Hatua hiyo inatokana na uamuzi wa Mahakama wa kuamuru miili ya watoto wake watatu iliyohamishiwa Mvezo, ifukuliwe na kwenda kuzikwa tena Qunu
Pretoria. Vita ya wapi atakapozikwa Rais wa kwanza mzalendo wa Afrika Kusini, Mzee Nelson Mandela imefikia tamati na sasa ni rasmi kwamba atazikwa Qunu uamuzi ambao umeacha ufa na uhasama mkubwa katika familia ya kiongozi huyo.
Jana, mabaki ya miili ya watoto watatu wa Mandela ambao ni marehemu ilitarajiwa kuzikwa upya katika eneo la Qunu, yakiwa ni mazishi ya mara ya tatu tangu walipofariki dunia katika vipindi tofauti, ukiwa ni utekelezaji wa amri ya Mahakama Kuu ya Eastern Cape.
Uamuzi huo ulimaanisha kushindwa kwa mjukuu wa Mandela, Mandla ambaye jana katika mkutano wake na waandishi wa habari alisema: “Sikusudii kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa Mahakama,” lakini akahusisha ugomvi katika familia ya babu yake kwamba ni vita ya fedha na mali za Mandela.
Mabaki hayo ni ya mtoto wa kwanza wa kiume wa kiongozi huyo, Makgato aliyefariki dunia 2005, binti yake wa kwanza Makaziwe (mkubwa) ambaye alifariki akiwa mchanga mwaka 1948 na mtoto wake wa pili wa kiume, Madiba Thembekile aliyefariki katika ajali ya gari 1969.
Mahakama Kuu ya Eastern Cape ilitoa uamuzi uliowapa ushindi wanafamilia 16 wa Mandela ambao walifungua madai wakiongozwa na shangazi yake Mandla, Makaziwe.
Jaji Lusindiso Pakade katika hukumu yake, mbali na kutoa amri hiyo alitaja vitendo vya Mandla kuwa ni vya aibu visivyo vya kibinadamu hivyo kutoa amri ya kufukuliwa miili hiyo na kisha kurejeshwa Qunu. Mabaki hayo yalihamishwa kutoka kijiji cha Mvezo ambako yalizikwa mara ya pili kwa kificho miaka miwili iliyopita na mjukuu mkubwa wa Mandela, Mandla ambaye pia ni kiongozi wa kimila katika kijiji hicho.
Kazi ya kufukua makaburi ya watoto wa Mandela katika eneo la Mvezo ilifanyika hadi juzi usiku chini ya ulinzi wa polisi baada ya madalali wa mahakama kutumia sururu kuvunja lango (geti) kuu la kuingia katika makazi ya Mandla.
Kwa mujibu wa msemaji wa polisi wa eneo hilo, Luteni Kanali Mzukisi Fatyela, uchimbuaji wa makaburi ulifanywa na wataalamu wa Kituo cha Afya cha Mthatha na baadaye kupelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha kituo hicho juzi usiku na jana asubuhi mabaki ya marehemu hao yalifanyiwa uchunguzi wa kimaabara kabla ya kupelekwa Qunu kwa maziko.
Madaraka au fedha?
Makaziwe (60) ambaye ni binti mkubwa wa Mandela na wenzake 15 kutoka katika familia hiyo, walifungua madai wakitaka kurejeshwa kwa mabaki ya miili hiyo Qunu wakisema Mandla aliyahamisha bila makubaliano ya familia. Mandla katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika Mvezo jana alisema ugomvi uliopo ni wa kimasilahi na kwamba familia inawania fedha za babu yake.
Alisema chimbuko la kuandamwa linatokana na msimamo wake wa kukataa kuondolewa katika bodi ya ya mfuko wa Mandela baadhi ya watu wakiwamo Wakili George Bizos na Waziri wa Makazi Tokyo Sexwale. “Sasa wameamua kunilenga mimi kama mlengwa dhaifu.”
Kabla ya familia kuamua kufungua kesi Juni 28, mwaka huu kiliitishwa kikao cha familia na Mandla alihojiwa na kutakiwa arejeshe mabaki ya miili hiyo Qunu lakini hakukubali na badala yake alitoka na kuacha kikao kikiendelea, hatua ambayo ilitafsiriwa kuwa ni kudharau familia hiyo.
Mvutano baina ya Mandla na shangazi yake Makaziwe anayewaongoza wanafamilia wengine unatafsiriwa na baadhi ya watu kwamba ni vita ya kuwania madaraka na fedha ikiwa Mzee Mandela atafariki dunia. Juzi, Msemaji Mkuu wa chama tawala cha ANC, Jackson Mthembu alisema chama hicho hakiwezi kuingilia masuala ya familia hiyo na kwamba kinaamini wana uwezo wa kuyamaliza... “Tunasikitishwa na hali hiyo, inaweza kuharibu sifa ya Mandela ndani na nje ya nchi, lakini tunaamini kwamba familia ina uwezo wa kuyamaliza.” Inaaminika kuwa Mandela mara kadhaa alisema akifa angependa azikwe Qunu ambako kuna makaburi ya familia yakiwamo ya watoto wake, hivyo Mandla aliyahamishia Mvezo ikiwa ni hatua ya kushawishi babu yake (Mandela) azikwe katika eneo hilo ambalo yeye ni kiongozi wake.
Uamuzi wa Mahakama una maana kwamba kaburi la Mandela litakapokuwa ni dhahiri ndipo makumbusho yake yatakapojengwa, hivyo kama atazikwa Qunu basi makumbusho hayo yatakuwa mikononi mwa familia yake na kama atazikwa Mvezo yatakuwa chini ya usimamizi wa Mandla ambaye ni dhahiri tayari amekosa nafasi hiyo.
Katika hati yake ya kiapo iliyowasilishwa mahakamani Mthatha, Mandla alidai kwamba anataka Mandela azikwe Mvezo kwani ndiko alikozaliwa na kwamba eneo hilo lina umuhimu wa kipekee katika historia ya babu yake.
Hivi sasa mjukuu huyo wa Mandela ambaye pia ni Mbunge wa Eastern Cape, ana hoteli kubwa ya kitalii yenye thamani ya mamilioni ya Dola za Marekani katika Kijiji cha Mvezo. Mwaka jana mmoja wa wanakijiji wa Mvezo alimfungulia mashtaka kwa tuhuma za kufukua makaburi kwa lengo la kujenga hoteli, lakini kesi hiyo hadi sasa haijasikilizwa.
Mgawanyiko wa familia
Ni dhahiri kwamba uamuzi wa juzi wa Mahakama umeiacha familia hiyo ya Mandela vipande kwani Mandla anakabiliwa na kesi nyingine mbili za jinai ambazo huenda zikafunguliwa siku chache zijazo katika Mahakama Kuu ya Western Cape baada ya uchunguzi wa kipolisi kukamilika.
Kesi hizo ni ile inayotokana na wanafamilia kutaka polisi wachunguze madai kwamba Mandla ‘alichezea’ makaburi hali ambayo inaweza kusababisha uharibifu wa mazingira kinyume cha sheria za Afrika Kusini na pili uchunguzi unaolenga kubaini iwapo taratibu za kisheria kwa maana ya afya zilifuatwa wakati wa uhamishaji wa mabaki ya marehemu hao miaka miwili iliyopita. Polisi kwa upande mmoja na kituo cha afya kwa upande mwingine katika eneo la Mthatha wamethibitisha kuanza kwa upelelezi huo dhidi ya Mandla na ikiwa wataridhika, watamfungulia mbunge huyo mashtaka ya jinai.
Mandla kwa upande wake jana aliweka bayana kuwa baadhi ya watu siyo wanafamilia wa Mandela akiwarushia vijembe shangazi zake kwa maelezo kuwa walishaolewa na kupoteza jina hilo kwani walikuwa wakitumia majina ya waume zao.
“Sasa inaonekana kwamba kila mtu anaweza kusema kwamba yeye ni Mandela kudai kuwa mwanafamilia ili kushiriki katika uamuzi wa kifamilia, wameamua kuzikimbia familia zao na kurukia katika ‘jahazi’ la Mandela.”
Afya ya Mandela
Mandela hivi sasa yu mahututi kwa siku ya 28 na amelazwa katika Hospitali ya Magonjwa ya Moyo, Medclinic iliyopo Pretoria akisumbuliwa na tatizo la figo kushindwa kufanya kazi na hali yake inaelezwa kuwa ni mbaya.
Kesi hiyo iliwezesha kufahamika kwa hali ya afya yake kwani kwa mara ya kwanza, ilithibitika kwamba anapumua kwa msaada wa mashine na hiyo ni kwa kujibu wa hati ya kiapo ya Makaziwe aliyoiwasilisha mahakamani katika kesi hiyo ambayo pia inasema: “Matarajio ya kifo chake yamejengwa kwenye msingi wa uhalisia.” Hati hiyo ya Juni 28, mwaka huu ambayo pia inawahusisha wanafamilia wengine akiwamo mke wa Mandela Graca Machel na mtalaka wa Mandela, Winnie inasema afya ya Mandela haitii matumaini huku ikiweka bayana kwamba hati ya kiapo ya daktari ingewasilishwa mahakamani kuthibitisha kwamba anasaidiwa na mashine kupumua.
Kadhalika, hati hiyo inathibitisha kwamba lengo la kesi hiyo ni kuhakikisha Mandela anazikwa katika eneo ambalo wanafamilia wengine wakiwamo watoto wake wa kuwazaa wamezikwa na kwamba wanafamilia wanaamini kwamba hatua ya kuhamishwa makaburi matatu kwenda Mvezo kulifanyika kwa masilahi ya kifedha.
Hata hivyo, Mandla katika kiapo chake mahakamani alipinga hoja kwamba Mandela yu mahututi na kwamba hata kama ni kweli suala hilo halina uhusiano na mahali atakapozikwa.
“Ugonjwa hauna uhusiano wowote na mahali atakapozikwa na hakuna maelekezo maalumu ya wasia ambayo yanasema Mandela anataka azikwe Qunu,” inasomeka sehemu ya kiapo cha Mandla.
Kwa mujibu wa sheria za Afrika Kusini zinazosimamia masuala ya mila na desturi, Mandla asingeweza kushinda kesi hiyo.
Gazeti la Mail & Guardian lilimnukuu Mtaalamu wa Sheria na Katiba nchini hapa Profesa Shadrack Gutto akisema kuwa sheria zinamtaka Mandla ambaye ni kiongozi wa kimila wa Mvezo, Eastern Cape kufuata taratibu kabla ya kuhamisha masalia hayo.
Profesa Gutto alisema ni dhahiri kwamba Mandla hakufuata sheria na taratibu hizo kwani akiwa kiongozi wa Mvezo, alipaswa kushauriana, kisha kukubaliana na kiongozi wa Qunu kabla ya kufanya alichokifanya.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment