ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, July 20, 2013

Wanawake ni waathirika wakubwa maeneo ya kazi

Dar es Salaam. Kwa miaka mitatu iliyopita, Rehema Nduguru (50) anayeishi Mkoa wa Njombe alikuwa katika mazingira hatarishi ya kupata magonjwa ya ngono ikiwamo Ukimwi kutokana na kazi yake ya uhudumu wa baa.
Akitoa maelezo yake jijini Dar es Salaam hivi karibuni, Rehema anasema kutokana na kazi hiyo alikuwa akilazimika kufanya ngono zembe ili kujiongezea kipato. Hata hivyo, anashukuru Mungu hakupata maambukizi ya Ukimwi.
“Wakati tukifanya kazi hiyo, mimi na wenzangu tulikuwa tukifanya ngono zembe, hasa na madereva wa magari ya mizigo yanayoegeshwa karibu na baa tulizokuwa tukifanyia kazi,” alisema Rehema.
Hata hivyo, Rehema sasa ameachana na kazi hiyo na amepata msaada kutoka Shirika la Kazi duniani (ILO).
“ILO walikuja Njombe na kutushauri tuunde vikundi ambapo tulipewa fedha zilizotuwezesha kufanya kazi zenye staha. Sasa ninauza nguo sokoni na ninapata fedha za kutosha kutokana na biashara hiyo. Tumeanzisha ushirika wa kuweka na kukopa (Saccos) ambayo inatuwezesha kujiendeleza kiuchumi,” anasema.
Kwa upande wake Mwajuma Sabuni anayefanya kazi katika kiwanda kimoja jijini Dar es Salaam (jina linahifadhiwa) analalamikia unyanyasaji wa kijinsia kutoka kwa waajiri wao.
“Nimefanya kazi katika kiwanda hiki kwa miaka saba sasa. Kwa miaka miwili ya awali nilifanya kazi kama kibarua, lakini baadaye nikaingizwa kwenye mkataba wa kazi na kuanza kukatwa mafao ya uzeeni na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), bila kupewa kadi ya uanachama na mwajiri wangu. Hadi sasa sijui hatima ya pensheni yangu,” anasema na kuongeza:
“Kwa jumla hali ya ajira katika kiwanda hiki ni ngumu hasa sisi wafanyakazi wa kike kwani rushwa ya ngono iko nje nje. Wasimamizi wa vitengo ndiyo wahusika na ukiwakataa ajira yako inakuwa hatarini. Licha ya kuwepo kwa Chama cha Wafanyakazi (Tuico) kinachojua kero zote hizi, bado hazijashughulikiwa. Naiomba Serikali iingilie katika kwa kuchunguza madai haya kwani tunanyanyasika mno.”
Maelezo ya wanawake hawa yanawakilisha kilio cha wafanyakazi wengi wanaonyanyaswa kijinsia kutokana na kazi zao. Wengi hulazimika kujiingiza kwenye ngono zisizo salama, hivyo kuhatarisha maisha yao hasa kwa kupata ugonjwa wa Ukimwi.
Katika mkutano wa wadau wa kupambana na ugonjwa wa Ukimwi, hasa maeneo ya kazi uliofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam, wadau wanasema kuwa wanawake na wasichana wako kwenye hatari zaidi ya kuathirika na ugonjwa huo na kwamba hatua stahiki zinapaswa kuchukuliwa ili kukabilia na tatizo hilo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids), Dk Fatma Mrisho anasema kuwa makundi ya wanawake walijitokeza kuomba msaada ili kujikwamua kimaisha na kujilinda.

“Hatari ya wanawake hawa kuathirika na Ukimwi ni kubwa mno. Ni changamoto kubwa inayohitaji jitihada za kila mmoja wetu,” anasema Dk Mrisho.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (Tucta), Hezron Kaaya anapendekeza mifuko ya hifadhi ya jamii kuanzisha mfuko wa kuwasaidia wanawake na wasichana wanaofanya kazi zenye hatari ya maambukizi ya magonjwa ya ngono ukiwamo Ukimwi.
Kwa upande wake Justina Lyela, Mkurugenzi wa Sera na Utetezi wa Chama cha Waajiri Tanzania(ATE) amewataka waajiri nchini kuepuka kuwapunja wafanyakazi wa kike ukilinganisha na wanaume ili kuwawezesha kiuchumi, hivyo kuwasaidia kuepuka maambukizi ya Ukimwi.
Katibu Mkuu, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Kijakazi Mtenga aliyemwakilisha Waziri Sophia Simba katika mkutano huo, ametaka kuwepo kwa usawa wa fursa kama vile elimu na rasilimali za uchumi hasa kwa wanawake ili kuepusha hatari ya maambukizi hayo.
Hali ya maambukizi
Wito wa wadau hao umekuja wakati kiwango cha maambukizi kikionyesha kuwa kikubwa zaidi kwa wanawake.
Ripoti ya Tacaids inaonyesha kuwa maambukizi kitaifa yamefikia asilimia 5.7 huku wanawake wakiwa na maambukizi ya asilimia 6.8 huku wanaume wakiwa na asilimia 4.7.
Sababu kubwa ya maambukizi inatajwa kuwa ni umaskini, kuhama, mila na desturi mbaya, mfano mimba za utotoni. Nyingine ni kutokuwa na usawa, ulevi wa kupindukia na matumizi ya dawa za kulevya.
Ripoti hiyo inapendekeza kuongeza kipato cha makundi yaliyo katika hatari ya maambukizi.
“Baadhi ya wanawake waliohojiwa wamebainisha kuwa hulazimika kurithiwa baada kufariki kwa waume zao ikiwa ni mila inayowataka kufanya hivyo ili kulinda mali za marehemu.
Wengine wamesema kuwa hulazimika kukubali kufanya mapenzi kwa kuogopa kufukuzwa au kukosa misaada kutoka kwa wanaume wenye uwezo. Wahudumu wa baa na wafanyakazi wa ndani wamekubali kufanya ngono ili kulinda kazi zao,” inasema sehemu ya ripoti hiyo.
Upimaji unaongezeka
Kwa upande mwingine utafiti uliofanywa na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Dawa za Binadamu (NIMR), mwaka 2008 unaonyesha kuwepo kwa ongezeko la watu wanaopima afya zao na kupata ushauri kuhusu ugonjwa wa Ukimwi.
“Katika nchi nyingi, mwamko wa kupima VVU kwa hiari umeongezeka kwa kasi kutokana na upanuzi wa tiba ya VVU. Katika Tanzania, uwiano wa idadi ya watu waliowahi kipima umeongezeka kutoka asilima 15 hadi 32 kati ya 2004 na 2007,” inaeleza sehemu ya utafiti huo na kuongeza:
“Hata hivyo, mwelekeo wa kupima VVU kwa watu walioambikizwa katika katika ngazi ya jamii unafahamika kwa kiwango kidogo sana. Hii ni kwa sababu ni watu wachache sana wanaojua hali zao za maamukizo ya VVU kabla ya Upimaji wa hiari na ushauri nasaha.”
Utafiti huo ulifanyika Kata ya Kisesa jijini Mwanza kwa lengo la kuelewa kiwango ushauri nasaha unavyovutia watu walioambukizwa VVU na kutoa taarifa muhimu kuanzisha mpango wa ‘matibabu kama kinga’.
Wito wa ILO
Kwa mujibu wa mapendekezo ya Shirika la Kazi Ulimwinguni (ILO) kuhusu VVU na Ukimwi katika maeneo ya kazi ya mwaka 2010, ugonjwa huo una athari kubwa katika jamii na uchumi katika sekta rasmi na isiyo rasmi, kwa wafanyakazi na wategemezi wao.
“Jukumu la ILO ni kuhamasisha kuhusu ugonjwa huo katika ulimwengu wa kazi na haja ya kuongezwa kwa juhudi za kujikinga na kupambana na ubaguzi na unyanyapaa kwa walioathirika,” inasema taarifa ya ILO.
Inasisitiza pia umuhimu wa kupunguza kazi zisizo rasmi kwa kuongeza zenye staha na maendeleo endelevu ili kufikia malengo ya ulimwengu wa kazi bora bila maambuki ya VVU na Ukimwi.
Mwananchi

No comments: