ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, January 22, 2013

waliokataa sensa wameitia hasara serikali

Na Salma Said, Zanzibar

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imesema kitendo cha baadhi ya wananchi kususia sensa kilisababisha serikali kuingia gharama kubwa katika kuendelea kuhamasisha umma kukubali zoezi hilo kwa maendeleo ya Taifa

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha Uchumi na Mipango ya Maendeleo Zanzibar, Omar Yusuf Mzee ameyasema hayo alipokuwa akijibu suala la msingi katika ukumbi wa baraza la wawakilishi linaloendelea huko Chukwani nje kidogo ya Mji wa Zanziba lililoulizwa na mwakilishi wa Kiwani (CUF) Hija Hasan Hija .

Hija aliyetaka kujua ni kiasi gani serikali imepata hasa na imejifunza nini kutokana na mamuzi wa wananchi, je ni sheria gani iliyovunjwa na wananchi na je sheria hiyo ilipitishwa au kuridhiwa na baraza la wawakilishi.
Aidha Hija alitaka kujua iwapo sheria ipo na inafanya kazi ni kwa nini vyombo va Dola vikaaamua kuwapiga na kuwasumbua wananchi badala ya sheria kuchukua mkondo wake wakati wa zoezi la sensa lililofanyika mwishoni mwa mwaka jana.

Waziri alisema hasa pale serikali ilipoongeza wiki moja zaidi kwa ajili ya kuendelea na kazi ya kuhesabu watu sio rahisi kupata tathmini ya fedha zilizotumika kughaamia kazi za ziada zilizofanywa na makundi ya watu mbali mbali walihamasisha na kuelimisha watu washiriki katika zoezi la sensa ya watu na makazi baada ya kugomea kuhesabiwa kwa wiki ya kwanza.

Alisema sheria iliyovunjwa ni sheria ya takwimu ya Zanzibar Namba 9 ya mwaka 2007 sehemu ya tano kifungu cha 14 (2) na (3) na sheria hii ilipitishwa na Baraza la wawakilishi

Mzee alisema serikali haina taarifa kuwa wananchi waliosusia sensa walipigwa na kusumbuliwa na vyombo vya dola na hakuna mwananchi aliyewasilisha madai ya aina hii katika chombo chochote cha kisheria hapa Zanzibar kinyume chake ni baadhi ya wananchi waliosusia zoezi hilo ndio waliofanya fujo.

“Serikali haina taarifa ya kuwa kuna watu waliyanyaswa kuhusu suala la sensa lakini tunajua kuwa maafisa wa sensa ndio walionyanyaswa, kupingwa na kuharibiwa mali ya serikali ilipokuwa ikifanya hiyo kazi” alisema Waziri.

Waliwapiga na kuwatukana makasaa wa sensa kuwanyananya maafisa vifaa vyao vyakufnayia kazi ni wananchi ambao hawakuwa wakitaka kuhojiwa kuhusiana na zoezi hilo la sensa ambapo mbali ya kuhatarisha usalama wa maafisa hao lakini pia wamehatarisha usalama wa wananchi wenzao katika maeneo ya makaazi yao.

Alisema muda wote huo serikali ilichukua busara na hekma kubwa na ilijiepusha na vitendo va kutumia nguvu na iliunda timu ya viongozi wa dini na watu mashuhui kwa leno la kuwaelimisha zaidi wananchi badala ya kuwachukulia hatua.

Naye Mwakilishi wa Jimbo la Chonga Abdallah Juma Abdallah (CUF) alisema sensa imeshindwa kufanikiwa kutokana na tabia ya masheha kukataa kuwatambua wananchi katika maeneo yao wakati wa uchaguzi na ndio wananchi wamejenga uadui kati yao na masheha.

“Mheshimiwa Spika Masheha wamekuwa na tabia ya kukataa kuwatambua wananchi wa maeneo yao katika shehia zao hata kama wanawajua lakini ikifika wakati wa uchaguzi wanasema hawawatambui jee serikali haioni kwamba kittendo cha Masheha ndio kilichochangia wananchi kukataa kutoa ushirikiano kwa Masheha wakilipiza kutotambuliwa kwako na Masheha?” alihoji Abdallah.

Waziri akijibu hilo alisema inawezekana ikawa suala hilo ni kweli lakini akasisitiza ushirikiano mzuri kwa kati ya wananchi na masheha ni serikali kuendelea kutoa elimu kwa wananchi na masheha ambao wamekuwa hawataki kutoa ushirikiano kwa wananchi ili wananchi waweze kuelewana na masheha kwani bila ya mshirikiano hakuna kazi ya maendeleo itakayofanikiwa.

No comments: