Kichupa cha ‘In The Congo’
Mimi kama Mtanzania, na mpenzi wa muziki wa Hip Hop, nafurahi kuona Waafrika wengine wakijiunga katika kutuhabarisha juu ya vita hii, kwa kupitia nguvu ya kinasa na mashairi ya Hip Hop. Ujumbe ni rahisi, hauchochei watu kugoma kutumia vifaa hivi vya elektroniki, lakini kuwa makini, kwa kununua vile ambavyo havichochei maafa zaidi na ambavyo vinakuza haki katika biashara. Hii itasaidia kuokoa maisha ya Wakongo wengi. Ni matarajio kuwa ujumbe umefika, na hivyo kutusukuma mimi na wewe kuchukua hatua. Hii ni muhimu, hasa tukizingatia Afrika ndio soko linalokuwa kwa kasi ya vifaa kama simu za mikononi, ambazo ndio zinatengenezwa na madini hayo ya coltan kutoka Kongo
Ndugu Zavara, mmoja wa waanzilishi wa Bongo Hip Hop na waasisi wa kundi la Kwanza Unit, anagusia vita ya Kongo katika ‘In The Congo‘ kwa mtindo wa kipekee kwenye kichupa hiki adhimu.
Pamoja na wimbo huu kugusia vita mas-ala ya maafa ya vita Kongo, halkadhalika kuhomola (kwiba kwa “Kitemeke”) utajiri wa madini ya huko kwa ndugu yetu wa Msasani, bwana Josefu Kabila.
Zavara kwa umakini bila kupitiliza amefanikiwa kuinakshi mandhari ya kichupa, kwa muundo tofauti kabisa na hivi vya siku zote hapa Bongo. Madini husika, yanayoendeleza ukatili angamizi wa Mfalme Leopold ni madini ya coltan, yanayotumika kutengezea vifaa vyetu vya elektroniki. Hata hivyo, vita ya Kongo inasababishwa na mwingiliano wa mambo mengi, kutokana na utajiri wake wa madini na historia ya nchi hiyo.
Nyimbo inashirikisha wasanii wa kike, kama mwanaharakati na mahiri sana wa mitindohuru toka jiji la Tofaa Bovu (New York), Toni Blackman (aliyepewa wadhifa wa balozi wa US Hip Hop), akishirikiana na kundi lake la Rhyme Like A Girl, pamoja na mwanadada mzaliwa wa jiji la Malkia Bi’ Khalifa (siku hizi Kalifonia) mwenye asili ya Kenya, Nasambu. Huu upangaji katika ushirikishwaji una umuhimu. Bado sijui kama Zavara alidhamiria kushirikisha wasanii wa kike tu, au ilitokea bila kukusudia. Hii ina umuhimu wake, hasa ukizingatia maafa ya Kongo pamoja na kuendelea kuuawa kwa halaiki ya watu, ubakaji uliokithiri umeacha wanawake wengi na makovu. Hivyo, kuona muungano wa sauti za akina dada katika ‘In The Congo’ inatia imani na faraja kuwa kuna wanaojali.
Mpangilio wa washirikishwaji katika ‘In The Congo’ unaweza kutazamwa kama kichaka cha saruji (New York) ukutanapo na misitu ya Kongo, wanapopigana wanajeshi na waasi. Vita hii inaendeshwa na ulevi wetu wa vifaa vipya vya elektroniki, kama simu za mikononi, kompyuta za kupakata na kadhalika, huku Wakongo wakijikuta wamebanwa katikati ya risasi za wanajeshi na waasi wanao faidika na mauzo ya madini hayo ya coltan. Wakongo wengi wanaweza kutojua madini hayo yanatumiwa kwenye nini hasa, lakini wanajua fika jinsi gani vita hii inayosukumwa na mauzo ya madini hayo inavyoendelea kuathiri maisha yao.
No comments:
Post a Comment