ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, September 3, 2013

KISIWA CHA SAA NANE CHA PANDISHWA HADHI NA KUWA HIFADHI YA TAIFA

Tumbili wapo wa kutosha tu kisiwani hapo.
Ofisi za wasimamizi wa hifadhi ya Taifa ya Saa Nane. Awali kisiwa hiki kilikuwa ni hifadhi lakini mwanzoni mwa mwezi wa Tisa mwaka huu, Bunge limekipandisha hadhi na kukifanya kisiwa hiki kuwa Hifadhi ya Taifa na kuwa chini ya usimamizi wa TANAPA.
Kisiwa cha Saa nane kinafikika kwa njia ya boti tokea jiji la Mwanza. Boti inayoonekana juu ndio iliyompeleka Mdau Abdul mpaka Kisiwa cha Saa Nane tokea Mwanza mjini.
Mdau Akiwa kwenye boti tayari kwa kuanza safari kuelekea Kisiwani. Hapa ni akiwa upande wa Mwanza mjini
HIFADHI ZA TAIFA TANZANIA
TAARIFA KWA UMMA


KISIWA CHA SAANANE CHATANGAZWA RASMI HIFADHI YA TAIFA


Kisiwa cha Saanane kimetangazwa rasmi kuwa Hifadhi ya Taifa kufuatia Tangazo la Serikali Namba 227 lililotolewa hivi karibuni.

Kutangazwa kwa Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Saanane kunafuatia kupitishwa kwa Azimio la Bunge mwezi Oktoba mwaka jana lililoridhia kupandishwa hadhi kwa kisiwa hicho kutoka Pori la Akiba na kuwa Hifadhi ya Taifa.

Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Saanane itakuwa na ukubwa wa kilomita za mraba 2.18 na itajumuisha maeneo ya lililokuwa Pori la Akiba , Visiwa vya Chankende kubwa na ndogo pamoja na eneo la maji ya Ziwa Victoria linalozunguka visiwa hivyo.

Kuanzishwa kwa Hifadhi mpya ya Taifa ya Saanane kutawezesha haja ya kuongeza spishi mbalimbali za wanyamapori na hivyo kuongeza utalii wa mjini, utalii wa ndani, utafiti na kutoa elimu kwa vitendo kwa wanafunzi na wananchi watakaotembelea hifadhi hii mpya.

Aidha, uamuzi huu utasaidia kutunza hali ya bioanuwai, uhifadhi wa mazalia na makuzio ya samaki na uendelezaji wa utalii wa mjini kuendelea kuimarika.

Kabla ya kupandishwa hadhi, Kisiwa cha Saanane kilikuwa Bustani ya wanyama mwaka 1964 kabla ya kupandishwa hadhi kuwa Pori la Akiba mwaka 1991. Ilipofika mwaka 2006, Serikali ilikikabidhi kisiwa hicho kwa Shirika la Hifadhi za Taifa kwa ajili ya kukiendesha na kusimamia mchakato wa kukipandisha hadhi kuwa Hifadhi ya Taifa.

Kufuatia uamuzi huu, Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) sasa litakuwa na jumla ya Hifadhi 16 nchi nzima ambazo nyingine ni pamoja na Serengeti; Ziwa Manyara; Tarangire na Arusha.

Nyingine ni pamoja na Kilimanjaro; Mkomazi; Saadani; Mikumi; Milima ya Udzungwa; Ruaha; Kitulo; Katavi; Gombe; Milima ya Mahale na Kisiwa cha Rubondo.

Wakati huohuo, eneo la Hifadhi ya Taifa Gombe limeongezwa ukubwa kutoka Kilometa za mraba 33.74 hadi kufikia kilometa za mraba 56. Uamuzi huu unatokana na Tangazo la Serikali Namba 228 lililotolewa hivi karibuni ambalo linafuatia Azimio la Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lililotolewa mwaka jana linalohusu kuridhiwa kwa uamuzi wa kurekebisha mipaka ya Hifadhi ya Taifa Gombe kwa kuondoa eneo la makaburi na kuliacha kwa wananchi pamoja na kujumuisha eneo la ufukwe wa maji ya Ziwa Victoria na eneo la ukanda wa maji.

Kuongezeka kwa eneo la ufukwe wa ziwa na ukanda wa maji kwenye eneo la hifadhi kutaongeza wigo wa shughuli za utalii katika Hifadhi kama vile kuogelea, utalii wa boti, mitumbwi na uvuvi wa kitalii.

Imetolewa na Idara ya Uhusiano
Hifadhi za Taifa Tanzania
S. L. P 3134
ARUSHA
03.09.2013

No comments: