ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, September 26, 2013

MBONA MAJANGA, MPUNGA WA MBEGU HAUMALIZI NJAA

SALAMU waleykumu wapenzi wa kona yangu mimi anti Naa, kwa uwezo wa Manani nina imani wote hamjambo wazima wa afya kama kuna wagonjwa basi tuwaombee na kama kuna aliyetangulia mbele ya haki vilevile tumuombee apokelewe kwa amani pia apate huruma ya Muumba.
Jamani leo nataka kuzungumza na wazazi, watu wazima wenzangu. Kwa vile ni watu wazima tutazungumza kwa lugha ya kiutu uzima lakini vikinipanda mtaniwia radhi kwa vile siwezi kuuzuia mzuka kama chafya ikija lazima niiachie.
Nataka kuwauliza wazazi wenzangu, hivi mnapoamua kuwaachisha shule watoto wenu mnamaanisha nini? Au wanaume wa kuwaoa wamekwisha, kwa hiyo anayetokea mnawahi hata bila kuangalia unaharibu kwa kiasi gani maisha ya mwanao.
Jamani hivi kweli tuna akili timamu zinazotufanya watoto na wajukuu zetu watutegemee? Unamuoza mtoto wa miaka kumi na nne ili akafanye nini kwa mwanaume pengine unampeleka kwa zee la miaka 70 kwa vile ana vijipesa.
Wazazi wenzangu, hivi watoto wetu wa kike tunawaonaje? Kukaa nao tunaona sawa na kufuga bomu, ambalo tunawahi kulitupa ili wakalipukie mbali.
Hivi nani aliwaambia watoto wetu wakiolewa tutamaliza matatizo yetu? Hatujui kumnyima elimu mtoto ni sawa na kumuondoa macho. Kwa vile umemuoza hajui lolote lazima nyumba itamshinda na kurudishwa nyumbani.

Hebu jamani tuangalie ukatili tuliowafanyia watoto wetu, tumewanyima elimu wakati huohuo tumewachanganya kisaikolojia. Matokea yake mtoto anaingia kwenye ukahaba anakosa aibu kwa vile tayari kalaaniwa kwa kutembea na babu yake.
Tunajua kila mtu anapenda kuona binti yake anaolewa, lakini si kwa ukatili tunaoufanya kuwauza kama makinda ya kuku kwa wauza chipsi bila kujali kama yamekomaa, wewe unajali fedha kuliko afya za watu.
Unawahisha kumuoza mtoto kwa sababu gani? Amekuwa mzigo kwako na kuamua kuutoa kwa kuutupa ovyo? Jamani wazazi ninyi ndivyo mlivyoozwa na wazazi wenu? Tusiendekeze njaa nani alikuambia mpunga wa mbegu unamaliza njaa. Hebu tuheshimu haki za wanetu tuwe wakali kwa wanaume wanaowafuata watoto wetu wadogo ili kuwaoa, amini hao hawana nia nzuri.
Hao ni waharibifu, inakuwaje mtu akitembea na binti yako mdogo unashtaki amebakwa lakini wewe unampeleka mwanao kwa mbakaji kwa ajili ya kukupa fedha ambayo matumizi yake hata mwezi hayafiki?
Tuache kuendekeza njaa, hebu tukae na mabinti zetu tuwakomaze ili wakiingia kwenye ndoa waingie na akili timamu ya kuweza kukabiliana nayo.
Na ninyi mibazazi mliokosa haya wala hamjui vibaya, hamuwaoni wanawake wote wanaozurura na kuzunguka kwa waganga kutafuta ndoa, mnawafuata watoto wadogo tena wa shule, wewe ni sawa na muuaji kwa vile unamuharibia maisha yake, unamchakaza kisha unamkimbia na kusababisha kuongezeka watoto wanaoishi maisha magumu.
Hivi tuna akili? Tunakula mpunga wa mbegu tumechoka kulima? Jamani serikali mpo wapi? Wizara ya wanawake na watoto hamuoni? Na nyinyi walimu wa kiume, jamani mbona mmekuwa majanga, mwanafunzi akitoka viziwa halali yenu.
Sasa tuwapeleke wapi watoto wetu? Baharini papa na nyangumi, mtoni mamba, porini simba, nyumbani wazazi na shuleni walimu.
Jamani mtoto wa kike aende wapi? Mbona kila kukicha wanakosa raha. Shida zenu, muwaoze wao mbona majanga! Yangu yameisha heshimuni haki za watoto wa kike.

Kwa leo inatosha japo watu wazima nyuso zimewashupaa hawana hata chembe ya aibu. Makavu yamefika, ni mimi Anti Nasra Shangingi Mstaafu.
GPL

No comments: