ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, August 10, 2013

Mabinti waliomwagiwa tindikali wapelekwa UK

Watano washikiliwa Polisi, donge la mil. 5/- latangazwa
Wakati wasichana wawili raia wa Uingereza waliomwagiwa tindikali visiwani Zanzibar, wakisafirishwa kuelekea nchini kwao kwa matibabu zaidi, watu watano wanahojiwa na polisi kuhusiana na tukio hilo.
Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema serikali yake itahakikisha inawasaka na kuwafikisha mahakamani waliopanga na kufanya shambulio hilo.

Dk. Shein ametoa tamko hilo wakati akihutubia Baraza la Idd Fitr, kufuatia kukamilika kwa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani mjini Zanzibar.

Alisema vyombo vya ulinzi na usalama vitafanya liwezekanalo kuwatafuta na kuwakamata waliohusika kuwafanyia vitendo vya uhalifu raia hao.

“Serikali imesikitishwa sana na kitendo hiki, kimezua dhahama ndani ya nchi yetu na nje ya nchi yetu jambo ambalo hatukulilalia wala hatukuliamkia,”alisema Dk. Shein.

Hata hivyo, alisema serikali itaendelea kulinda misingi ya amani na kuwataka wananchi kushirikiana na vyombo vya ulinzi kuwafichua wahalifu wa vitendo vya aina hiyo kwa manufaa ya Zanzibar na wananchi wake.
Aidha, alisema kwamba kitendo hicho kinastahili kulaaniwa kwa sababu ni kinyume na utu na misingi ya haki za binadamu.

Alisema vyombo vya dola vitahakikisha vinafanya uchunguzi kwa umakini mkubwa ili kuepusha kuwakamata watu wasiokuwa na hatia katika tukio hilo.

“Hatutowadhulumu waliokuwa hawana hatia, lakini aliyehusika hatutomsamehe, sheria itafuata mkondo wake,” alisema Dk. Shein.



Akizungumza na NIPASHE, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Mkadam Khamis Mkadam alisema watu watano wanahojiwa na polisi kufuatia tukio la kumwagiwa tindikali wageni hao.

Alisema kuwa watu hao wameanza kuchukuliwa maelezo ya kusadia kufanikisha uchunguzi wa kuwatafuta wahusika wa shambulio hilo na kuwataka wananchi kusaidia kutoa taarifa za siri za kufanikisha kukamatwa kwa watu waliofanya kitendo hicho.

Mkadam alisema kwamba majeruhi wamechukuliwa maelezo yao jijini Dar es Salaam juzi na taarifa yao ilitarajiwa kutumwa Zanzibar jana ili kufanikisha kazi ya uchunguzi wa tukio hilo.

Wakati huo huo, akizungumza na waandishi wa habari, Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo , Said Ali Mbarouk ametangaza zawadi ya Sh. milioni 10 kwa watu watakaotoa taarifa za kupatikana wahalifu waliowamwagia tindikali raia hao.

Awali akizungumzia kuondoka kwa mabinti hao kwenda Uingereza, Kiongozi Msaidizi wa Kikundi cha Shirika la Arts in Tanzania, Bashir Ismail, ambalo wasichana hao walikuwa wenyeji wao, alisema walisafirishwa juzi usiku saa 3:00 kwa ndege ya kukodi kupelekwa Uingereza.

Akizungumza na NIPASHE Jumamosi jana, alisema hadi kufika jana saa 6:00 mchana wasichana hao watakuwa wamewasili nchini Uingereza na baada ya kufika huko watapelekwa hospitali kwa matibabu ya kina.

Wakati mabinti hao wakipelekwa nchini mwao, madaktari waliokuwa wakiwatibu wa Hospitali ya Aga Khan wamesema wasichana hao hawakuathirika sana kutokana na tindikali hiyo kutopenya zaidi katika miili yao.

Madaktari hao ambao walikuwa wakihojiwa na Shirika la Utangazaji la CNN, walisema kutokana na madhara kutokuwa makubwa ni wazi kuwa wakipelekwa nchini Uingereza watapona na kurejea katika hali yao ya kawaida.

Mabinti hao Kirstie Trup na Katie Gee, wote wenye umri wa miaka 18 kutoka London, walimwagiwa tindikali Jumatano wiki hii huko visiwani Zanzibar ambako walikuwa kwa ajili ya kujitolea kufundisha somo la Kiingereza katika Shule ya Msingi ya St. Monica inayomilikiwa na Kanisa la Angilikana Zanzibar.

Mama wa wasichana hao, Rochelle Trup na Nicky Gee, walieleza kusikitishwa na shambulizi hilo ambalo sababu yake haijajulikana hadi sasa na hivyo kuzua maswali mengi ndani na nje ya nchi.

''Tunashukuru kwa wale wanaotaka kujua kinachoendelea lakini tungeomba vyombo vya habari vituache kwa sasa hadi tutakapokutana na watoto wetu,'' walisema akina mama hao.

Tukio hilo la kinyama linakumbushia matukio mengine kadhaa ya kufanana nayo ambayo yameacha watu kadhaa vilema na vifo.

Kumwagiwa tindikali kwa Waingereza hao kumezua hofu na taharuki kubwa ndani na nje ya nchi na juzi Rais Jakaya Kikwete aliwatembelea majeruhi hao katika hospitali ya Aga Khan jijini Dar es Salaam walikohamishiwa kutoka Zanzibar na kulaani vikali uhalifu huo, huku akiviagiza vyombo vya dola kufanya uchunguzi na kuwakamata wahusika wote ili washitakiwe.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Mkadam Khamis Mkadam, akizungumza na NIPASHE juzi alisema tukio hilo lilitokea Jumatano saa 1:15 usiku mtaa wa Shangani eneo la mji Mkongwe wa Zanzibar, karibu na ofisi za serikali ikiwamo ile Wizara ya Sheria na Wizara ya Katiba na Maendeleo ya Ustawi wa Jamii, Wanawake na Watoto.

*Thobias Mwanakatwe, Dar na Mwinyi Sadallah, Zanzibar
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: