Dar es Salaam. Wanasayansi nchini Marekani wamesema kuwa wamegundua aina ya chanjo, ambayo mtu akipatiwa hataugua tena ugonjwa wa malaria maisha yake yote.
Ugunduzi huo ambao tayari umefanyiwa majaribio kwa watu kadhaa na kufanya kazi kikamilifu ukiwa pia salama, utaandika historia ya kufuta malaria na kuwa ugonjwa wa nadra kwa watu kuugua.
Taarifa kwa gazeti hili iliyotolewa Alhamisi wiki hii na Taasisi ya Marekani ya Kudhibiti Magonjwa ya Kuambukiza na Mzio (NIAID), inaeleza kuwa chanjo hiyo iliyopewa jina, PfSPZ imeonyesha mafanikio hayo kwenye hatua yake ya awali ya majaribio.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mtu akipatiwa chanjo hiyo mwili wake unatengeneza chembe kinga ambazo zinakuwa na uwezo wa kuangamiza vimelea wa malaria katika hatua yake ya mwanzo mara baada ya kuumwa na mbu.
Chanjo ya PfSPZ, inaelezewa kutengenezwa kwa vimelea dhaifu wa malaria ambao huhamasisha mwili kutengeneza askari wa kudumu.
Kumbukumbu za Shirika la Afya Duniani (WHO) za mwaka 2010, zinaonyesha kuwa zaidi ya watu 3.3 bilioni, ambao ni karibu sawa na nusu ya dunia nzima wapo kwenye hatari ya kuugua ugonjwa wa malaria.
Katika kipindi cha mwaka huo, inaripotiwa kuwa watu 210 milioni walibaini kuugua malaria, baada ya kupimwa hospitalini ambapo takriban 660,000 walipoteza maisha.
Asilimia 90 ya waliopoteza maisha walikuwa kutoka Bara la Afrika, licha ya juhudi kubwa za kusambaza vyandarua vyenye dawa na dawa za tiba.
WHO inasema kuwa kuongezeka kwa mbinu za kuzuia na kutibu malaria katika maeneo mbalimbali duniani kumesaidia kupunguza tatizo la malaria kwa asilimia 25 na kwa asilimia 33 katika Bara la Afrika.
Imesema kuwa nchi nyingi za Afrika zina uwezo mdogo wa kifedha, hivyo hutegemea mataifa tajiri kuzisaidia kwa kuwezesha kupatikana vifaa vya kuzuia malaria na dawa za tiba za bei nafuu, hata kutolewa bure kwa watoto na wajawazito.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment