Na Flora Wingia.
Wiki hii nakuja na kisa kingine alichonitumia msomaji wetu mzuri. Ni kisa kinachomhusu yeye mwenyewe bila kupepesa macho, anaanza namna hii;
“Anti Flora, naomba uniambie kwa uzoefu wako katika makala yako hii una muda mrefu, Je, kati ya wake na waume ni nani huanza kusaliti mahusiano zaidi. Baada ya hii nina kisa kingine nitakujuza.”
Msomaji wangu hilo ni swali kauliza msomaji wetu huyu. Hebu andaa majibu yake tuyajadili wiki ijayo. Wakati tunasubiri, amenijuza kisa kingine pengine kikilenga swali lake hapo juu. Hebu tumsikilize, kisha wiki ijayo tuwe na majibu hapa.
Naam. Anaanza hivi; Anti samahani nitazidi kukusumbua. Yote haya nataka kujifunza kwani nilijikwaa nikaanguka! Sasa sitaki kuangalia nilipoangukia nataka kuangalia nilipojikwaa! Kwa hiyo usichoke kunipa ushauri; nilikwambia siku chache zijazo nategemea kuoa!
Nikakwambia napata woga kutokana na vitimbi vingi vya ndoa. Ulinipa ushauri mzuri mno nimeupenda na ninaufanyia kazi; sasa nina kisa kinachonihusu mimi, je, utanisaidiaje?
Kijana huyu anasema hivi;“Mke alinitoroka nikiwa mgonjwa. Kwa kifupi nilimuoa nikapata naye mtoto. Tukaja Dar kutafuta unafuu wa maisha. Nikawa Napata vibarua vya hapa na pale ilimradi tunaishi. Siku moja akaniomba naye akatafute kazi za ndani kwa Wahindi.
“Akatoa sababu kwa kuwa kipato ninachopata hakitoshi na kuwapa msaada wazazi wake wanaomtegemea. Nikaona sawa nikamwambia mshahara wake utumike kwa ajili hiyo na mimi nitalipa kodi ya nyumba, kula na mahitaji mengine.
“Maisha yakaendelea sasa akawa na pesa nazo jeuri zikaanza. Ananiambia mhindi wake anaumwa anampeleka Bagamoyo na kulala huko huko. Siku nyingine anadai analala na mgonjwa Aga Khan hospitali na sababu mbalimbali ili mradi alale huko. “Ilifikia hatua anti naumwa ndani hathubutu hata kwenda kunitafutia panadol. Natoka mwenyewe usiku wa saa tano mpaka Magomeni pale kichangani kwenye maduka ya dawa, yeye kalala wala hashtuki.
“Nakumbuka anti kuna siku amepasha maji ya moto akachanganya na unga akaniwekea ninywe, sikuweza. Kuna siku nimekwenda kwenye kibarua nikazidiwa na homa nikalazwa kwa mapumziko asubuhi muda wa saa akanipigia simu mdogo wake kwamba dada yake kabeba vitu vyote kahamisha.
“Nikaomba ruhusa hospitali nikaenda kukuta chumba cheupeee! Nikaendelea na vipimo nikagundulika nina matezi kwenye mapafu nikaanza matibabu kwa miezi sita. Namshukuru Mungu nikamaliza salama. Ninachoshukuru sikuwa na maambukizi, ninaendelea na kazi zangu. “Nimeanza ujenzi wa nyumba yangu. Amesikia najenga ameanza kunisumbua, ananipigia simu anataka tuonane tuyamalize na kunitumia sms za kuomba nimsamehe. Na talaka nilishamtumia. Sasa hivi nina mchumba nipo katika hatua za mwisho, siku si nyingi tutaoana. Je, nini ushauri wako anti Flora? Pia hili ni somo kwangu,” anamaliza ujumbe wake msomaji wetu huyu.
Mpenzi msomaji, ni ujumbe mrefu kidogo lakini uliojaa tafakari nyingi zenye machungu ambazo yafaa sote tuzijadili na mwishowe kupata ufumbuzi wa kudumu. Hatupaswi kuishi kwenye maisha yenye mitihani ya aina hii pasipo kupata majawabu.
Kijana huyu baada ya kupitia kwa undani kisa chake, nilimwambia kuwa kama hivyo ndicho kilichotokea, Mungu ni mwema sana kwani lipo jambo alilomwepusha na mwanamama huyo. Inaonyesha kabisa kuwa mkewe huyo wakati wakiwa pamoja hakuwa anamjali.
Kati ya hawa wawili, aliyesaliti mahusiano ni mwanamke huyo. Mume alionyesha busara kwa kumruhusu atafute kazi. Lakini baada ya kuipata jeuri ikaanza. Mume akakubali hata pale alipojulishwa kuwa hatarudi nyumbani kwani anasafiri na bosi wake Mhindi na kulala huko huko. Hiyo haikumsumbua mumewe.
Kilichodhihirisha wazi kuwa mwanamke huyo hakuwa anampenda mumewe ni pale alipougua na japokuwa mkewe yupo lakini hakuonyesha kumhudumia ipasavyo. Huu ni ukatili mwingine alioonyesha mama huyo.
Na ukatili mwingine mbaya zaidi, ni pale mumewe alipolazwa hospitalini, huku nyuma mwanamke akafungasha virago na kuondoa pasipo kuaga. Siyo ajabu aliona amefanikiwa kimaisha na kwamba mumewe huyo ataabika maishani.
Kumbe akasahau kuwa hata kama umeanguka, ukamuomba Mwenyezi Mungu, mkono wake uliojaa utukufu utakuinua tena. Na wale waliokudharau na kukutesa, atawaonyesha ushindi kwa kukuinua tena kimaisha na kudhihirisha hilo mbele za maadui zako.
Naam. Hilo limetendekea juu ya msomaji wetu huyu. Angalia mwanamke alimtesa, akamnywesha uji mbichi, akamkimbia kwa kuchukua vitu vyote ndani na kutokomea huku akimwacha taabani hospitalini.
Angali mkono wa Mungu ukamuokoa, ukamponya na sasa amepata mchumba na ameanza kujenga nyumba yake. Ndipo mwanamama yule anajipitisha pitisha ati anaomba msamaha na kutaka waonane yaishe. Hivi mama huyu alitegemea kweli kumuona hai mumewe huyu wa zamani? Na kama alishapewa talaka, nini anahangaika tena?
Katika ushauri wangu nilimwambia kijana huyu maadam mama yule alihama na vitu vyote na kumwacha taabani, na maadam alishamtaliki, na sasa anaye liwazo la roho anayetaka kumuoa karibuni, ajipange upya kwa maisha mapya kwani Mungu ndiye aliyemwepusha na yote hayo. Maisha Ndivyo Yalivyo.
No comments:
Post a Comment