ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, July 21, 2013

Kilio kwa makamanda waliokufa Darfur

Askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) wakiwa wamebeba jeneza moja kati ya saba ya miili ya askari wa Tanzania waliokuwa katika jeshi la kulinda amani la Umoja wa Mataifa (Unamid) baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Jeshi (Airwing) Dar es Salaam jana.Picha na Fidelis Felix
Dar es Salaam. Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal jana aliwaongoza mamia ya waombolezaji kupokea miili saba ya wanajeshi wa Tanzania waliouawa Darfur, Sudan, Julai 13, mwaka huu.
Miili ya wanajeshi hao saba iliyowasili jana ni SajIni Shaibu Sheha Othman, Koplo Osward Paulo Chaula, Koplo Mohamed Juma Ally, Koplo Mohamed Chukilizo, Private Rodney Ndunguru, Private Peter Werema na Private Fortunatus Msofe.
Wanajeshi hao walikuwa sehemu ya Jeshi la Kulinda Amani la Umoja wa Mataifa (Unamid), kusini mwa Darfur na walitoka katika vikosi vya, 42KJ Chabruma, Songea, 44KJ Mbeya, 36KJ Msangani, 92KJ Ngerengere, 94KJ cha Mwenge, Dar es Salaam, 41KJ Nachingwea na Makao Makuu ya JWTZ- Upanga, Dar es Salaam.
Imeelezwa kuwa wanajeshi hao waliuawa na kikundi cha waasi cha Janjaweed kinachoungwa mkono na serikali ya Sudan, huku wengine 19 wakijeruhiwa kutokana na kile kilichoelezwa kuwa walikuwa wakifuatilia magari yao yaliyokuwa yametekwa na kundi hilo.
Hali ilivyokuwa
Baada ya miili hiyo kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Jeshi saa 10:40 jioni na ndege ya Antlantis iliyotolewa na Umoja wa Mataifa(UN), mamia ya watu waliokuwapo uwanjani hapo walionekana kuingiwa na huzuni baada ya kuona miili ya marafiki, ndugu na jamaa zao ikishushwa kwenye ndege hiyo.
Baada ya ndege hiyo kuwasili, viongozi wakuu wa Serikali pamoja na wambolezaji wengine waliisogelea ndege hiyo kwa ajili ya kupokea miili ya wanajeshi hao.
Miili hiyo ilishushwa na kuingizwa kwenye magari saba ya jeshi, na kupelekwa katika Hospitali ya Jeshi la Lugalo kwa ajili ya kuhifadhiwa.
Wanajeshi hao wanatarajiwa kuagwa kesho Jumatatu katika viwanja vya Makao Makuu ya Jeshi Upanga, baadaye miili hiyo itasafirishwa kwenda kuzikwa katika maeneo yaliyotengwa na familia zao.
Waombolezaji
Baadhi ya ndugu wa marehemu waliofika kwenye viwanja hivyo walisema kuwa walikuwa wakiwategemea sana ndugu zao.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti walisema mara baada ya kupata taarifa za vifo hivyo, walishtuka na kutoamini kilichotokea huku wakieleza kuwa walikuwa wanawasiliana nao mara kwa mara wakati wakiwa Darfur.
“Tuliwasiliana na baba (Koplo Mohamed Chukilizo wa kikosi cha 41KJ, Majimaji, Nachingwea), siku chache kabla ya kifo chake, aliniambia anarudi hivi karibuni na kunitaka niendelee vizuri na masomo,” alisema Amina mtoto wa marehemu Chukilizo.
Aliongeza, “Baada ya wiki mmoja tulipewa taarifa za kifo chake, jambo hili lilitustua sana na hatukuamini kabisa.”
Amina ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha nne, Shule ya Sekondari Nachingwea alisema mpaka sasa hajui hatima yake katika elimu kwa sababu alikuwa akimtegemea baba yake kwa kila kitu.
Binti huyo aliyekuwa ameongozana na mama yake, hawakuwa na ndugu yeyote wa familia ya baba yake waliomsindikiza.
Chukilizo atazikwa mkoani Kigoma mara baada ya kukamilika kwa taratibu za mazishi.
Naye Msemaji wa familia wa marehemu, Sajini Shaibu Othman kutoka Makao Makuu ya Jeshi Upanga (MMJ) jijini Dar es Salaam, Mohamed Sadiki alisema kuwa marehemu ameacha mjane na watoto watatu.
Alisema baada ya kupata taarifa hizo, walishtuka na kutoamini kilichotokea.
“Tumeshtushwa sana na tukio hilo, hatukuamini kabisa kwa sababu tulikuwa tukimtegemea kwa kiasi kikubwa, na ameacha mama yake mzazi, mjane na watoto watatu,”alisema Sadiki.
Aliongeza, marehemu alikuwa anaishi Kigamboni, kwamba atazikwa Zanzibar kwa maelezo kuwa ndiko familia ilikopendekeza kumzika.
Naye mke wa marehemu, Oswald Chaula kutoka kikosi 42KJ Chabruma, Songea, Maria Chaula alisema kuwa baada ya kupata taarifa hizo walipatwa na mshangao na walikusanyika nyumbani kwa marehemu kwa ajili ya kupanga taratibu za mazishi.
“Nilipopata taarifa za msiba huu wa mume wangu nilihisi kuchanganyikiwa. Mume wangu tegemeo langu niliomba arudi salama ili tuweze kupanga maisha yetu, lakini Mungu amempenda zaidi,” alisema kwa uchungu Maria.
Hata hivyo, waombolezaji wengine walishindwa kuongeza chochote katika eneo hilo, huku wakionekana kulia wakati wote tangu walipofika kwenye eneo la uwanja huo hadi miili ya wapiganaji hao ilipowasili.
Hata hivyo, Kaimu Msemaji Mkuu wa JWTZ, Meja Joseph Masanja alisema kuwa, miili ya wapiganaji hao imehifadhiwa katika hospitali ya jeshi kwa ajili ya kusubiri utaratibu wa kuagwa ifikapo Jumatatu ili iweze kusafirishwa vijijini kwao.
“Ratiba iliyopo ni kupokea miili ya marehemu na kwenda kuihifadhi katika Hospitali ya Jeshi Lugalo, na ifikapo Jumatatu majira ya saa 2:30 asubuhi itapelekwa kwenye viwanja vya Makao Makuu ya Jeshi kwa ajili ya kuaga,”alisema Meja Masanja.
Dk Bilal aliongozana na mke wa Rais, Salma Kikwete, Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Idd, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, Mkuu wa Majeshi, Davis Mwamunyange na Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP)Said Mwema.
Mwananchi

No comments: