ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, August 4, 2013

Fainali uwanjani

Tido Mhando

Tido Mhando aliifanya kazi ya utangazaji katika redio kwa muda mrefu sana, akianzia tangu chini akiwa na umri mdogo wa miaka 19, hadi kushika wadhifa wa juu kwenye sekta hiyo kama Mkurugenzi Mkuu. Sasa kwenye makala zake hizi za kila Jumapili, Tido anasimulia yale aliyokumbana nayo, aliyokutana au kukabiliana nayo katika kipindi cha zaidi ya miaka 40 ya utangazaji. Wiki jana alisimulia jinsi alivyofika nchini Uganda, kwenye enzi ya utawala wa Idi Amin kutangaza mashindano ya mpira wa miguu kwa nchi za Afrika ya Mashariki, ambapo Tanzania na Uganda zilifanikiwa kuingia fainali ya michuano hiyo. SASA ENDELEA…
Naam, baada ya mechi ile ya mwisho ya michuano ya awali ya makundi ambapo kwenye Kundi B Tanzania iliishinda Kenya kwa mabao 2 kwa 1 na hivyo kushika nafasi ya kwanza kwa kuwa na jumla ya point 6, ikawa bayana kuwa mahasimu hawa wawili wangekutana sasa ana kwa ana kwenye mechi ya fainali ya uwanja wa kandanda.
Hali hii iliongezea msisimko mkubwa michuano hii. Msisimko ambao labda haukuwa umetarajiwa mwanzoni. Uganda na Tanzania ambazo kidogo zingekuwa zichapane kwenye uwanja wa vita, kama si busara za kuzipatanisha, sasa zikawa zinakabiliana macho kwa macho kwenye mechi ya fainali ya kabumbu.
Sasa pakawa panafikia kilele cha sinema ya kusisimua. Msisimko ambao haukuwa umetanda nchini Uganda pekee bali pia Tanzania na labda pote Afrika ya Mashariki. Msisimko uliojaa mzizimo wa aina yake wa hofu fulani hivi, kwani tulikuwa nyumbani kwa mbabe Idi Amin Dada.
Tulirejea hotelini mwetu baada ya mechi ile ya Tanzania na Kenya tarehe 27 Septemba tukiwa na furaha kubwa, lakini mioyoni tukiwa tumeanza tena kujawa na woga juu ya nini kitatokea kwenye fainali hiyo ambayo hapana shaka yoyote, mgeni mheshimiwa angekuwa mwenyewe Rais wa Uganda.
Tulipoketi wenyewe kujadili mashindano hayo kama michuano halisi ya soka, tulijipa matumaini makubwa kwamba timu yetu ilikuwa na uwezo mkubwa tu wa kuigaragaza Uganda nyumbani kwao na kuitia aibu mbele ya mwamba wao huyo.
Lakini ni pale tulipokuwa tukijaribu kuitafsiri aibu hiyo ndipo miili yetu ilipozizima kwa woga; woga wa uwezekano wa kutokea lolote baya, hata pengine kudhuriwa maisha yetu ama yeyote miongoni mwa kundi kubwa la Watanzania waliokuwepo nchini Uganda wakati ule.
Tulikuwa tumekwishamwona Idi Amin pale uwanjani kwenye mechi za nyuma, akipita kifua mbele kwa maringo makubwa na mbwembwe za aina yake, akionyesha ya kwamba hakuna linalomshinda.
Huu ulikuwa ni mwaka 1973, tayari mbabe huyu alikuwa ameshakaa madarakani kwa zaidi ya mwaka. Alikuwa anafaidi madaraka, akifanya fujo na vitimbi vya aina yake ambavyo dunia ilikuwa ikivishuhudia.
Kama aliweza kuwalazimisha Waingereza, raia wa dola iliyotawala, siyo Uganda pekee, bali sehemu kubwa ya dunia, wambebe mabegani mwao, kwenye kiti cha Mfalme, huku akiwapungia watu mikono, ni kipi basi ambacho hangeweza kukitenda?
Kama alithubutu kuwatimua Wahindi wote waliokuwa wakiushikilia uchumi wa Uganda na kuwavurumushia huko nchini Uingereza, huku maduka yao na biashara zao nyingine zote akiwakabidhi kama njugu Waganda wenzake, basi asingeshindwa kufanya lolote ambalo labda angeliota usiku ule kuhusu mechi hiyo ya Uganda na Tanzania.
“Bila ya shaka hii ilikuwa nafasi yake mwafaka ya kuuonyesha ulimwengu kwamba yeye ndiye yeye,” Nilijiwazia mwenyewe, wakati nikiwa peke yangu ndani ya chumba changu hotelini.
Kwa maana hii, tulijikumbusha tahadhari kubwa tuliyolazimika kuichukua kuanzia wakati huo hadi siku yenyewe ya mchezo huo wa fainali, yaani Jumamosi, Septemba 29. Ilikuwa imebakia siku moja nzima. Tuliamka Ijumaa asubuhi ambapo magazeti yote ya Uganda yalikuwa yamepambwa na habari chungu nzima kuhusu pambano hilo lililokuwa likitarajiwa baina ya Taifa Stars na Uganda Cranes.
Zilikuwa ni habari za kimchezo tu zikitabiri na kudadisi kuhusu uwezo, nguvu na udhaifu wa timu zote mbili kama ulivyobainishwa kwenye mechi za hatua za awali. Lakini wengine wetu tulikuwa tukienda ndani zaidi na zaidi kuhusu pambano hilo.
Je, ni kweli jambo hili litaishia kwenye mshike mshike wa kiwanjani pekee ama litalipuka vinginevyo? Hakuna aliyekuwa akijua kwa wakati huo. Basi tuliamua kumuachia Mwenyezi Mungu pekee.
Hatukuwa na nafasi kubwa ya kusikia mengi kutoka kwa mashabiki wa Jiji la Kampala kuhusu kipute hicho kilichokuwa kikitarajiwa mbali ya kauli za majigambo na majivuno kutoka kwa wafanyakazi wa pale hotelini tulipokuwa tunaishi.
Nasema hatukuweza kuwasikia wengine kwani lazima nikubali kwamba katika siku zote tulizokuwepo ndani ya jiji hili la Kampala kwenye mashindano hayo, kamwe hatukutoka na kutembeatembea mitaani kutokana na wasiwasi tuliokuwa nao.
Hata hivyo, katika siku hiyo ya mapumziko, tulipata fursa ya kuchukuliwa na kutembezwa jijini na jamaa mmoja wa pale hotelini ambaye tulishajenga urafiki naye na kwa kiasi fulani tulimuamini, hasa kwa kuwa pia alikuwa ni rafiki wa karibu na mwandishi mwingine wa habari kutoka Kenya, Harry Were Silas ambaye baadaye naye aliishia kuwa rafiki yangu mkubwa.
Hata hivyo, hatukutaka kutembezwa mbali sana, tukamwomba atupitishe haraka haraka kwenye yale maeneo maarufu Jiji la Kampala, jiji la vilima vilima, lenye mambo mengi sana ya kihistoria.
Kwa hiyo, alituchukua na kutupeleka kutuonyesha Chuo Kikuu cha Makerere, Hospitali Kuu ya Mulago, eneo yalipokuwa makao makuu ya Kabaka wa Buganda na hata pia kwenye eneo la Makanisa ya Kikatoliki na Anglikana yenye historia kubwa ya kusisimua.
Nilifurahishwa na hali ya utamaduni wa dhahiri uliokuwa ukiweza kuuona bayana jijini mle hasa katika uvaaji wa kinamama, wakubwa kwa wadogo, wakiwa kwenye mavazi yao ya asili yaliyopendeza mno. Ni kama vile ukifika Tanga, ambapo idadi kubwa ya kinamama na wao huwa wamejitanda mabaibui.
Nikamkumbuka yule binti wa Kiganda ofisini pale RTD, Emilie na jinsi alivyokuwa na desturi zilizomilikiwa na tabia hizi za huku nyumbani kwao za mwanamke kuwa mnyenyekevu sana mbele ya mwanamume. Niliowaona wengi wao wakiwa vivyo hivyo mtaani mle.
Haikuwa ziara ya muda mrefu, kwani ilituchukua muda wa pengine saa mbili hivi, kisha tukarejea hotelini mwetu na kujituliza. Tulikuwa tukiisubiri kwa hamu kubwa siku inayofuata yaani siku yenyewe ya mechi ya fainali, siku ya kilele cha safari yangu ya kwanza nje ya Tanzania.
Naam, siku ya Jumamosi ikawadia. Ilikuwa siku nzuri kwa kila kitu. Jua la wastani na upepo hapa na pale. Jiji lilikuwa limejaa shauku kubwa. Shauku ya kushuhudia pambalo kali la mpira baina ya timu za taifa za nchi jirani, Uganda na Tanzania.
Tuliwasili kwenye Uwanja wa Nakivubo mapema -- yapata saa nane hivi – lakini tayari wakati huo uwanja ulikuwa umejaa “mpaka pomoni”. Mashabiki wa Uganda wakipiga kelele ama nisema mayowe, maana walikuwa kama wamepagawa. Nikajua hawa jamaa hawataki jambo jingine lolote kinyume cha matokeo ya kunyakua kombe!
Mayowe hayo yaliongezeka zaidi pale ilipoingia timu yao ya taifa, wakiwa kwenye sare zao maarufu za rangi za njano na nyeusi zenye michirizi ya rangi nyekundu.
Hali ilikuwa tofauti pale ilipoingia timu ya taifa ya Tanzania. Ukatanda ukimya wa aina yake uliojawa na hofu kwani kusema kweli timu hiyo nayo ilikuwa imejengeka vilivyo na haikuwa na masihara hata kidogo. Niliona fahari mno, nikajawa na matarajio makubwa ya mafanikio.
Ghafla, lile zogo la hoi hoi likavuma tena. Alikuwa anaingia mwenyewe Rais Idi Amin. Uwanja ukajaa nderemo na vifijo. Nikawa najiuliza kama ni kweli Waganda wale, pamoja na zahama zote hizi za huyu jamaa, ni kweli walikuwa wanampenda hivyo au walikuwa wanamvika kilemba cha ukoka tu? Nikaona nisiendelee kuwaza wala kuwazua.
Maana, mambo ya uwanjani yalikuwa ndiyo yameanza na mimi na mwenzangu Mshindo Mkeyenge tulikuwa sasa tumeingia kazini kuwapasha Watanzania kwa mamilioni kile kilichokuwa kinaendelea kwenye Uwanja wa Nakivubo.
Nilipata furaha kubwa kutangaza pambano langu kubwa la kwanza la mechi ya fainali ya kimataifa. Nikajua sasa nimekomaa. Nikafahamu kwamba kwa kweli ndoto yangu imetimia na kamwe sasa sitarudi nyuma.

Kama ilivyotarajiwa, mechi ile ilikuwa ya kusisimua sana. Kikosi cha Waganda kikiongozwa na Waswa, Omondi, Kulabingwa na jamaa ambaye mashabiki wa Uganda walimwita Mubiru “Tank” walilisakama lango la Taifa Stars kama nyuki tangu mwanzo, lakini mlinda mlango Omar Mahadh alikuwa imara mno.
Lakini, ghafla, upepo ukabadilika. Watanzania nao wakaja juu, ikawa sasa ni “vuta ni kuvute”. Ghalfa, uwanja ukawa kimya, Maulidi Dilunga aliweka chuma kimiani, nikapiga kelele zilizosikika sana pale uwanjani maana Waganda walipigwa na butwaa. Hawakuamini!
Baada ya goli hilo, Waganda nao wakapandisha mori, huku wakishangiliwa kwa nguvu zote. Idi Amin mwenyewe akiamka mara kwa mara kutoka kwenye kiti chake kwa shauku kubwa kila walipofanya kosa.
Hata hivyo, kukiwa kumebakia muda mfupi kufikia mapumziko mashambulizi hayo yalizaa matunda. Uganda walipata penalti na hivyo wakapata bao la kusawazisha. Hadi mapumziko Uganda 1 Tanzania 1. Mambo yakawa bado mabichi.
Lakini mara tu baada ya kipindi cha pili kuanza, haraka haraka Uganda ikapata bao la pili na licha ya Taifa Stars kupigana kufa na kupona wakiongozwa na nahodha Abdurahaman Juma, mambo hayakutengemaa tena. Mchezo ukamalizika kwa Uganda kupata ushindi wa mabao 2 kwa 1. Nikamuona Idi Amin amefurahi sana kupita kiasi. Nikajua na sisi tumepona. Jioni ile yeye mwenyewe akaandaa sherehe kubwa. Tukakaribishwa kunywa na kula na kucheza dansi na akina dada walioalikwa mahususi kutoka Chuo cha Wauguzi cha Mulago.
Tukasahau wasiwasi tuliokuwa nao. Jumapili tarehe 30 Septemba, tukaondoka Kampala, kurejea Dar, nikiwa na mengi zaidi ya kusimulia.
SIMULIZI NYINGINE ZA TIDO NI JUMAPILI IJAYO.
MWANANCHI

No comments: