndugu wa mume. Shida yake ni zile mali, akipona waendelee kutumbua, akifa arithi.
Mume au mke kafungwa jela, hapo mapenzi ya kweli hudhihirika. Je, mwenzi wake anaendelea kuwa naye, akimtia moyo kwamba atamaliza kifungo? Kama ndivyo, angalia na maisha yake halisi, je, habadili wapenzi kwa kutumia kigezo kuwa mwenzake hayupo?
Mpenzi wa kweli hawezi kumuacha mwenzake anapopatwa na matatizo, atahakikisha anakuwa faraja yake. Atakwenda gerezani kumsalimia na kumuonesha namna walivyo pamoja. Ukiwa na penzi la kweli, huwezi kupata hisia za mapenzi na mtu mwingine, wakati umpendaye yupo matatizoni.
Buriani Juma Kilowoko ‘Sajuki’. Yeye na mke wake, Wastara Juma, wamenipa sababu ya kuandika makala haya. Nimekuwa nikisimamia darasa la mifano ndiyo maana siwezi kuacha kuliacha hili lipite. Mapenzi ya Sajuki na Wastara ni kitabu kizito chenye mafundisho ya namna wapenzi wanavyopaswa kuishi.
Usidhani namna walivyoweza kushuka kwenye mabonde na kupanda milima ni rahisi, wengi yamewashinda. Wastara na Sajuki ni watu bora zaidi wa mfano katika kizazi cha sasa.
Chukua mfano mmoja tu, kuna mrembo maarufu nchini anaitwa Jacqueline Patrick, mume wake, Abdulatif Fundikira yupo mahabusu (siyo mfungwa) lakini huku nyuma yalishaonekana madudu mengi. Jack ameshindwa kumfariji mume wake mbele ya mtihani mdogo mno ambao huwezi kuulinganisha na wa Sajuki.
Itaendelea wiki ijayo.

www.globalpublishers.info

No comments: